Waingereza wanyonyeshaji wa kweli hawafiki asilimia moja

03Aug 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Waingereza wanyonyeshaji wa kweli hawafiki asilimia moja
  • Wanaongoza kwa rekodi mbaya duniani

MADAKTARI magwiji wa masuala ya uzazi, wamebainisha Uingereza ndiyo inaongoza kuwa na kiasi kidogo zaidi duniani ya kinamama wanaonyonyesha watoto wao inavyopaswa.

Inatajwa kuwa asilimia 0.5 pekee ya kinamama hao, ndio wanaonyonyesha katika kiwango kinachotakiwa cha miaka miwili, kwani waliobaki asilimia 99, wanawaachisha ziwa watoto wao chini ya umri wa mwaka mmoja.

Sababu kuu inayotajwa ni kuendekeza mfumo wa maisha, kama vile kuona aibu mbele ya watu wengine. Haikutajwa watu wa jinsia gani.

Kwa mujibu wa miongozo ya unyonyeshaji, mama anapaswa kunyonyesha mwanawe miezi sita ya kwanza iwe ni maziwa pekee ya mama, bila hata ya maji na unyonyeshaji huo uendelee hadi umri wa miaka miwili, sambamba na vyakula vingine.

Nchi nyingine kama Ujerumani, kunaelezwa kinamama wanaokamilisha miongozo ya kunyonya ni asilimia 23, huku Brazil wanafikia asilimia
56.

Sasa madaktari wa Uingereza wanajenga hoja ya kuishauri serikali, kwamba mambo hayo muhimu katika maisha, yaanze kufundishwa shuleni, ili kuleta mabadiliko kupitia jamii kujitambua.

Wataaluma kutoka chuo kiitwacho Royal College of Paediatrics and Child Health, wanataja sababu kuu ni kinamama wanyonyeshaji kuona aibu ya kunyonyesha watoto wao katika maeneo ya wazi.

Mantiki ya aibu yao inaelezwa kuwa wataonekana wanachokifanya ni cha aibu mbele ya umma na hawazitendei haki jumuiya wanazoishi. Ni asilimia 0.5 tu ndiyo inanena kuwa huru, hawaoni haya kunyoyesha mbele ya umma unaowazunguka na ndiyo hao wanaofikisha miaka miwili ya kunyonyesha.

Takwimu za utafiti zinaonyesha kuwa katika kundi la wanaokwepa kunyonyesha na hasa hadharani, asilimia 63 wanadai wanaona aibu mbele ya wageni na asilimia 44 ni mbele ya umma kwa ujumla.

Muuguzi Mkuu wa Afya ya Umma nchini Uingereza, Viv Bennett, anasema:”Sote tunaweza kuwasaidia wanawake kokote waliko. Hiyo inapanua utamaduni wa mapana wa kuwatia moyo na kuanza na uzoefu wenye mwenendo chanya.

“Unyonyeshaji una faida nyingi kwa mama na mtoto na inajumisha na kumsaidia kuzuia maambukizi, kupunguza kitambi (tumbo) na kuboresha upeo wa akili.”

Kinachohimizwa na wataaluma hao ni kwamba, unyonyeshaji unapaswa kufikia hatua ya kugeuzwa sehemu ya elimu ya jumla kwa umma, pia mtu mmoja mmoja.

Idara ya Afya ya Umma ya Uingereza, inahimiza kwamba itakuwa vyema wanafunzi wanaopaswa kufundishwa shuleni kuanzia umri wa miaka 11 na katika hatua ya elimu ya sekondari.

Wataaluma kutoka chuo cha Royal, wanahimiza hatua hiyo kufika mbali zaidi katika sehemu za kazi, kunakopaswa kuandaliwa vyumba maalum vyenye huduma muhimu za majumbani kama vile friji, ili kuwawezesha kinamama wazazi kunyonyesha watoto wao vizuri, kama wanavyokuwa majumbani.

Katika hilo, pia wanatoa angalizo kuwa, kamwe mishahara ya kinamama hao wazazi isiguswe kwa namna yoyote ile, kutokana na udhuru huo unaotokana na kunyoyesha.

Utafiti uliofanywa kwa kuwahusisha kinamama 1,000, ulibaini sababu nyingine ya kinamama kuachisha mapema kunyonyesha watoto ni hofu kwamba watoto hawapati maziwa ya kutosha na wanawatafutia lishe ya kutosha kupitia mbadala wa maziwa ya mama.

Utafiti mmojawapo unaonyesha kuwa, asilimia 27 ya kinamama walifikia uamuzi huo, bila ya kutambua wanachokifanya na kuna baadhi waliamua kutokana na kile wanachokitafsiri katika mabinti zao kuwa “wamechoshwa na kunyonyesha.”

Justine Roberts, ambaye ni mdau muhimu katika haki za wanawake na Mtendaji Mkuu wa taasisi inayohudumia afya ya wazazi, anatamka:

“Hakuna haja ya kuendelea kuwaelezea kinamama kila kukicha kuhusu wajibu wao kuendelea kunyonyesha, wakati huo huo mnawaangusha wakiwa na watoto wao mikononi.”

“Kunyonyesha ni jambo linalohitaji ufundi na kinamama wengi wanahitaji kuungwa mkono wanapokabiliwa na matatizo, ikizingatiwa huwa wananyamazishwa na kukosa usingizi.

“Aibu, hasira na unyonge wanaokumbana nao kinamama wanaoachana na kunyonyesha, si haki zaidi na kuwaacha wengi katika fikra kwamba wameshindwa.”

Kwa mujibu wa wasomi wa afya kutoka chuoni Royal, ni kwamba kuna tabia ya serikali yao kuopuuza ushauri wa wakunga kuhusiana na jambo hilo la afya ya uzazi na ndiyo inazaa walakini huo unaolalamikiwa sasa.

Soma makala nyingine uk. 15

L Makala hii inatokana na taarifa za gazeti la Daily Mail ya Uingereza.

Habari Kubwa