Wadau ndiyo maelekezo ya wanafunzi kumaliza ukeketaji

23Feb 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wadau ndiyo maelekezo ya wanafunzi kumaliza ukeketaji

SHERIA ya Mtoto ya 2009 inasisitiza kumlinda mtu wa chini ya miaka 18 na  ibara 13(1) inaeleza haya:” Ni kosa la jinai kumsababishia mtoto mateso au adhabu za kikatili, matendo yasiyo ya kibidamu au vitendo vya kumdhalilisha ambavyo ni pamoja na mazoea ya tamaduni ambazo hazina utu au .....

Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari zilizopo Kivule jijini Dar es Salaam, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kupinga ukeketaji. PICHA: SABATO KASIKA

zinasababisha maumivu kimwili na kiakili kwa mtoto”.

Licha ya kuwapo sheria hiyo ukeketaji unaosababisha mateso kwa mabinti na wanawake ambao unakwenda kinyume na matakwa ya sheria unaendelea pamoja na kufanyika uhamasishaji wa kupinga mila hiyo iliyopitwa na wakati.

Februari  6 mwaka huu, ilikuwa ni kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Kupinga Ukeketaji ikiwa na kaulimbiu "Hakuna muda wa kutochukua hatua. Ungana, fadhili na chukua hatua kukomesha ukeketaji".

Maadhimisho ya siku hiyo hulenga kuhimiza serikali, asasi za kiraia, mashirika na jamii kuongeza uelewa na kutokomeza  ukeketaji, ambao unaathiri wanawake na wasichana kote duniani.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, baadhi ya wanafunzi wa Dar es Salaam, wanaomba wigo upanuliwe zaidi kwenye utoaji wa elimu ya kupinga ukatili huo ili wengi wajitambue na wawe tayari kuukwepa.

Wanatoa wito huo katika kampeni za kupinga ukeketaji zilizofanyika kwenye kata za Kivule na Kitunda, zikihusisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, serikali na wasaidizi wa kisheria.

Washiriki wengine katika  kampeni hizo ni wa vituo vya taarifa na maarifa na Mpango wa Taifa wa Kukomesha Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), ngazi ya kata.

Mmoja wa wanafunzi  hao, Asia Salum wa Sekondari ya Kivule , anasema, tatizo la ukeketaji ni mtambuka linaathiri mamilioni ya wanawake na wasichana kote duniani, hivyo elimu ya kulikabili inatakiwa kupanuliwa zaidi.

NINI KIFANYIKE?

Anasema,   ukeketaji ni mkubwa, lakini anaamini ni wanafunzi wachache wanaojua madhara ya ukeketaji, hasa wa mijini na kwamba ipo haja elimu hiyo kutolewa zaidi kwenye maeneo ambayo mila hizo zinafanyika.

"Wadau wa kupinga ukeketaji wanaweza kuwa na ratiba ya vipindi ya kutoa elimu hiyo katika shule zote za vijijini hasa kwenye mikoa ambayo yanasifika kwa ukeketaji ili kukomesha vitendo hivyo," anasema Asia.

Mwanafunzi huyo anafafanua kuwa elimu hiyo isiishie shuleni bali hata wazazi, walezi, ngariba na wazee wa kimila nao waelimishwe vya kutosha, kwa maelezo kwamba hao ndiyo tatizo.

Pili Makulu wa Shule ya Sekondari Abuu Juma, anasema, maeneo ya Kivule yamekuwa yakitajwa kuwa na vitendo vya ukeketaji, hivyo wanafunzi wa shule zote za maeneo hayo wafuatiliwe na kupewa elimu.

"Huwa ninasikia kwamba huku Kivule kuna watu kutoka mikoa inayokeketa na yanaendelea kufanya vitendo hivyo, ninawashauri nyie watoa elimu mje huku shule kwetu mfundishe madhara ya ukeketaji," anasema Pili.

Anasema, wanafunzi wakipewa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya ukeketaji, wataifikisha kwa wazazi wao na kwamba kwa utaratibu huo, kuna uwezakano wa kumaliza vitendo hivyo kwenye jamii.

"Ninaamini kwamba, kampeni ya kupinga ukeketaji na jitihada za pamoja vinahitajika kwa ajili ya kumaliza tatizo hili. Kikubwa zaidi wadau kuanzisha ratiba ya kutoa elimu katika shule mbalimbali na kuwafikia wale wote wanaohusika na kuendeleza mila hii potofu," anasema.

Anasema, vita dhidi ya ukeketaji isisubiri siku ya maadhimisho tu bali mikakati ya kupanua wigo wa utoaji elimu ya kupinga vitendo hivyo inahitajika ili kumwezesha mtoto wa kike kusoma bila hofu ya kukatisha masomo.

KUPENDA UHALIFU

Viongozi wa dini waliokuwa kwenye kampeni hizo, wanasema umefika wakati jamii kuachana kukumbatia mila ambazo zinakwenda kinyume na kile ambacho Mwenyezi Mungu ameagiza.

Mchungaji Joseph Mapunda wa Kanisa la Calvary Assembulies of God (ACG) la Kivule Machimbo, anasema, katika maandiko matakatifu, hakuna sehemu inayohalalisha ukeketaji.

"Ukeketaji ni kwenda kinyume na kile ambacho Mungu ameagiza, kwani wanaume ndiyo wameruhusiwa kutahiriwa, siyo kukeketa wanawake, hivyo wanaokeketa wanamkosea Mungu," anasema Mchungaji Mapunda.

Abdi Mahanyu ni Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)  Kipunguni, anasema, ukeketaji ni kumkosoa Mungu, na kwamba wanaofanya hivyo, wanapingana na uumbaji wake na kufuata matakwa yao wenyewe.

Mzee wa kimila wa eneo la Kivule, Joseph Gasaya, anasema dunia ya leo imebadilika, na kwamba wanaoendekeza mila za ukeketaji hawana budi kubadilika na kuachana nazo.

"Ukeketaji ulikuwa enzi hizo wakati sisi tungali vijana huko nyumbani kwetu Musoma, lakini dunia imebadilika, magonjwa yameongezeka, hivyo niwaombe wanaoendelea kukeketa waache," anasema Gasaya.

NI VITA YA JAMII

Mratibu wa Miradi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ambao waliratibu kampeni hizo, Hellen Urio, anasema kila mtu akishiriki katika vita ya kukomesha vitendo vya ukeketaji nchini.

"Jamii inatakiwa kutambua kuwa vita dhidi ya ukeketaji ni ya kila mtu katika eneo lake. Kila mmoja akishiriki, vitendo vya ukatili ukiwamo huo wa ukeketaji, vitakoma nchini, hivyo tuendelee kushirikiana," anasema Urio.

Urio anasema, wanafunzi ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa ukeketaji, na kuwaelekeza kuwa wanapoona dalili au tukio la ukeketaji, watoe taarifa haraka ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

"Kuna sehemu nyingi za kutoa taarifa kuanzia vituo vya taarifa na maarifa, MTAKUWWA, kwa wasaidizi wa kisheria na hata kwenye madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi," anasema.

Mratibu huyo anamtaka kila mtu mwenye taarifa yoyote ya vitendo hivyo kuifika mahali husika, na kwamba kufanya hivyo ni moja ya elimu ya kupambana na ukeketaji kwenye jamii.

 

 

Habari Kubwa