Wajibu wa kiongozi kutambua kiu na mahitaji ya jamii yake

05Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wajibu wa kiongozi kutambua kiu na mahitaji ya jamii yake

KATIKA zama za sasa, watu wanaishi na kutenda kazi katika jamii inayobadilika kwa kasi, kiuchumi, kijamii na kisiasa na mabadiliko yanayotokea katika jamii ya Tanzania ni changamoto kwa viongozi wanaochaguliwa na kuteuliwa.

Na Dk.Enock Mlyuka

Hali inavyobadilika, ndivyo mategemeo ya wananchi yanavyobadilika juu ya uongozi. Kutokana na mabadiliko hayo, wananchi wanategemea kiongozi ambaye ana uwezo wa kiutendaji na elimu ya kutosha kujisimamia na kutoa hoja zinazoenda na wakati na kasi iliyopo.

Aidha, wananchi wanategemea kiongozi mwenye ujuzi wa kubuni mwelekeo wa eneo analoongoza, kuwasilisha mawazo thabiti ili yaeleweke na kukubalika, kusimamia utekelezaji na kutunza heshima yake binafsi na jamii yake.

Kiongozi ni mwonesha njia, lakini kiongozi bora haishii kuonyesha njia ya watu wengine kupita, bali naye hupita katika njia anayowaelekeza watu kuipita. Kiongozi bora anajua fika kuwa yupo kwa ajili na kwa niaba ya watu.

Kiongozi anayejua hivyo, anajitambua kuwa yeye ni mtumishi wa anaowaongoza ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

Uongozi ni ushawishi kwa wengine ili wamfuate, hivyo kila wakati kiongozi akiongoza, lazima ageuke nyuma na kuangalia kama kuna mtu yeyote anayemfuata. Kuna wakati kiongozi ambaye ni mtu wa mabadiliko, atalazimika kutembea peke yake kwa muda hadi watu waelewe anataka kufanya nini.

Wakati mwingine nafasi za juu za uongozi huwafanya viongozi waonekane wako peke yao, lakini haina maana hawana wafuasi.

Ni vizuri kiongozi ajitambue kwa nini yuko pale juu kwani hii ni sehemu ya gharama za mtu kuwa kiongozi. Kiongozi anapoongoza hana budi kutambua ukweli kuwa hawaongozi watu wasiojua kitu bali anawaongoza watu wenye ufahamu wa mambo tena wakati mwingine kuliko hata yeye mwenyewe.

Kufanikiwa au kushindwa kwa kiongozi kunategemea sana watu anaowaongoza. Hivyo, viongozi hawana budi kujua namna ya kuishi na kuenenda na wale walio chini yao. Viongozi wapo kuchochea tumaini na kujenga ushirikiano mzuri na wananchi. Hili ni jambo la maisha mazima ya kiongozi ni si suala la msimu au kipindi cha uchaguzi unapokaribia.

Kiongozi pia anapaswa kujali na kukerwa na matatizo ya wananchi wake na ajione ni sehemu ya matatizo hayo. Kutokana na hali hiyo, anapaswa kuchukua hatua ya utatuzi wa matatizo ya watu wake kwa wakati.

Ni fedheha kubwa kama mambo ambayo yako katika uwezo wa kutatuliwa na viongozi wa kijiji, wilaya, mkoa, wizara na taasisi zingine za serikali yatasubiri Rais au Waziri Mkuu.

Inapofikia hatua hiyo, ni dalili tosha ya viongozi katika maeneo husika hawawajibiki ipasavyo. Viongozi watambue kuwa ni watumishi na si mabosi wa wananchi. Wawe viongozi waliojaa moyo wa huruma na kuguswa na matatizo ya wananchi, kwani wananchi ndio wanaowafanya waitwe viongozi.

Viongozi pia wanatakiwa watembee pamoja na wananchi wao katika kero na huzuni zao. Watangulize maslahi ya wananchi mbele na si maslahi binafsi. Wasiwadhulumu na kuwaonea wananchi wanaowaongoza wala kutumia nafasi zao kujinufaisha.

Wawe na uongozi shirikishi kwani hakuna kiongozi atakayeweza kutatua matatizo ya watu wake bila ushirikiano na viongozi wengine na wale anaowaongoza.

UTENDAJI WA KITIMU

Ni muhimu kwa viongozi kuwa na uongozi wa kitimu katika maeneo yao. Lolote wanalofanya wafahamu wao ni timu moja yenye nia na lengo moja. Tanzania ya sasa inahitaji viongozi wenye uhusiano mwema.

Ni ukweli kwamba hata kiongozi awe mzuri kiasi gani, kama hana uhusiano na wenzake ni vigumu kufikia malengo tarajiwa.

Timu huundwa ili kuwawezesha watu kufanya zaidi yale ambayo angefanya mtu mmoja. Timu husaidia watu watumie vipawa na ujuzi ili kuleta ufanisi, pia ushirikiano hufidia udhaifu uliopo kwa kila mmoja, hivyo kuongeza tija.

Pia kiongozi si malaika, bali ni mwanadamu anayeweza kukosea, hivyo viongozi wapende kusikia mazuri na mabaya yanayowahusu na wawe tayari kukosolewa na kujisahihisha. Kukataa kukosolewa na kujisahihisha ni kukataa kukua katika uongozi.

Lakini wakosoaji nao, wanao wajibu wa kukosoa kwa staha na utaratibu. Tofauti za kimtazamo na hulka havikwepeki. Watu tofauti huwa na mawazo au mitazamo tofauti, lakini wajifunze namna bora ya kukosoa na kuwasilisha hoja za msingi kwa nia njema ya kujenga badala ya kubomoa au kutafuta umaarufu.

KUSIKILIZA KERO

Ni jukumu la viongozi kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kutoa mawazo yao na kusema kero zao. Viongozi wajenge utamaduni wa kusikiliza na kuheshimu mawazo ya wengine. Mtu kuwa kiongozi haimaanishi kujua kila kitu.

Inawezekana baadhi ya mawazo yatakayotolewa yasiwe sahihi au rafiki kwa kiongozi, lakini yatamsaidia kujua wengine wanawaza nini kuhusu yeye na utendaji wake kwani wasiposema hawezi kujua.

Katika hilo, kiongozi atajua mitazamo ya watu wake kwa kusema kwao. Kwa hiyo, wakosoaji wasichukuliwe kuwa wasaliti na wakorofi wakati wote kwani kwa upande mwingine, wanaweza kuwa msaada kwa kiongozi katika kumwimarisha, kumwongezea umakini wa kiutendaji na umaarufu.

UONGOZI NI DHAMANA

Mtu yeyote anayepata fursa ya kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa kiongozi ni muhimu atambue kuwa kinachomfanya aitwe kiongozi ni wananchi, hivyo kuwajali na kutatua kero zao ni sehemu ya wajibu wake.

Katika muktadha wa sasa, Tanzania iko katika msimu wa uchaguzi mkuu wa viongozi katika nafasi mbalimbali, hivyo Tanzania mpya inahitaji viongozi bora na si bora viongozi. Wanahitajika viongozi ambao ajenda yao kuu ni ‘Mama Tanzania’ na si familia au matumbo ya watu.

Umakini unahitajika sana, hivyo tabia ya kuchagua viongozi kwa misingi ya udini, ukabila, jinsia na ukanda hata pale mtu anapokosa sifa stahiki, inahitaji kukemewa kwa ukali. Tabia hizi hujitokeza maeneo fulani hasa nyakati za uchaguzi.

Tanzania mpya inahitaji viongozi wanaokerwa na tabia hiyo na kiongozi atambue kuwa hachaguliwi au kuteuliwa kufanya kazi ya uongozi kwa sababu alichaguliwa na mtu au kikundi fulani cha watu, bali kwa sababu ya mapenzi ya Mungu kuwaongoza Watanzania pasipo kujali hali, itikadi wala maeneo wanayotoka.

Tanzania ya sasa pia inahitaji viongozi wanaotambua kuwa matatizo ni mtaji wa uongozi. Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (marehemu), aliwahi kuwaambia viongozi wa chama na serikali kuwa: “Wakati wa amani kila mtu anaweza kuwa kiongozi. Lakini kiongozi hodari ataonekana wakati wa matatizo”.

Tanzania ya sasa inahitaji viongozi wenye utashi, mguso kwa watu, kutambua matatizo ya wananchi na uwezo wa kuyatatua. Ili kutimiza yote hayo, viongozi wanaochaguliwa na kuteuliwa, hawana budi kupatiwa semina elekezi za kiuongozi kabla ya kuanza au wakati wa kutekeleza majukumu yao ya uongozi ili kuongeza ufanisi.

•Mwandishi wa makala hii ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania (KKKT), Mtafiti na Mwanataaluma katika masuala ya theolojia, maadili na Rasilimali Watu

Habari Kubwa