Wabunge waache uhasama kivyama

18Jun 2016
Nipashe
Wabunge waache uhasama kivyama

Kama moja kati ya mihimili mitatu ya dola, Bunge lina nguvu ya umma kwani ni Watanzania kwa ujumla waliokusanyika kwa kuwakilishwa ukumbini humo kujadili masuala muhimu katika ustawi wa nchi.

Lakini Bunge la sasa linakabiliwa na changamoto kubwa ya mgawanyiko.

Ikumbukwe wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) wana jeraha la uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ambao waliususia, na Ukawa, muungano wa vyama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi uliokusanya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi pia wana vilio vyao kadhaa kisiasa.

Kwa upande wa pili, wabunge wa chama tawala, CCM, ni kama bado wapo kwenye sherehe za ushindi wa chaguzi zote mbili za Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa msingi huo, Bunge la 11 lina hisia mchanganyiko, pengine za kutosha kuzua uhasama na chuki, kwa itikadi za kivyama.

Uhasama huu wa kisiasa unahitaji Spika Job Ndugai na Naibu wake, Dk. Tulia Ackson, kuliongoza kwa kuleta maridhiano na kuepusha misimamo ya kichama ambayo inaongeza uhasama.

Ni uhasama ambao ulionekana kuanzia Bunge Maalum la Katiba, wakati wa uzinduzi wa Bunge la sasa na hata katika vikao vya mkutano wa Bajeti ambapo Kambi Rasmi ya Upinzani imeamua kumsusa Naibu Spika.

Wapo baadhi ya wataalamu wa siasa kama Ted Gurr na Monty Marshall, wanaoona kuwa mara nyingi uhasama na mitafaruku kwenye nchi nyingi za Kiafrika inatokana na mchanganyiko wa umaskini na udhaifu wa vyombo inavyoshughulikia amani na demokrasia.

Bunge ambalo ni mhimili wa kudumisha demokrasia halikustahili kukandamiza demokrasia.Linatakiwa kuwa muhimili usiojiegemeza kwenye kuadhibu na kubana zaidi wawakilishi wa wananchi.

Spika na Naibu wanapokutana na changamoto bungeni hawana budi kutafuta namna bora ya kuunganisha wabunge na kuleta usuluhishi, badala ya kukuza mgogoro na kutoa maamuzi ambayo hayaleti umoja na mshikamano bungeni humo.

Ukiangalia kinachoendelea bungeni sasa, baina ya Spika na wabunge wa Ukawa, utaona kuwa ni msingi wake uhasama baina ya CCM na Ukawa. Inaonyesha jinsi ile hali ya kutokubaliana kimisimamo ya kivyama inavyoshamiri ndani ya vyama hivyo mpaka bungeni kiasi cha kuathiri jukumu la mhimili huo muhimu.

Ni wakati wa kiti cha Spika kuchukua hatua na kuja na maamuzi ya kizalendo ya kupunguza mikwaruzano ndani ya Bunge. Viongozi hao wawili wafahamu kwamba kama hali ikiachwa iendelee itaongeza maswali kuhusu weledi wa uongozi na taratibu za kuendesha na kukisimamia chombo hicho cha kukosoa, kusimamia serikali pamoja na kutunga sheria.

Upinzani baina ya CCM dhidi ya Ukawa pamoja na misimamo ya kichama imekuwa ndiyo ‘dira’ kuu ya matatizo ya chombo hicho, kiasi cha kulifanya Bunge kuwa la kichama zaidi, tena lililojaa kukomoana, kutunishia misuli ya ubabe, kujibu mapigo badala ya kuleta suluhu na maelewano.

Kwa upande mwingine uhasama huo wenye dharau na kutokukubali kutafuta suluhu unatishia hatima ya majukumu ya taasisi hii ambayo haijitambulishi kama ya uwakilishi wa wapiga kura, bali kundi la watu wenye nguvu na wasiokuwa na nafasi ya kushirikiana ama kupokea au kusikiliza wazo kutoka kwa wengine wasiounda serikali.

Kujitenga huko si uzalendo, kunawafanya wapinzani kuichukia Tanzania na kuona kuwa hawapewi nafasi licha ya katiba kuruhusu kuwapo kwa mawazo tofauti na upinzani kwa nia ya kutimiza wajibu wa kuisimamia serikali.

Bunge letu ni lazima likubali kuwa kuna kushindana, kubishana na kutokukubaliana lakini kwa manufaa ya nchi, tena kunakoongeza uzalendo. Wabunge wafahamu kuwa kuna mamlaka iliyo kuu nayo si Spika wala Naibu ama kanuni bali ni hekima, kuridhiana, kuheshimiana, kujadiliana, kuvumiliana na kusameheana.

Kama wangezingatia hayo wapinzani wasingeendelea kumkimbia Naibu Spika nje ya ukumbi wa Bunge. Hata pale alipofungua semina, hawakutaka kujihusisha naye. Huko ni kukosa nidhamu na uvumilivu wa kisiasa, kutokuheshimiana na kukosa hekima.

Wapinzani wakitaka kushinikiza jambo wanaweza kususia lakini isiwe ndiyo utaratibu kila mara kususia Bunge.
Kuko wapi kukomaa kisiasa kunakoruhusu masuala usiyoyapenda na kuyasimamia yaende pamoja na yale unayoyaunga mkono na kuyatetea?

Ni wazi kuwa wabunge wa CCM na wa upinzani wana jukumu la kuondoa umaskini na hali duni ya maisha ya Watanzania na hilo ndilo wanalotakiwa kulipigia kelele kila siku.

Kuna wabunge wengi ndani ya CCM wakiwa na fikra kama walizo nazo Ukawa za kutaka kubadilisha kasoro za kiungozi na kiutendaji ili kuondoa ubadhirifu, ukandamizaji wananchi na kwa ujumla kuleta maendeleo kwa Mtanzania. Lakini ukweli ni kwamba upinzani ni fikra na utendaji unaotaka mabadiliko.

Aidha, haipendezi kuwatenga wapinzani mathalani kuwafukuza wasishiriki vikao vya Bunge vya vipindi viwili au kuwatimua wasihudhurie Bunge la bajeti na tena kufikia maamuzi ya kuwanyima posho bila hata kupeana maonyo. Athari zake ni kuwafanya wasisikike.

Kadhalika kukataa hoja zao, hata kama zina mashiko ni kuendelea kuotesha mbegu za uhasama ndani ya Bunge ambalo ndicho chombo cha uwakilishi, kinachosikiliza kila kilio cha mpiga kura na kufuatilia iwapo serikali inakitatua.

ANGALIZO
Nje ya Bunge, wakuu wa mikoa, madiwani wa CCM wakubali kushirikiana na viongozi wengine wa Ukawa ndani ya halmashauri. Pia wanasiasa kwa ngazi zote waache kuudharau upinzani na kuuona kama haustahili kuwapo na kufikiria mbinu za kuumaliza.

Wapinzani nao waache kuongeza mipasuko ya kisiasa ambayo haina sababu wala haikustahili kukuzwa na kuwa migogoro ya kitaifa, kama ambavyo ilitokea kususiwa kwa Bunge la Katiba ambako kulisababisha katiba pendekezwa kuandaliwa bila kuwa na muafaka wa kisiasa wa kitaifa.

Hata sasa, warudi bungeni na kutafuta suluhu badala ya kikimbia kila wanapomuona Naibu Spika.Lakini pia, ni wakati wa kufikiria kuwa na chombo cha maspika wa zamani, kinachohusisha viongozi na watu wanaoheshimika kwa ajili ya kulishauri Bunge kunapotokea sintofahamu inayosababishwa na migongano baina ya wapinzani na chama tawala.

Hili litasaidia kuondoa matatizo yanayotokana na kanuni kwa vile nazo zina mtizamo wa kichama. Zimeandaliwa na kupitishwa na wabunge wa CCM , hivyo zinaakisi matakwa ya walio wengi kwa manufaa yao. Hivyo haziwezi kutumiwa na kukubalika katika mazingira ya vyama vingi. Hata kama leo, zinaongoza lakini wakati mwingine zinapwaya kama ilivyotokea sasa.

Kamati hiyo ama chombo cha kulishauri Bunge inatakiwa kushughulikia zaidi chanzo na jinsi ya kumaliza tatizo badala ya kukimbilia kuadhibu zaidi kwa kuangalia kanuni na sheria ambazo zinaweza kuwa na upungufu kama ambavyo imethibitika.

Wakati mwingine kitengue adhabu kama za kuwafukuza wabunge bungeni, kuwanyima posho na kuwatoa nje ya ukumbi wa Spika kwa kuwadhalilisha, taasisi hii ya demokrasia iakisi demokrasi na si vinginevyo.Chombo hiki kiundwe kwa kuboresha sheria pamoja na kanuni za Bunge hilo.

Habari Kubwa