Wachezaji 11 waliotisha Chalenji wanawake

02Dec 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wachezaji 11 waliotisha Chalenji wanawake

MICHUANO ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ilimalizika Jumatatu iliyopita (Novemba 25, mwaka huu), kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini, Dar es Salaam kwa Kenya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza.

Mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake, Mwanahamisi Omari 'Gaucho' wa Kilimanjaro Queens, (kushoto), akipambana kuwania mpira dhidi ya beki wa Kenya, wakati wa mechi ya fainali ya michuano hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex. Kenya ilishinda mabao 2-0. PICHA: MAKTABA.

Kenya ilibuka kidedea baada ya kuwafunga wenyeji Kilimanjaro Queens ya Tanzania Bara, mabao 2-0 katika mechi ya fainali.

Ni michuano iliyokuwa na msisimko wa aina yake, mashabiki wakijazana kwa wingi tangu ilipoanza kutimua vumbi Novemba 16, mwaka huu, mechi zote zikichezwa kwenye uwanja huo huo.

Jumla ya michezo 16 ilichezwa hadi fainali, ikishuhudia magoli 85 yakifungwa hadi kumalizika kwa michuano hiyo.

Hat-trick saba zimepigwa na wachezaji mbalimbali kwenye michuano hiyo, wakati penalti sita zilipatikana.

Mabingwa wapya Kenya, ndiyo timu iliyoondoka bila kufungwa hata goli moja, huku Zanzibar na Djibouti zikiwa zimeondoka kwenye michuano hiyo bila goli lolote.

Baada ya michuano hiyo kumalizika, mwandishi wa makala haya amekusanya majina ya wachezaji 11 bora walioonekana kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na kustahili kuunda kombaini ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

 

1. Annedy Andey-Kenya

 

Ndiye kipa bora wa michuano hiyo mwaka huu. Mpaka michuano hiyo inamalizika na kuiwezesha timu yake kutwaa ubingwa hajaruhusu wavu wake kuguswa.

Ni golikipa wa viwango vya juu, kwani ukianzia umbo ni mrefu, ana nguvu mikononi kiasi cha kudaka mashuti makali bila kutema, kitu ambacho kinawashinda makipa wengi wa kike.

 

2. Happyness Mwaipaja-Kili Queens

Ni beki wa kulia wa Kilimanjaro Queens, aliyecheza vema sana kwenye michuano hiyo iliyomalizika na anastahili kuwamo kwenye kikosi hiki, licha ya kasoro ndogo kwenye mechi ya fainali kushindwa kumkaba vema mchezaji hatari wa Kenya, Jentrix Shikangwa na kusababisha magoli yote mawili yaliyotokea upande wake.

 

3. Nally Sawe-Kenya

 

Beki huyu wa kushoto ameonyesha uwezo wa hali ya juu akiwa mgumu kupitika, mwenye uwezo na nguvu na akili ambazo zimeifanya beki wa Kenya kutopitika ovyo.

 

4. Amina Ally- Kili Queens

 

Beki wa kati maridadi kabisa anayecheza kwa kutumia akili zaidi kuliko nguvu. Ana "kontroo" ya hali ya juu na uwezo wa kumiliki mpira, kutoa pasi za uhakika kiasi cha mashabiki wengi kumshangilia kila anapochukua mpira.

Wengine wanadai angechezeshwa namba nane kutokana na uwezo alionao.

 

5. Dorcus Nixon-Kenya

 

Moja ya faida ya wachezaji wa Kenya ni warefu na wana fikizi ya hali ya juu, hasa mabeki.

Dorcus ni mmoja wa mabeki wa kati ya Kenya mrefu na mwenye nguvu, pia ndiye kapteni wa timu hiyo ambaye kwa kiasi kikubwa alichangia kuifanya timu isiyofungika hadi kutwaa ubingwa.

 

6. Aquino Corazole-Kenya

 

Huyu dada ni mkata umeme kweli. Ni mrefu, mbishi, asiyependa masihara wala mzaha hata kidogo awapo uwanjani, ingawa ndiye aliyekuwa kinara wa kuselebuka muziki baada ya kutwaa kombe.

Nguvu alizokuwa nazo, ziliwaweka salama mabeki wake na kipa kwa kupambana na mastraika wa timu pinzani na kuwapunguza nguvu kabla ya kuwafikia ukuta wa timu yake.

 

7. Mwanalima Jereko-Kenya

 

Huwezi kumtofautisha sana na Mwanahamisi Omari jinsi ya uchezaji wake, wakati mwingine hata wajihi.

Ni mchezaji mwenye ufundi wa hali ya juu mguuni, anayeweza kupiga chenga za kunyanyasa, mbio na kuweza kufanya chochote muda wowote.

Ndiye aliyekuwa chachu ya ushindi wa Kenya, aliweza kuuvusha mpira kutoka nyuma na kuupeleka mbele akicheza kama winga wa kulia, wakati mwingine hata beki wa kulia, lakini akitumika zaidi kushambulia kupitia pembeni.

Naye alifunga hat-trick kwenye mechi ambayo timu yake ya Kenya ilicheza dhidi ya Djibouti.

 

8. Juliet Nalukenge- Uganda

 

Ni mchezaji tegemeo kwenye ufungaji kikosi cha Uganda na ndiye staa wa timu hiyo ya taifa.

Alifunga hat-trick kwenye mechi ambayo timu yake iliichapa Djibouti mabao 13-0.

Ni mchezaji ambaye anafaa kabisa kuwa kwenye kikosi hiki cha wachezaji 11 bora wa Cecafa, akiungana na wenzake kutoka timu nyingine wanaweza kutengeneza kikosi hatari sana kwenye ukanda huu.

 

9. Asha Rashid 'Mwalala' - Kili Queens

 

Ni mchezaji kiongozi na mkongwe kwenye kikosi cha Kilimanjaro Queens ambaye ametoa mchango mkubwa hadi timu kufika fainali.

Ana nguvu na uwezo wa kufumua mashuti makali ambayo humfanya awe mfungaji mzuri, mwenye uwezo wa kucheza kama straika wa kati namba tisa, 10 au kiungo mchezeshaji.

 

10. Jentrix Shikangwa-Kenya

 

Ndiye mshindi wa kiatu cha dhahabu kwenye michuano hiyo, akimaliza akiwa amefunga mabao 10, akipiga hat-trick kwenye mechi dhidi ya Djibouti, Kenya ikishinda mabao 12-0, Jentrix akifunga mabao matano peke yake kwenye mechi hiyo.

Ndiye aliyefunga magoli yote mawili kwenye mechi ya fainali Kenya ikiichapa Kilimanjaro Queens magoli 2-0.

Ni mchezaji hatari na wa kuchungwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukokota mpira hasa kwenye mguu wake wa kushoto, chenga za maudhi ya kupiga mashuti makali.

Kocha wa Kenya mara nyingi alikuwa akimuingiza kipindi cha pili ambacho mabeki wa timu pinzani wanakuwa wamechoka.

 

11. Mwanahamisi Omari-Kili Queens

 

Huyu ni Mchezaji Bora kwenye michuano hiyo ambayo mwaka huu imefanyika katika msimu yake watatu. Ni mmoja wa wachezaji waliopiga hat-trick kwenye michuano hiyo.

Alifanya hivyo kwenye mechi dhidi ya Sudan Kusini alipofunga magoli matatu, Kilimanjaro Queens ilishinda mabao 9-0. Alimaliza michuano hiyo akiwa na magoli manne.

Uwezo wake wa kucheza na mpira, kasi, chenga za maudhi zimekuwa kivutio kikubwa kwenye michuano hiyo. Na ndiye mchezaji aliyekuwa akichungwa zaidi na wapinzani waliokuwa wakipambana na timu hiyo ya Tanzania Bara, hasa Kenya ambao walimuwekea ulinzi wa watu watatu waliokuwa wakitembea naye kila anakokwenda.

Mshambuliaji huyo kwa sasa anaichezea Simba Queens ya Dar es Salaam ambayo ilimsajili akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Wanawake msimu wa 2017/17,  Mlandizi Queens ya mkoani Pwani,

  

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa