Wadau: Inakuwaje ajira, mafunzo walimu kisiwe kipaumbele 2023

18May 2022
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wadau: Inakuwaje ajira, mafunzo walimu kisiwe kipaumbele 2023

AJIRA na mafunzo kazini kwa walimu ni kipaumbele cha kipekee kinachotajwa na wachambuzi wa bajeti ya Wizara ya Elimu, iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, wakishangaa kwanini serikali imekiweka kando.

Katibu wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu (CHAKAMWATA), Meshack Kapange. PICHA: MTANDAO

Wanatoa ushauri huo wanapozungumza na Nipashe kuhusu bajeti ya wizara hiyo na kile ambacho wanadhani, ingefaa serikali ikitazame kwa jicho pana wakati wa kutekeleza miradi ya kufikia maendeleo ya elimu.

 

Gratian Mkobwa ni rais mstaafu wa Chama cha Walimu (CWT), anapochambua bajeti ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, inayotaja uboreshaji wa mitaala, elimu ya juu, mikopo ya elimu ya juu na utafiti kuwa maeneo ya umuhimu wa juu kuwa vipaumbele. 

“Vipaumbele hivi ni sawa, lakini ni lazima tuweke nguvu katika ajira za walimu wengi zaidi 10,000 pekee hawatoshi bado pengo ni kubwa.”

 

“Pamoja na kuwaajiri pia tuwape mafunzo. Kuna upungufu mkubwa wa walimu, shule zimepungukiwa na zaidi ya nusu ya walimu, hivyo waliopo wanabeba mzigo mkubwa" anasema Mkoba.

 

Anakumbusha kuwa licha ya kuongeza shule za msingi kutokana na fedha za UVIKO-19, na serikali kutangaza ajira ya walimu, ikumbukwe wapo waliostaafu, kufariki, kuacha kazi, kuumwa, kupewa majukumu mengine na hata kufukuzwa.

 

Anasema la muhimu ni kuchambua upungufu huo kuajiri na kuwapa mafunzo kuendana na wakati.

Anaongeza: “Niliwahi kwenda shule moja ya sekondari nikakuta ina mwalimu mmoja wa Hisabati aliyepangiwa kufundisha vipindi 80 kwa wiki. Mazingira kama hayo ni kumchosha.”

"Lakini kuna suala la mbinu bora za ufundishaji ambalo nalo ni la muhimu, kwani tangu tubadili mwelekeo wa elimu yetu ambayo sasa inatoa maarifa na ujuzi inakuwaje walimu hawapewi mafunzo kuandana na wakati?" anahoji.

Anaongeza kuwa baadhi ya walimu hutoka vyuoni wakiwa na ujuzi unaoendana na walichojifunza hivyo wanahitaji elimu ya mabadiliko yanayojitokeza wakiwa kazini na kushauri wapewe mafunzo kazini kwa ajili ya kujiongezea maarifa .

 

"Pamoja na hayo, nipongeze wizara kwa mkakati wa kutaka kutoa elimu inayoendana na soko la ajira, kutokana na ukweli kwamba, wahitimu wa vyuo wamebakia kuzurura mitaani kutafuta kazi," anasema.

 

KIZUNGUMKUTI MITAALA

 

Akizungumzia kipaumbele cha kuboresha mitaala, Katibu wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu (CHAKAMWATA), Meshack Kapange, anasema kama nchi inataka kuboresha elimu, kutunga mitaala kurejeshwe kwenye Taasisi ya Kukuza Mitaala.

 

Mwalimu Kapange anasema Taasisi ya Ukuzaji Mitaala na ya Elimu Tanzania zirejeshewe majukumu ya kuzalisha vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ili kuendelea kuboresha elimu nchini.

"Ninaamini kwamba, utaratibu wa kuwapa watu binafsi jukumu la kutunga mitaala umesababisha ubora wa elimu kushuka, lakini lipo suala la utawala ambalo nalo ni changamoto nyingine,"anasema Kapange.

Anafafanua kuwa utawala wa walimu wa shule za msingi na sekondari unasimamiwa na wizara mbili ya TAMISEMI, huku vifaa vya kufundishia, sera, mitaala vipo Wizara ya Elimu.

 

“Lakini walimu ambao hukaa na wanafunzi na kuwafundisha hawashirikishwi katika mambo ya uboreshaji wa elimu. Kwa hiyo wito wangu ni kwamba, wakati wizara ikiwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha elimu katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, iangalie ushirikishwaji wa walimu, taasisi za kuboresha mitaala na kuandaa vifaa kutimiza majukumu yake," anasema.

 

UWEKEZAJI UTAFITI

 

Wadau wanaozungumzia utafiti wanashauri kuwekeza fedha za kutosha kwenye utafiti badala ya kutegemea wageni kuwekeza kwenye eneo hilo.

 

Baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, majina tunayo wanasema kazi nyingi za kitafiti nchini kwenye kilimo, viwanda, ubunifu, teknolojia zinakwama kutokana na serikali kutoweka fedha.

 

“Zipo taasisi nyingi za kitafiti, kuna Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  COSTECH, SIDO, TIRDO, CARMATEC, TEMDO lakini kazi zake ziko wapi zikibadilisha maisha ya Watanzania mijini na vijijini?   Tunataka kuona kazi za kitafiti zilizokwama zikipewa fedha na msukumo ili ziwafikie wananchi na kuleta mabadiliko.” Anasema mhadhiri jina tunalo.

 

BAJETI YA 2022/23

 

Katika mwaka wa fedha wa 2022/3, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepanga kutumia Shilingi  trilioni 1.49, huku ikiwa imeweka kipaumbele kwenye uboreshaji wa mitaala, elimu ya juu, mikopo ya elimu ya juu na utafiti, Waziri Mkenda anasema.

 

Anasema serikali imefanya tathmini ya mitaala 72 iliyowasilishwa na vyuo vikuu nchini na kutoa ithibati kwa mitaala hiyo na kwamba  mingine 41 iko katika hatua mbalimbali za kupatiwa ithibati.

 

Anaongeza kuwa serikali imeendelea kuongeza fursa za elimu kwa kuboresha huduma za upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

 

 Lengo la kuboresha huduma ya mikopo hiyo ni kuwezesha wanafunzi wenye sifa na uhitaji kuendelea na elimu ya juu bila vikwazo.

   MIKAKATI YA WIZARA

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa ndani wa kufanya utafiti na kutumia matokeo ya utafiti katika kuchangia ajenda ya maendeleo ya nchi.

Anasema, itafanya utafiti 252 katika maeneo ya mazingira, TEHAMA, nishati, kilimo na chakula, uongozi na biashara, maendeleo ya utalii, sheria, udhibiti wa ubora, utawala na maendeleo, watu wenye ulemavu na mahitaji maalum.

Prof. Mkenda anataja maeneo mengine ya utafiti kuwa ni maliasili, umaskini, utamaduni, haki za binadamu, maendeleo ya watu na mawasiliano, mifugo, biashara, uvuvi, elimu, sayansi, lugha na fasihi.

Kwenye suala la wabunifu, anafafanua kuwa serikali itawaibua, kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu na wagunduzi wachanga kupitia mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), ili kuwezesha ubunifu wao kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Walengwa wa ubunifu huo ni kuanzia shule za msingi na sekondari, vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu, vituo vya kuendeleza teknolojia, taasisi za utafiti na maendeleo pamoja na mfumo usio rasmi.

Habari Kubwa