Wabia serikalini ‘PPP’ walioweka kambi Dodoma 2021 kueneza Kilimo

23Jul 2021
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Wabia serikalini ‘PPP’ walioweka kambi Dodoma 2021 kueneza Kilimo

KITAIFA kuanzia sera hadi falsafa ‘Kilimo ni Uti wa Mgongo.’ Ndio imeushika uchumi wa taifa. Utekelezaji wake unagusa mtazamo wa sura mbili, ubia katika serikali na sekta binafsi, kupitia sheria maalum inayojulikana kwa kifupi PPP (Ubia wa Sekta Binafsi na Umma).

Moja ya shughuli za maonyesho ya kilimo yaliyofanywa na PASS Trust. PICHA: MTANDAO.

Hapo katika mlango wa sekta binafsi, ndipo inapopatikana taasisi ya Pass Trust iliyojikita katika utekelezaji kilimo nchini, kusaidia kuwainua wajasiriamali wa sekta ya kilimo, mtazamo uwe wa kibiashara.

Pass Trust, ilianzishwa kwa ushirikiano wa serikali za Tanzania na Dermark miaka 20 iliyopita, lengo ni kuwezesha upatikanaji huduma za kifedha na biashara kwa bidhaa na huduma katika sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini

Dhima kuu ilijikita katika kupunguza umaskini, huku ikiwezesha upatikanaji mitaji kwa wakulima, yenyewe ikijikita jukumu la udhamini.

Imekuwa ikiwezesha mikopo wastani wa asilimia 20 hadi 80 kwa wanawake, ikiwa ni njia ya kuongeza dhamana ya kuwawezesha wateja kupata mikopo hiyo na katika hilo, Pass hadi sasa inafanya kazi na benki 14 zilizopo nchini kwa mkataba maalum.

Pia, asasi hiyo inatoa huduma za ukuaji biashara kama vile mafunzo ya ujasiriamali, upembuzi yakinifu wa miradi husika, unaosaidia wateja kuandaa maandiko ya miradi bora ya uwekezaji.

Mikakati iliyopo ni kwa taasisi inalenga kusaidia sekta ya kilimo kuwasaidia wajasiriamali, kuwainua kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ya pembejeo, zana za kilimo na ufugaji na zinazosaidia kuendeshea ujasiriamali.

Hadi sasa PASS imeshadhamini miradi ya wajasirimiali 46,300, huku kuna wajasiriamali million 1.7 wanaonufaika na udhamini huo, pia fursa za ajira.

MKURUGENZI PASS

Anna Shanalingigwa, ni Kaimu Mkurugenzi wa asasi ya PASS, anasema ilianzishwa mwaka 2000 na hadi sasa imeshadhamini miradi 46,300 wenye thamani ya Sh. trilioni moja na kuna wajasiriamali milioni 1.7 waliokwishanufaika na udhamini huo.

Mkurugenzi huyo anasema, asilimia 45 ya wanufaika hadi sasa ni wanawake, pia ajira sasa imefika watumishi milioni 2.5.

Kwa nini jijini Dodoma?

Anna anaimbia Nipashe kwamba wako katika mzunguko wa kutoa huduma ya kilimo na upatikanaji fedha za kuchochea ukuaji wa kilimo biashara nchini na wameandaa maadhimsho yaitwayo ‘Wiki ya PASS’.

Ni tukio linalowaleta pamoja wakulima wauzaji zana za kilimo, pembejeo, taasisi za fedha, viongozi wa serikali na wachakataji, wakutane kujadili kupatikana fedha za kuchochea ukuaji kilimo biashara.

Pia, anamtaka kuwapo kampuni ya PASS Leasing inayojihusisha na mikopo ya kilimo bila ya dhamana kwa wakulima ngazi zote: Wadogo, kati, wakubwa na vikundi mbalimbali, lengo ni kukuza mnyonyoro wa thamani ndani ya kilimo.

DC DODOMA

Jabir Shekimweri, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, akizungumzia katika Wiki ya PASS Trust inayofanyika katika viwanja vya Nyerere Sguare, anasema asasi PASS Trust ina fursa ya kuwekeza katika zao la zabibu, yenye faida kubwa.

Rai yake Shekimweri ni kwamba, ufike wakati wakulima wafanye kilimo chenye tija, kwani mwelekeo uliopo sasa ni jamii kujikita zaidi katika kilimo biashara, hivyo anasogeze wito hadi kwa wafugaji, wavuvi na wajasiriamali katika mnyonyoro wa thamani wa kilimo

WAKULIMA NA YAO

Mkulima Japhet Lusita, anaeleza matarajio yake kwamba taasisi hiyo itasaidia hasa katika miongozo, hasa ya kutoa mikopo ya zana za kilimo, akiamini ni moja ya maeneo yatakayowasaidia kwa kiasi kikubwa wakulima kuinuka na kusonga zaidi katika dhima wanayoielekeza, kilimo biashara.

Sura tofauti ya matarajio ni kunufaika na mikopo. Anaongeza:“Hii itatusaidia wakulima wengi kupata fursa nyingi kutoka katika taasisi hiyo na wataalamu wa sekta ya kilimo ambao watakuwapo.”

Lusita anafafanua kwamba, maadhimisho hayo yaliyofanyika Nyerere Square, ni fursa yao kukutanisha wakulima kutoka maeneo mbalimbali, kwa ajili ya kuwaelekeza namna fursa za kilimo zilivyo.

Habari Kubwa