Wajawazito mmesikia ni ruksa kuchanjwa UVIKO- 19 ila…..

26Aug 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Wajawazito mmesikia ni ruksa kuchanjwa UVIKO- 19 ila…..

TANGU kuwapo kwa maambukizi ya virusi vya corona duniani hadi jitihada za kupatikana chanjo zilipofanikiwa hivi karibuni, suala la wajawazito na wanaonyonyesha kupewa chanjo linaendelea kuhitaji ufafanuzi na taarifa zaidi.

Makundi ambayo yalipewa kipaumbele kuchanjwa ni pamoja na wataalamu wa afya, wazee, wenye magonjwa yasiyoambukiza na watu walio katika huduma au kazi zinazowakutanisha na mamia ya watu.

Hata hivyo, suala la wajawazito na wanaonyonyesha kupata chanjo hiyo halikutajwa kwa kiwango kikubwa hasa kwa baadhi ya nchi, hivyo, kuibua hisia kuwa huenda wanaweza kuathirika iwapo wangechanjwa.

Kufuatia hatua hiyo, Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Wanawake na na Uzazi Tanzania (AGOTA), hivi karibuni kimetoa ufafanuzi kuhusu mustakali wa wajawazito na wanaonyonyesha kuchanjwa, na kushauri wachanje.

Mabingwa 10 wanachama wa Chama cha Madaktari wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika andiko hilo wanaeleza kuwa kundi hilo nalo linastahili kupata chanjo ya corona, lakini kwa kuchukua tahadhari kwa kujua hali ya afya zao.

Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Matilda Ngarina, mmoja wa walioshiriki kuandaa andiko hilo, anasema sababu ya kutoa maelezo kuhusu wajawazito na kinamama wanaonyonyesha na chanjo hiyo kunatokana na kupokea maswali ambayo watu wameomba kupatiwa ufafanuzi.

Ngarina ambaye pia ni Rais (AGOTA), anasema kutokana na hilo wataalamu hao walikusanya taarifa za takwimu kutoka sehemu tofauti na kuja na maelezo kuwa kundi hilo linahitaji chanjo pia.

AGOTA inaeleza kuwa wajawazito wamo katika hatari ya kupata maambukizo ikilinganishwa na wengine.

Aidha, wapo katika hatari ya kujifungua mapema kabla ya wakati au kutimiza iwapo watapata COVID-19, hivyo wanahitaji kukingwa.

Inaendelea kubainisha kwamba wajawazito wanatakiwa  kusubiri siku 14 iwapo wamepatiwa chanjo nyingine zinazohusiana na ujauzito, kabla ya kuchanjwa chanjo ya corona.

Pia baada ya chanjo hiyo ya corona inatakiwa kukaa siku 28 kabla ya kupatiwa chanjo nyingine ambayo inatolewa kwa wajawazito, isipokuwa kama kuna dharura kwa magonjwa kama homa ya ini itokanayo na kirusi cha Hepatitis B.

ATHARI BAADA YA CHANJO

Kuhusu athari baada ya chanjo AGOTA inasema iwapo umechanjwa chanjo dhidi ya corona kama ilivyo kwa nyingine hususan kwa chanjo yenye dozi mbili, wajawazito hawajaripoti athari zozote, isipokuwa kero ndogo ikiwamo homa, ambazo hupunguzwa na dawa za kutuliza maumivu kama paracetamol na panadol.

Pia baadhi hupata athari kutokana na mzio au aleji walionao baada ya kuchanjwa, na kwamba watoa huduma za afya wanatakiwa wawaulize kabla ya kuwachanja kama wana historia ya kupata madhara.

WANAONYONYESHA

Wakati wa kunyonyesha, AGOTA inaeleza kuwa hakuna utafiti unaoonyesha kuna athari kwa walio kwenye kundi hilo, na kwamba kinamama hao ambao hupatiwa chanjo ya corona wana kinga maalumu kupitia maziwa ambayo huwalinda watoto wao.

WAJAWAZITO WATARAJIWA

Kwa upande wa wanawake wanaotarajia kubeba ujauzito, AGOTA inasema kupitia utafiti uliofanyika katika nchi kadhaa hakuna taarifa rasmi zilizoonyesha madhara kwa walio katika kundi hilo iwe ni wanaume au wanawake.

UFAFANUZI ZAIDI

Jopo la wataalam wa afya wa mashirika ya Kimarekani hapa nchini, nalo pia lilitaja makundi ambayo hawastahili kuchanjwa UVIKO-19, lakini likaeleza kuwa wajawazito wanachanjwa lakini kwa kuangalia masuala muhimu ya kiafya.

Makundi hayo ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Pia ni mtu anayejisikia kuumwa mfano homa siku anayotakiwa kichanjwa na wenye nzio (aleji).

Kwa upande wa wajawazito ambao wana ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na upungufu wa damu wanatakiwa kupata ushauri wa madaktari wao kwanza kabla ya kujichanja.

Daktari wa Huduma za Matibabu kwa Raia wa Marekani wanaokuja nchini kwa ajili ya kujitolea, Dk. Arkan Ibwe, anasema kwa wenye umri huo sababu ni kuwa hadi sasa hakuna utafiti wa kuthibitisha chanjo inayofaa kwao.

Anasema kwa wanaoumwa homa siku ya kuamkia kuchanjwa wanapaswa kusubiri mpaka wapone ndipo wachanje, huku wenye aleji wanatakiwa kujulikana aina ya aleji zinazowasumbua ili kuangalia chanjo itakayoendana nao ili kuepusha madhara.

Katika maelezo yake daktari wa Elimu na Afya ya Jamii na Huduma za Uzazi wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), Dk.Emmanuel Tluway,anasema hakuna kinachozuia wajawazito kupewa chanjo.

“Lakini kutokana na hali zao wanashauriwa kupata ushauri kwa madaktari wao au wataalamu wa afya kabla ya kufanya uamuzi.”

Anaongeza: "Kutokana na mabadiliko ya mwili kwasababu za ujauzito wako katika uwezekano mkubwa wa kuambukizwa UVIKO-19 ni muhimu kuangalia faida na hasara kwanza. Kama faida ni kubwa basi wachanje kwa ushauri wa wataalam wa afya, hadi sasa hakuna utafiti unaozuia wasichanje na haijaelezwa kama utafiti wa chanjo uliwahusisha wajawazito,hivyo hatuna majibu ya kisayansi kwa asilimia 100,ila wanashauriwa wachanje."

Alisema kwa wenye ugonjwa wa kifua kikuu wanapaswa kuwasiliana na madaktari wao kabla ya kufanya uamuzi, kwa kuwa wagonjwa hao huwa katika hatua tofauti.

"Wenye magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, saratani, UKIMWI na Shinikizo la Damu wanatakiwa kuchanja lakini kubwa ni kutoa taarifa sahihi kwa mhudumu wa afya kabla ya kuchanja ili aweze kushauri vyema,"alisema Dk.Ibwe.

Kuhusu kazi ya chanjo mwilini,Dk. Tluway alisema inasisimua mwili, kuuwezesha kuamka na kupambana kwa haraka na UVIKO-19, inaimarisha kinga kwenye chembe hai (seli) nyeupe zinazohusika na kupambana na kuangamiza maradhi na kuyazuia yasiingie mwilini.

Hadi sasa Watanzania takribani 261,000 walikuwa wamepata chanjo kutoka mikoa tofauti nchini, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya.