Wajue mke, mume wasioona walivyonasa katika umaskini

03Nov 2017
Yasmine Protace
Nipashe
Wajue mke, mume wasioona walivyonasa katika umaskini
  • Walia watoto kuwatelekeza, kompyuta Tasaf ‘kuwasahau’

IJUMAA wiki iliyopita katika safu ya gazeti hili, ilikuwa na makala kuhusu mmoja wa wazee anayeishi maisha duni, kijijini Kisiju, akilalamika kuenguliwa katika Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Katika sehemu nyingine ya makala inayoainisha umasikini uliopo wilayani Mkuranga katika mazingira yanayoshabiliana na iliyotangulia, wapo wazee wawili; mke na mume wasioona kijijini Mlalameni.

Hao ni wazee Ramadhan Kinyogori mwenye umri wa miaka 85 na mkewe, Aisha Haruna (77), wanaodai kutokana na magumu, milo mitatu kwa siku kwao ni msamiati usiokuwamo katika kamusu yao, badala yake wanaishi kwa mlo mmoja kila siku.

Mbali na hali hiyo ngumu kiuchumi, wanandoa hao wana tatizo la kiafya, kwa kushindwa kuona vizuri, badala yake uono wao ni hafifu sana.

Wakieleza maisha yao, Kinyogori anasema katika ndoa yake, alifanikiwa kupata watoto saba, wanaoishi wilayani Bagamoyo na Kibaha mkoani Pwani.

Hata hivyo, analalamika kukosa msaada wao katika kukabili makuu ya kiuchumi yanayokwama, tangu watawanyike kimaisha baada ya kumaliza masomo.

Mzee Kinyogori anamtaka mwanawe mmoja aliyeolewa, ndiye aliwapa ‘msaada’ wa mtoto anayesoma darasa la kwanza sasa, ndiye amekuwa msaada kwao kama kuchota maji na kuwapikia chakula.

Anasema aliyewaletea mtoto hana uwezo, hivyo anawasaidia kutegemea na jinsi anavyopata, kwa sababu naye uchumi wake bado dunia sana.

Pia, anasema mara nyingi wamekuwa wakiomba kutoka kwa majirani walio na uwezo nao na anakiri kuna wakati wanachoka kuwasaidia na wanaishi kuteseka na njaa na anaelekeza kilio kwa serikali ya kijiji iwasaidie.

Mbali na chakula, Kinyogori anasema, hali yao ya maisha kwa jumla, nyumba wanayoishi haipo vizuri na hata jiko wanalolitumia ambalo liko katika hali mbaya sana.

Tasaf je?

Katika vijiji mbalimbali vya Mkuranga, Tasaf imekuwa ikiorodhesha na kuziingiza katika kaya masikini. Je, Mzee Kinyogori na mkewe, Asha, hali ikoje?

Mume huyo anajibu swali la mwandishi wa Nipashe, akisema pamoja na Tasaf kuwafikia kijijini, lakini familia yake haijaambulia chochote kutoka mfuko huo.

Kinyogori anafafanua: “Huu mfuko wa Tasaf upo kijijini, lakini hautusaidii. Baadhi ya wazee na tunaendelea kuishi katika maisha ya shida, japo tunaambiwa mfuko huo unasaidia watu wasio na kipato.”

Anataja vigezo vyake vya umasikini wake huku akilalamika kwamba yeye na mkewe hawana uwezo wa kuona kabisa, nyumba wanazoishi ni mbaya na jiko wanalotumia ni bovu sana, lakini Tasaf haikutambua changamoto hizo na kuamua kutosaidia chochote.

Anasimulia kuwa Tasaf ilipofika kijijini kwao, waliorodheshwa majina, lakini wakati wa malipo yalipotoka wakiwa miongoni mwa waliopewa, walijibiwa “kompyuta imekosea majina yao, hivyo wataingizwa tena katika mpango wa kusaidia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.”

Bila ya kutaja tarehe aliyopewa majibu hayo, Kinyogori analalama akihoji namna watakavyoishi katika kipindi cha miaka mitano wakistahimili shida walizo nazo sasa.

“Hivi Tasaf wao wana mpango na Mwenyezi Mungu? Wanaona na hizi hali zetu, bado tutakuwapo hai mpaka miaka hiyo mitano? Kama waliona kuna matatizo ya kiufundi, basi walitakiwa kufanya marekebisho mapema, ili tuweze kupata na sisi fedha za kujikimu,’’analalamika Kinyogori.

Akizungumzia hali ya maisha kwa ujumla anasema kuwa, nyumba wanayoishi haipo vizuri na hata jiko wanalotumia nalo halipo vizuri kutokana na ubovu uliokithirti.

Mke anena

Ashura Haruna, mke wa Mzee Kinyogori, pamoja na kumshukuru Mungu kwa kumpa watoto saba, sehemu kubwa ya malalamiko yake anaelekeza kwa wanawe kumnyima msaada.

Ashura, anayeona kwa shida, anasema changamoto kubwa walio nayo wana- kijiji ni kusahaulika katika mfuko wa Tasaf na kuahidiwa kufikiriwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Siku ya Wazee  

Alipoulizwa kuhusiana na namna anavyoitumia Siku ya Wazee Duniani, anakana kuifahamu yenyewe na utetezi wake kwa maslahi ya wazee duniani katika fursa mbalimbali, kama vile misaada ya Tasaf.

“Nakusikia wewe ndio unasema huwa kuna siku ya wazee duniani. Mimi siijui wala siku wazee tunatakiwa kupatiwa matibabu bure,” anasema.

Viongozi kijiji

Damas Mapunda, ni Mshauri wa Wazee kijijini Mlalameni, anayekiri kuwepo changamoto kubwa katika maisha yao na wanaishi kuwa ‘ombaomba’ kama ilivyo kwa wanandoa hao wasioona.

Pia, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mlamleni, anasimulia Tasaf ilivyofika wilayani Mkuranga mwaka 2014, kuwasaidia wasioweza na walikuta kuna idadi kubwa ya wazee wasio na uwezo.

Anasema, kutokana na changamoto kubwa ya kutokuwamo kwenye orodha ya Tasaf mna nyinginezo, wamekuwa wakichukua baadhi ya hatua kuwasaidia kama vile, kuwaandikia barua ili wapate matibabu bure.

Kwa mujibu wa sheria ya nchi, wazee wenye umri unaozidi miaka 60 wanatakiwa kupewa matibabu bure.

Viongozi Tasaf

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Tasaf wilaya ya Mkuranga, Peter Nambuga, anasema kuwa wazee wanasaidiwa kupitia mfuko wa Tasaf kwa kugharamia matibabu yao na zaidi ya Shilingi milioni zimeidhinishwa katika bajeti ya mwaka huu, kuwatengenezea wazee kadi za matibabu.

Nambuga, anasema anawataja wenye jukumu kubwa la kuwasaidia wazee, ni madiwani na wenyeviti wa vijiji, kwa kuandika barua inayomuwezesha mzee mhusika kusaidiwa.
 
Anajitetea hadi sasa kuna wazee 15,000 waliotambuliwa, ambao wanaishi katika maisha magumu wilayani Mkuranga.

Kuhusu wanandoa wawili wanaolalamika, anasema usimamizi wake uko kijijini, kwani wao ndio wanaowaibua na kuwaletea taarifa zinapelekwa Tasaf makao makao makuu, kwa ajili ya kutoa ruzuku

 
    

Habari Kubwa