Wachezaji 10 waliofunga penalti nyingi mwaka 2020

18Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wachezaji 10 waliofunga penalti nyingi mwaka 2020

WAKATI soka lilitupa mambo mengi ya kuzungumza kwa mwaka 2020, moja ya topiki kubwa ambayo hatuwezi kuiacha ni VAR, athari yake na matokeo hasa kwa kutoa penalti.

Kutokana na uiamuzi wake, VAR ilijadiliwa kwa kipindi cha mwaka mzima. Kulikuwa na nyakati timu zilibahatika na nyingine kulia.

Julai 2020, Ligi Kuu Italia, Serie A, ilishuhudia msimu uliovunja rekodi kwa penalti nyingi.

Msimu wa 2018-19, jumla ya penalti 122 zilipatikana kwenye ligi hiyo. Lakini msimu uliofuata, idadi ilipaa hadi kufikia penalti 152 baada ya kila timu kufikisha mechi 30. Rekodi ya penalti nyingi 140 iliwekwa msimu wa 1949-50 kwenye Serie A.
Sawa na ligi nyingine, penalti nyingi zilitolewa kwa mwaka huo.

Makala haya inakuchambulia wachezaji waliofunga penalti nyingi zaidi katika ligi tano kubwa za Ulaya mwaka 2020.

#10. Andrej Kramaric (1899 Hoffenheim/Croatia) – Penalti 7

Mchezaji wa 1899 Hoffenheim, Andrej Kramaric amecheza mechi 166 kwenye mashindano yote kwa klabu yake, lakini tayari ndiye mfungaji bora katika historia ya klabu hiyo, akiwa na mabao 83 kwa jina lake. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, alifunga mabao 25 katika mechi 36 kwa klabu.

Kwa mwaka 2020, raia huyo wa Croatia alifunga penalti saba, tano alifunga kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, moja kwenye Ligi ya Europa na moja kwenye Kombe la DFB-Pokal.

#9. Mohamed Salah (Liverpool/Misri) – Penalti 7

Mohamed Salah ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Liverpool kwa kiwango kisichoshuka. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, amefunga mabao 111 katika mechi 177 kwa klabu hiyo.

Mwaka 2020 ulikuwa muhimu kwa Liverpool, ambapo kwa mara ya kwanza walitwaa taji la Ligi Kuu England kwa kipindi cha miaka 30. Salah alikuwa nguzo muhimu zaidi wakati Liverpool wakibeba taji hilo, huku akifunga penalti saba.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri, ameanza msimu wa 2020-21 kwa kasi kubwa, akifunga mabao 17 katika mechi 25, huku mabao sita yakiwa ya penalti.

#8. Neymar (Paris Saint-Germain/Brazil) – Penalti 8

Neymar amefunga mabao mengi na penalti kwa kipindi chake cha uchezaji. Mambo hayajawa tofauti pale Paris Saint-Germain pia, nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, amefunga mabao 79 katika mechi 97 kwenye mashindano yote licha ya muda mwingi kukabiliwa na majeraha.

Katika mabao yake 320, alifunga kwa jina lake hadi sasa, 50 ameyafunga kwa penalti. Mwaka 2020, Neymar alifunga penalti nane – sita kwa PSG na mbili kwa Brazil.

#7. Lucas Ocampos (Sevilla/Argentina) – Penalti 9

Lucas Ocampos alikamilisha uhamisho wa kwenda Sevilla, Julai mwaka 2019. Msimu wa 2019-20 ulimfanya yeye kufunga mabao 17 katika mechi 44 kwenye mashindano yote yakiwa mengi zaidi kwa msimu mmoja, huku matano kati yake yakiwa ni ya penalti.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 raia wa Argentina, amefunga mabao manne kwa msimu unaoendelea wa 2020-21, huku manne akifunga kwa penalti.

Kwa ujumla, Ocampos amefunga penalti tisa kwa mwaka 2020, na zote akiwa na klabu (nane kwenye LaLiga na moja kwenye mchezo UEFA Super dhidi ya Bayern Munich).

#6. Jordan Veretout (AS Roma/Ufaransa) – Penalti 9

Baada ya kucheza kwa mkopo kwa mwaka mmoja pale AS Roma, Jordan Veretout alijiunga kwa mkataba wa kudumu wa miaka minne na klabu hiyo Julai mwaka jana.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, kwa sasa amecheza mechi 59 kwa klabu hiyo ya Serie A kwenye mashindano yote na kufunga mabao 15.

Mabao 11 kati ya hayo alifunga kwa penalti. Mwaka jana Veretout alifunga mabao 13, tisa kati yake kwa penalti.

#5. Lionel Messi (Barcelona/Argentina) – Penalti 9

Lionel Messi kwa sasa anaonekana kama anaelekea mwisho. Hata hivyo, mfungaji huyo wa wakati wote wa Barcelona bado ni mchezaji muhimu kwa timu.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33, amefunga mabao 45 katika mechi 65 zilizopita kwa Barcelona, ametoa pasi za mwisho 33 kwa kipindi hicho.

Mwaka 2020, raia huyo wa Argentina alifunga penalti nane kwa Barcelona (tano kwenye LaLiga na tatu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja kwa Argentina.

#4. Romelu Lukaku (Inter Milan/Ubelgiji) – Penalti 10

Romelu Lukaku, ambaye amefunga penalti tatu msimu huu, anaonekana kama mchezaji muhimu zaidi kwa Inter Milan tangu alipotua hapo akitokea Manchester United. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, amefunga mabao 50 katika mechi 71 tu kwenye mashindano yote kwa klabu hiyo.

Kwa msimu huu 2020-21, Lukaku amefunga mabao 16 katika mechi 20 pekee kwa Inter, huku mabao matatu yakiwa ya penalti.

Alifunga penalti 10 mwaka 2020 – nane kwa Inter Milan na mbili kwa Ubelgiji.

#3. Ciro Immobile (Lazio/Italia) – Penalti 14

Tangu alipojiunga na Lazio Julai 2016, Ciro Immobile amekuwa mmoja wa mastraika wenye kiwango cha juu duniani.

Kwa sasa yupo katika msimu wake wa tano na klabu hiyo, na nyota huyo mwenye umri wa miaka 30, amecheza mechi 196 kwenye mashindano yote na amefunga mabao 141.

Kwa kipindi chote cha kucheza soka, Immobile amefunga mabao 219 katika mechi 391, huku 55 kati yake ni kwa penalti. Mwaka 2020, mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia alifunga penalti 14 na zote kwa klabu.

#2. Bruno Fernandes (Manchester United/Ureno) – Penalti 15

Bruno Fernandes alijiunga na Manchester United Januari 2020 kwa ada iliyoripotiwa kuwa euro milioni 80. Katika miezi 12, amethibitisha kwamba ni usajili bora zaidi uliofanywa na klabu hiyo.

Katika mechi 47 alizowachezea 'Mashetani Wekundu' hao kwenye mashindano yote, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, amehusika katika mabao 44, akifunga 27 na kutoa pasi za mwisho 17 na kwa sasa ni mchezaji muhimu kwa timu.

Mwaka 2020, alifunga penalti 15 kwa Manchester United (tisa kwenye Ligi Kuu, mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, tatu kwenye Ligi ya Europa na moja kwenye Kombe la FA).

#1. Cristiano Ronaldo (Juventus/Ureno) – Penalti 17

Inawezekana kweli Cristiano Ronaldo asiwapo kwenye orodha hii? Mshindi huyo mara tano wa Ballon d'Or yupo kwenye msimu wa tatu na klabu yake ya Juventus na tayari ameshaweka rekodi kadhaa.

Alimaliza msimu wa 2019-20 akiwa na mabao 37 kwenye mashindano yote katika mechi 46 mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwa msimu mmoja kwa Juventus.

Katika msimu huu unaoendelea, raia huyo wa Ureno tayari amefunga mabao 18 katika mechi 16 pekee.

Kwa sasa amefikisha mabao 758 kwa klabu na nchi yake. Ronaldo amefunga jumla ya penalti 133 kwa klabu na timu ya taifa.

Mwaka 2020, nahodha huyo wa Ureno alifunga penalti 17, zote kwa Juventus (13 kwenye Serie A, tatu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja kwenye Coppa Italia).

Habari Kubwa