Waganga jadi wawekwa ‘kitimoto’ kisa cha kuendekeza ramli mauaji

06Aug 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Waganga jadi wawekwa ‘kitimoto’ kisa cha kuendekeza ramli mauaji
  • • RPC: Wao, wanaowatuma, tunao!

MKOA wa Shinyanga awali ulikabiliwa na adha ya ugumu wa mauaji ya wazee yatokanayo na imani za kishirikina, kwa kila aliyekuwa na macho mekundu alihisiwa uchawi, baadhi wakiangukia kukatwa mapanga.

Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, Debora Magiligimba, akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa wazee, kujadili athari za imani potofu za kishirikina na ramli chonganishi. PICHA: MARCO MADUHU.

Chanzo kikuu kinatajwa ni imani za kishirikina, yanayosababishwa na waganga wa jadi, kupitia ramli wanazopiga kuwaambia wateja wao kuwa wamerogwa na wazee, ndipo mchakato wa kuanza kutekelezwa mauaji ya kilipiza kisasi yanapoanzia.

Namna ya kuyatekeleza, huwa kuna watu maalumu wanaokodiwa kufanya mauaji kazio hiyo, ikidaiwa wanapewa ujira wa fedha kuanzia Sh. 300,000.

NENO LA RPC

Mwaka jana, Polisi mkoani Shinyanga liliwakamata waganga wa jadi 19 wapiga ramli, wakiwa na nyara za serikali wanazotumia kama vile mikia ya nyumbu, ngozi za kenge na simba, kucha za simba, mayai ya mbuni, kichwa cha kenge, jino la ngiri, na bundi mmoja.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Debora Magiligimba, anasema ukamataji wa waganga hao wa jadi, ni uamuzi muhimu katika kukomesha matukio ya mauaji dhidi ya wazee.

“Mauaji ya wazee yatokanayo na imani za kishirikina mkoani Shinyanga yamepungua kwa kiasi kikubwa, ikilinganisha na miaka ya nyuma. Hali hii inatokana na kuwakamata waganga wa jadi ambao hupiga ramli chonganishi, sababu wao ndio chanzo kikubwa cha mauaji haya,”anasema Kamanda Debora.

“Januari mwaka huu (2020), tulifanikiwa kumkamata mganga maarufu wa upigaji ramli chonganishi,” anasema, huku akifafanua hatua hiyo iliendana na kuwanasa watu wanne waliokodiwa kutekeleza mauaji hayo hayo mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kamanda Debora, watu hao wanadaiwa kukodishwa kufanya kazi hiyo kwa ujira wa Sh. milioni tatu.

Aidha, anasema mauaji saba yalitokea mwaka jana kati ya Januari na Juni na mwaka huu idadi imeshuka kwa kipindi kama hicho, ameuawa mzee mmoja.

BARAZA LA WAZEE

Laurent Mihayo, Mjumbe wa Baraza la Wazee Wilayani Kahama, Shinyanga, katika taarifa anayotoa kwa niaba ya Katibu wa Baraza hilo, anasema waganga wa jadi wapiga ramli wamekuwa tatizo katika ukomeshaji mauaji ya wazee, unaosukumwa na ushirikina.

“Takwimu za mwaka jana zinaonyesha kulitokea mauaji ya wazee wawili yatokanayo na imani za kishirikina, lakini mwaka huu hadi sasa tunamshukuru Mungu hakuna,” anaongeza Underson Lyimo, Katibu wa Baraza Wazee Mkoa.

Pia, Katibu wa Baraza la Wazee ngazi ya Wilaya Shinyanga, Ngassa Maganga, anasema, pia elimu inapaswa kutolewa kwa umma ubadilike dhidi ya nyendo za ramli za kishirikina zinazoangukia kuwashuku wazee.

Anaainisha undani wa wazee kuwa na macho mekundu na hasa wanawake, sababu kuu ni kupika kwa kutumia kuni kwa muda mrefu na daima haihusiani na dhana ya kuhusika na uchawi.

WANAOWATETEA WAZEE

Mratibu wa Shirika la Tawlae, Eliasenya Nnko linalotetea haki za wazee mkoani Shinyanga, ambao wanatekeleza mradi wa kuifanya mifumo ya utawala kuwajibika kwa wazee ikiwamo kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili, yakiwamo masuala ya afya, pamoja na kutokomeza mauaji ya wazee.

Anasema tangu mradi huo uanze kufanya kazi mkoani Shinyanga mwaka 2018, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la mauaji ya wazee tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma. Mradi huo unakoma mwezi huu.

“Vitu ambavyo tunavifanya kwenye mradi wetu huu, nikutoa elimu ya ukatili dhidi ya mauaji ya wazee kwa kukutana na wazee wenyewe, waganga wa jadi, wazee maarufu, viongozi wa dini, maofisa ustawi, wakuu wa wilaya na jeshi la Polisi,”anasema Nnko, anayekiri kushuhudiwa mafanikio.

“Sisi kama Shirika la Tawlae linatotetea haki za wazee, tunaipongeza serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kupambana na hawa waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi na kufanikiwa kupunguza matukio ya mauaji ya wazee,” anaongeza.

Aidha, anataja jicho la kitaifa upande wa serikali, unaonuia kutokomeza mauaji ya wazee, ufikapo mwaka 2023.

Habari Kubwa