Waja na mapinduzi kilimo

11Jun 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Waja na mapinduzi kilimo
  • Wafikia watu 32,000; ekari 70,000
  • Mahindi, alizeti, matunda, mpunga
  • Mikoa 10; Manyara, Tanga, Moro…

KILIMO kinatajwa kula kila kitu katika uchumi na maisha kwa jumla. Ni mwajiri na mwingizaji mkubwa wa Pato la Taifa kwa wingi.

Ili kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo waboreshe maisha yao, kinapaswa kuwa cha uhakika kwa usalama wa chakula na lishe na kuchangia Pato la Taifa.

Hadi sasa kilimo kitaifa kinakabiliwa na changamoto ya ukuaji ikihitaji maboresho ya teknolojia katika uzalishaji shambani, vivyo hivyo mbinu za masoko ya bidhaa zake ambayo teknolojia ya digitali inachukua nafasi kwa kasi ndani ya kila sekta.

Kampuni ya Kilimo na Biashara ya Jatu PLC, inayoendesha na kusimamia miradi ya kilimo nchini, kwa kushirikiana na wanachama wake.
Hadi sasa inatamka kupanga kuboresha miundombinu ya kilimo kwa kutoa pembejeo za kisasa za kilimo na mbegu.

Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo, Peter Gesaya, anasema wanawajibika na kushauri wanachama kumiliki mashamba makubwa na yenye rutuba yanayokubali mazao mahsusi ambayo wanayahitaji katika uzalishaji bidhaa.

"Hadi sasa Jatu kwa kushirikiana na wanachama wetu, tumefanikiwa kumiliki mashamba makubwa matatu yanayopatikana mkoani Manyara, Morogoro na Tanga," anasema Gesaya.

Anafafanua mpango wao ni kuhakikisha wanaanzisha mashamba kila wilaya nchini na wanayoyawekea miundombinu ya umwagiliaji, yakiambatana na viwanda ndani yake.

MIRADI ILIYOKO

Gesaya anasema katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, kampuni ya Jatu inaendesha mradi wa kilimo cha mahindi na alizeti na zaidi ya ekari 2,000 zimeshalimwa, huku matarajio ni kufikisha ekari 5,000 za mazao hayo ifikapo mwaka 2022.

Gesaya anasema Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, kampuni ya Jatu imejikita katika kilimo cha mpunga. Hadi kufikia sasa ekari zaidi ya 200 zimeshalimwa na asasi hiyo inaendeleza uwekezaji zaidi katika kilimo hicho, ili ifikapo mwaka ujao ifikie wastani wa ekari 1000 za mpunga.

WANAVYOTANUA SOKO

Wiki iliyopita kampuni ya Jatu ilianza kutangaza kuanza kuuza hisa zake katika soko la hisa jijini Dar es Salaam (DSE) kwa lengo la kupanua kilimo nchini.
 
Gesaya anasema kwa sasa wameshawanufaisha zaidi ya wanachama 32,000, ikiwa na lengo la kuwafikia Watanzania zaidi ya milioni mbili.

"Tumeamua kuingia kwenye soko la hisa ili kupanua kilimo na kuwasaidia wakulima kufanya kilimo chenye tija na kila mwanahisa atalima kulingana na hisa zake," anasema Gesaya.

Anasema uuzaji wa hisa hizo ni katika kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana kwa ajili ya kuuza kwa umma katika soko la awali.

Gesaya anasema mpaka sasa wameshafanikisha shughuli za kilimo katika ekari 70,000 nchini. Anafafanua: “Mpaka sasa tumeshafikia mikoa 10 na tumefanya kilimo cha machungwa, maparachichi, mahindi, alizeti, mpunga, ndizi na mboga.

Anafafanua kwamba asasi yao imepanga kuboresha miundombinu ya kilimo kwa kutoa pembejeo za kisasa za kilimo pamoja na mbegu.
 
AINA YA KILIMO

Gesaya anasema uzalishaji vyakula wanavyovihamasisha inajumuisha mchele, unga wa dona, karanga, unga wa lishe na ngano. Pia, kuna mboga za mlo kama maharage, samaki na dagaa na matunda; ndizi, nanasi na parachichi.

Anasema viungo wanavyozalisha ni mafuta ya alizeti, chai mbadala, sukari na chumvi na vinywaji ambavyo ni maji ya kunywa na juisi.

Kiongozi huyo anajumuisha kuwa wamejikita katika kuzalisha vyakula vinavyotumika kila siku katika familia.

MASOKO

Gesaya anasema kuna masoko ya uuzaji wa bidhaa hizo katika mfumo wa mtandao, pia kupashana habari kati ya mtu mmoja na mwingine kuhusu zilizoko na zinakopatikana.

Anataja faida zinazopatikana ndiyo zinazotumika kumtengenezea mwanachama kipato cha kudumu kila mwezi.

Mkurugenzi huyo anaeleza zaidi kuwa soko la biashara ya mtandao, linaenda sambamba na utengenezaji mtandao wa walaji wa bidhaa hizo.

Anasema, wamekuwa wakitoa fursa ya masoko ya bidhaa za wajasiriamali wanachama kwa kuwaingizia sokoni. 

Gesaya anasema, wanatumia mfumo wa masoko ya mtandao katika kuhudumia na ununuzi wa bidhaa za chakula, usafi na nishati.

Anasema baada ya kuona bidhaa hizo katika mtandao ndipo mnunuzi anauchaguzi wa bidhaa na kuagiza katika mchato unaopitia kwa wakala wa karibu na mteja ili kumrahisishia msafirishaji kujua pa kumfikishia mzigo mnunuzi kwa mawasiliano maalum yaliyoandaliwa.

Habari Kubwa