Wabunge hamkuiona sheria ya mafao inayominya wastaafu ?

25Nov 2018
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wabunge hamkuiona sheria ya mafao inayominya wastaafu ?

MOJA ya taarifa zilizotengeneza vichwa vya habari hivi karibuni ni ile iliyoandikwa na Nipashe ya kila siku, kuhusu kanuni na sheria moja ya hifadhi ya jamii ilivyoainisha mafao kwa ajili ya wastaafu, wategemezi na warithi

Habari hiyo iliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti la kila siku na ndipo iliendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala hasa katika kipengele cha kiasi ambacho mstaafu atalipwa kwa ujumla baada ya kustaafu na kile kitakachobaki kwenye mfuko.

Kwa mujibu wa kanuni hiyo mstaafu atalipwa malipo ya mkupuo ya asilimia 25 na asilimia 75 inayobaki italipwa kama mshahara kwa kipindi chote cha maisha yake.

Wasimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii yaani Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), imefafanua kuwa, lengo la kubaki kwa fedha hizo ni kumsaidia mstaafu kuishi vizuri kwa kuendelea kupata fedha ambazo zinasaidia maisha yake, kuliko kumpa zote ambazo huenda akazitapanya na kurudi katika umaskini.

Siku kadhaa baada ya habari hiyo kuandikwa aliibuka Waziri Kivuli (Ofisi ya Waziri Mkuu) wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Esther Bulaya, aliyeeleza kuwa kikokotoo hicho kinawaumiza wastaafu na hakikujulikana kwa wabunge.

Mbunge huyo ambaye ni wa jimbo la Bunda Mjini (Chadema), hakuwahi kusikika kufafanua kikokotoo hicho hadi ilivyoandikwa na Nipashe na kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linanifanya nijiulize kuwa kwa wakati huo wote hakuwa ameona kanuni hizo?

Anachoeleza mbunge huyo ni kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani haikukubaliana na sheria hiyo hadi watakapoona kikokotoo kilivyo kwa kuwa ndicho kinagusa maslahi ya Watanzania wengi, lakini kiliachwa mikononi mwa serikali.

Nimejikuta nawaza kwa sauti kuwa wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi, ndiyo wanaotunga sheria ambazo zinakwenda kuwang’ata wao baada ya kustaafu na jamii zao ambazo ni wapiga kura na Watanzania wote.

Waliotunga sheria hii hata kama hawakuona kikokotoo ni wabunge ambao waliridhia kuwa wastaafu wasipewe mafao yao yote kwa mkupuo bali kuendelea kulipwa kidogo kidogo kwa muda wa maisha yao uliobaki.

Wakati wakiamua hivyo wao wanapomaliza muda wa utumishi wao wamejipa ahueni kuwa wanapokea kilichokuwa chao na kuendelea na maisha, lakini kilichoumiza zaidi kwa sasa ni kwa jinsi ambavyo fedha nyingi itabaki na wastaafu kuambulia ‘kiduchu’.

Haijulikani moja kwa moja nini kiliwasukuma wabunge kufanya maamuzi haya kwa niaba ya wawakilishi wao, lakini malipo ya jumla ni madogo sana kwa mstaafu kwa kuwa hataweza kufanya miradi ambayo itamuwezesha kuendelea na majukumu mapya.

Kipato cha watumishi wengi wa kada za chini ni kidogo, hivyo anapostaafu na kupewa fedha hizo ndiyo anakwenda kumalizia ujenzi au kuanza nyumba, hivyo kwa malipo haya ya sasa maana yake hataweza kujenga au kufanya uwekezaji wowote bali kuishi kwa masononoko kwa maisha yake yaliyobaki.

Ni vyema wabunge wanapopelekewa sheria kuzisoma kwa kina na kuomba ushauri wa wataalamu, ili wanapopitisha sheria flani isiwe ni kwa vile upande flani unazungumzia kinyume chake bali ni kwa jinsi gani maslahi ya wananchi yamelindwa.

SSRA ilitoa mfano wa mtu aliyestaafu na mshahara wa Sh. milioni 1, ambaye mshahara wa kila mwezi utakuwa 557,000, lakini hebu tujiulize ni Watanzania wangapi wanastaafua wakiwa na kiwango hicho? Kwa wanaolipwa chini ya hapo maana yake mshahara utakuwa mdogo na wapo ambao watalipwa Sh. 100,000 kwa mwezi.

Kwa maisha ya sasa ambayo kila siku gharama za uendeshaji zinapanda ni mstaafu gani atakayeweza kuendesha maisha ya kutumia Sh. 100,000 kwa mwezi? Matokeo yake mstaafu huyu atafariki kwa msononeko na kuacha fedha zake nyingi kwenye mfuko, ambazo zitaendelea kulipwa kwa warithi wake kwa miaka mitatu yaani miezi 36 pekee.

Ni vyema wabunge waliopewa nafasi ya kuwakilisha wananchi wanapotunga sheria wasiangalie maisha yao na familia zao au marafiki, bali Watanzania wote wenye maisha ya viwango tofauti ili kuepusha mambo kama haya ya sasa ya usononeko kwa walio wengi.

Naamini muswada wa sheria hii uliandaliwa na wataalamu na walikuwa na sababu ya kuweka kikokotoo hicho lakini walisahau kuwafikiria watu wenye mishahara midogo na matokeo yake waliifikiria kada ya juu ambayo inanufaika moja kwa moja kwa kuwa mishahara minono.

Katika kikokotoo hicho lipo suala jingine la faida anayopata mwanachama kulingana na uwekezaji aliofanywa na mfuko kwa kutumia fedha zake, ukipiga hesabu vyema ni fedha ndogo ambayo mstaafu anaipata licha ya kwamba fedha yake imehifadhiwa kwa miaka 60.

Nafikiri ipo haja ya kuifanyia mapitio sheria hiyo na kurekebisha baadhi ya maeneo ili kuhakikisha inawaangalia wastaafu wote ikiwamo wale wa kada za chini kuliko kuwa na sheria ambayo inapendelea waajiriwa wenye mishahara minono pekee. Tutafakari sote ……

Habari Kubwa