Wadau wazalishaji wadai iwe sekta rasmi ‘inalipa’ kiuchumi

11Jun 2021
Julieth Mkireri
Kibaha
Nipashe
Wadau wazalishaji wadai iwe sekta rasmi ‘inalipa’ kiuchumi

IKO wazi kuhusu mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi na maendeleo barani Afrika. Ni chanzo kikuu cha chakula kwa watu zaidi ya milioni 950 wanaoishi katika nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara na malighafi zinazotumika viwandani.

Takwimu za Benki ya Dunia, zinabainisha mchango wa kilimo katika Pato la Taifa kwa nchi hizo ni asilimia 15 na katika nchi zilizoko Kusini ni zaidi, mchango uko juu zaidi. 

Nchini Tanzania, takwimu zinagusia hadi hivi karibuni, baadhi ya manufaa ya sekta ya kilimo ni pamoja na kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa kwa wastani hadi asilimia 27, ikiwa ni mwajiri mkuu wa theluthi mbili za Watanzania.

Aidha, kilimo kinarejewa kuwa chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa kuingiza wastani wa takriban robo ya fedha, zitokanazo na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Ni taarifa zilizotolewa baaada ya kufanyika  Sensa ya Tano ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/2020, hali inakuwa bayana Watanzania wengi wanajishughulisha katika Sekta ya Kilimo wakizalisha mazao mengi na kuyauza ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, mazao wanayoyazalisha yamekuwa hayapati masoko stahiki na mengine yanaharibika kwa kutokuwa na viwanda vya kutosha kuchakata mazao hayo kwa wakati.

WADAU USINDIKAJI

Mkurugenzi wa Asasi ya Vijana ya YPC, Israel Ilunde anaelezea namna wanavyotoa elimu kwa vijana wajikite kwenye sekta ya usindikaji badala ya kusubiri ajira.

Ilunde anasema katika hatua za awali, wametafakari hali halisi ya sekta hiyo ya usindikaji vyakula na kuwahamasisha vijana kujikita huko.

"Baada ya kutafakari suala la ajira tulienda zaidi kwenye ukosefu wa ajira hata ajira zikipatikana ni vizuri kuangalia na ajira yenyewe kazi zenye staha ndani ya Sekta ya Usindikaji Vyakula," anasema Ilunde.

Katika hatua ya awali, anasema wamewakutanisha vijana na kuzungumzia sekta hiyo ya usindikaji kupitia kilimo, ili yeyote anayejihusisha nayo iwe kazi yenye staha.

Anasema, usindikaji wote unategemea mazao kutoka mashambani hivyo kama kilimo kitadorora, kama ilivyo usindikaji.

"Tumelenga kilimo kwa kuwa ndiyo kinacholeta unafuu wa maisha, asilimia kuwa ya Watanzania wanategemea mazao kutoka shambani.

“Hivyo, vijana wenye nguvu wanatakiwa waingie shambani wazalishe mazao na wengine wanunue na kusindika baadaye waviuze ndani na nje ya nchi na kujikwamua kiuchumi," anasema.

Ufafanuzi wake ni kwamba, kazi ya usindikaji vyakula ina mapokeo ya chini kutoka kwa vijana, hivyo kwa sasa wanatakiwa kubadilika kuhamishia mawazo yao kuchakata mazao na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.

"Walimu wa stadi za kazi waanze kuwafundisha wanafunzi wa shule ya msingi kulima bustani, waandaliwe kujikita katika sekta hii ya kilimo tukianzia chini, mabadiliko makubwa yataonekana na baadaye hakutakuwapo malalamiko ya ajira," anasisitiza. 

Anasema kwa sasa wanawake wanaongoza kwenye Sekta ya Usindikaji na vijana bado wachache na sasa kundi la wanawake wanatakiwa kuanza kuwafundisha, ili nao watumie fursa hiyo kujiajiri. 

Katika kongamano la vijana lililoandaliwa na YPC, walieleza Sekta ya Usindikaji inategemea uzalishaji wa kilimo, hivyo kilimo kinapaswa kupewa umuhimu unaostahili kitaifa na kuwekewa mazingira mazuri, ili wasindikaji vyakula wafanye kazi zenye staha na kuwa na matokeo bora. 

Mapendekezo mengine yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa YPC ni pamoja na Sekta Usindikaji, itambuliwe kama mwajiri na itungiwe sera itakayosaidia namna ya kuzalisha ajira zenye staha kwa vijana

Nyingine inahusu wanaoanzisha kampuni au miradi katika sekta ya usindikaji, wapewe motisha  na kuungwa mkono na serikali na wadau wote, kuepuka vizuizi vya kuanzisha na kuendesha shughuli za usindikaji

Pendekezo lingine ni kwa nguvukazi ya Taifa  hususan wahitimu wa elimu ngazi mbalimbali, waandaliwe na taasisi ikiwamo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ili waweze kuajiriwa na sekta ya usindikaji,

Lengo linataja ni kuwezesha vijana wanaojishughulisha na usindikaji vyakula kifedha, teknolojia na masoko, ili kazi ziwe zenye staha na tija kwa umma.

Ilunde anaeleza kuwa, maofisa maendeleo ya jamii pamoja na maofisa maendeleo ya vijana, wanapaswa kuongeza juhudi ya kuwasaidia vijana waliopo katika sekta ya usindikaji wafanikiwe zaidi, hata kuweza kuajiri vijana.

"Pendekezo letu lingine ni serikali kupitia jumuiya za kikanda na kimataifa ihakikishe kuondolewa kwa vikwazo vya kuvuka mipaka wakati wa kufanya biashara ya bidhaa za usindikaji, ili kupanua masoko na kubadilishana uzoefu na mataifa mengine juu ya tasnia na bidhaa zitokanazo na usindikaji," anabainisha.

Pendekezo lake ni kutaka YPC ishirikiane na serikali na wadau husika kutoa elimu ya uraia na ujasiriamali kila mara kwa vijana wasindikaji na wanaotaka kuwa wasindikaji waweze kuwa na uwezo wa kuvumbua fursa ndani ya kilimo na kuweza kutumia haki yao na kuwajibika vema.

Mratibu Miradi wa YPC, Fred Mtei, anasema tatizo la ajira linaweza kupungua, endapo sekta ya usindikaji itapewa kipaumbele.

Anasema, endapo vijana watapata mafunzo ya usindikaji, ni wazi watajiajiri na kusindika mazao yatayokuwa yanaongezeka thamani na kuyauza maeneo mbalimbali.

Mdau wa mwenendo huo, Sarah Mwakabinga, anasema vijana wanatakiwa kutambua kuwa kilimo si lazima kushika jembe, badala yake watumie fursa zilizopo kwenye kilimo kwa kuchukua mazao kuyasindika na kuyauza katika masoko.

Mlongecha Mkuku, kijana mshiriki wa kongamano, anasema wakati taifa limeshagonga hiodi na kuingia katika Uchumi wa Kati, ni muhimu endapo sekta ya usindikaji itapewa kipaumbele ma kuongeza idadi ya ajira na uchumi stahiki.

Habib Hatibu, anatumia fursa hiyo, kuziomba taasisi nyinginezo kuwapatia elimu ya usindikaji ili wajikite katika eneeo hilo la uzalishaji.

RC PWANI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, anatoa wito kwa watafiti wa mazao ya kilimo kufanya utafiti wa mazao yanayokubalika katika ardhi ya mkoa wa Pwani.

Kunenge anasema, endapo wananchi wataelewa mazao yanayokubalika mkoani Pwani, ni wazi watajikita kwenye kilimo chenye tija na vijana watatoa elimu stahiki ya kilimo na kuyafanya maisha yao kuwa mepesi na yenye tija.

Akiwa katika maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI), Kunenge anasema, pia kuna haja ya utafiti masoko ufanyike kwa kupata sehemu ya kuuza mazao wanayozalisha.

Habari Kubwa