Wakali 10 wa kujifunga Ligi Kuu Bara

18Mar 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakali 10 wa kujifunga Ligi Kuu Bara

KABLA ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba dhidi ya AS Vita, habari kuu ya soka ilikuwa ni beki wa KMC Ally Ally alivyojifunga bao kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yake dhidi ya Yanga.

Beki wa KMC, Ally Ally, akijaribu kumzuia straika wa Yanga, Heritier Makambo (kulia), asilete madhara kwenye goli lake. Beki hiyo alijifunga na Yanga kuondoka na ushindi wa mabao 2-1.

Ally alijifunga bao Machi 10 na kuifanya Yanga kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Tatizo halikuwa kujifunga, ila wengi walikwenda nyuma na kukutana na rekodi safi ya kuifungia Yanga mabao, huku akiwa anaichezea timu nyingine.

Rekodi zilionyesha kuwa Machi 12 Ligi Kuu msimu uliopita, Ally Ally alipojifunga bao dakika ya saba, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar  es Salaam, Yanga ikiichapa Stand United mabao 3-1.

Siku aliyoifungia KMC ilikuwa ni Machi 10, hivyo zilisalia siku mbili tu atimize mwaka mmoja tangu aifungie Yanga bao akiwa Stand, lakini siku mbili kabla akajifunga tena.

Msimu huu si Ally Ally aliyejifunga kwa kuwa kuna mlolongo wa wachezaji wengi walioweka kambani mpira kwenye goli lao wenyewe. Nao ni hawa hapa...

1. Tumba Swedi-(Coastal vs Ruvu Shooting)

Mchezaji wa kwanza kabisa kujifunga kwenye Ligi Kuu msimu huu ni Tumba Swedi wa Coastal Union. Aliweka rekodi hiyo Septemba 22, mwaka jana, timu yake ikicheza dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Hilo likawa bao pekee, Coastal ikilala kwa bao 1-0.

2. Lameck Daniel-(Biashara vs Mwadui)

Beki wa Biashara FC ya Mara, aliwafungia wapinzani Mwadui bao la kwanza kwenye mechi iliyochezwa Oktoba 7, mwaka jana katika Uwanja wa Karume mjini Musoma. Bao hilo la kujifunga liliwapa nguvu Mwadui kiasi cha kuongeza la pili lililofungwa na Ibrahim Irakoze, Biashara ikafa nyumbani 2-0.

3. Erick Murilo-(Simba vs Stand United)

Mwingine ni Erick Murilo. Huyu ni beki wa Stand United. Oktoba 21, mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, mechi ya mzunguko wa  kwanza, Simba ilishinda mabao 3-0. Emmanuel Okwi alifunga moja na Clatous Chama moja. Murilo alijifunga dakika ya 77 na kuipa Simba bao la tatu.

5. Bakari Mwamnyeto-(Coastal vs Mbeya City)

Ilikuwa ni Desemba 8, mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wakati beki wa Coastal Union Bakari Mwamnyeto alipoingia kwenye orodha ya mabeki waliojifunga wenyewe.

Aliisawazishia Mbeya City bao dakika ya 49, wakati huo ikiwa nyuma ya bao 1-0 lililofungwa na Ayou Lyanga na timu hizo zikatoka sare ya bao 1-1.

6. Omari Salum-(African Lyon vs KMC)

Januari Mosi mwaka huu, beki wa African Lyon alijifunga bao akiisaidia KMC kushinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, Hassan Kabunda akifunga bao la pili.

 

7. Peter Mwangosi-(Mbao FC vs JKT Tanzania)

Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, JKT Tanzania iliichapa Mbao FC bao 1-0 Januari 20, mwaka huu.

Bao hilo lililoifanya JKT kushinda ugenini lilifungwa na beki wa Mbao FC, Peter Mwangosi ambaye aliuweka mwenyewe wavuni kwenye harakati za kuokoa.

8. Rolland Msonjo-(African Lyon vs Azam FC)

Mechi hii ilichezwa kwenye Uwanja wa Karume Machi Mosi, mwaka huu. Azam ilishinda mabao 3-1. Mabao mawili ya washindi yakifungwa na Obray Chirwa na mwenzake Mudathir Yahaya. La tatu lilifungwa na beki wa African Lyon, Rolland Msonjo dakika ya 89.

9. Jumanne El Fadhili-(Prisons vs Singida)

Jumanne El Fadhili ni beki mwandamizi wa Prisons ya Mbeya. Machi 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida, alijifunga mwenyewe bao lililoipa ushindi Singida United dhidi ya timu yake ya Prisons na kuifanya kutoka uwanjani ikiwa imelala kwa mabao 2-1.

10. Ally Ally-(KMC vs Yanga)

 Ally alijifunga dakika ya 67 Machi 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa likiwa ni la pili na kuipa Yanga ushindi wa mabao 2-1.

Kabla hajajifunga timu hizo zilikuwa sare ya kufungana bao 1-1. Mohamed Rashid, straika wa Simba aliyeko kwa mkopo KMC alifunga bao kabla ya Papy Tshishimbi kuisawazishia Yanga.

Habari Kubwa