WAKATI NCHINI KUNA WAGENI 3000...Wana-Mbeya kushudia Kupatwa kwa Jua

01Sep 2016
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
WAKATI NCHINI KUNA WAGENI 3000...Wana-Mbeya kushudia Kupatwa kwa Jua

KUPATWA kwa Jua ni kitendo cha mwezi kuwa katikati ya Jua na Dunia. Hivyo, kivuli cha mwezi kinaangukia sehemu ya uso wa dunia na kuifanya jua kuonekana katika mwonekano usiokuwa wa kawaida.

Ni tukio hilo ambalo ni nadra, litatokea katika baadhi ya maeneo ya dunia, hasa barani Afrika, hasa kuanzia ukanda wa ilipo Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), Tanzania na Msumbiji.

Tanzania inatarajiwa kuonekana zaidi katika mikoa ya Katavi, Mbeya, Ruvuma na wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Kwingineko kwa mujibu wa taarifa hiyo ambayo inatarajiwa kuvutia wageni wengi, ni katika eneo la Rujewa wilayani Mbarali, mkoa wa Mbeya ambako litaonekana kwa ukubwa wa asilimia 90.

Inaelezwa kuwa, watu wote walioko umbali wa kipenyo cha kilomita 100 kutoka eneo Rujewa watalishuhudia tukio hilo kwa ufanisi mkubwa kwa kuliona jua katika muonekano unaofanana na mwezi mwandamo.

Aidha tukio, hilo linaelezwa kuwa litadumu kwa muda wa saa tatu na dakika 37 yaani kuanzia saa 4:17 hadi saa 7:56 mchana.

Hata hivyo, tukio hilo linatajwa kuwa litatumika na wanafunzi mbalimbali wa shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali kama sehemu ya kwenda kujifunza kwa vitendo kuhusu tukio hilo ambalo kwa asilimia kubwa, wamekuwa wakijifunza nadharia pekee.

Kutokana na umuhimu wa tukio hilo, mkoa wa Mbeya umeunda kamati maalumu ya uhamasishaji kwa wananchi na wageni, kutoka maeneo mbalimbali kwenda kushuhudia tukio hilo.

Katika taarifa yake kuhusu tukio hilo kwa vyombo vya habari, pamoja na kamati teule, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, anasema kuwa eneo la Rujewa, ililoandaliwa maalumu kwa ajili ya watu kushuhudia tukio hilo, litatumika pia kuwa darasa kwa wanafunzi.

Makalla anaitaka Kamati ya Uhamasishaji, kuhakikisha inazishawishi shule mbalimbali kwenda kushuhudia tukio hilo, lenye maana kubwa kwa wanafunzi, kwani hutokea kwa nadra.

“Septemba Mosi mwaka, huu sisi watu wa Mbeya hakutakuwa na ‘Ukuta.’Badala yake, watu wengi watakuwa wanaenda kushuhudia kupatwa kwa jua katika eneo la Rujewa, wilayani Mbarali.

“Nawashauri wana – kamati mnahakikisha shule za msingi, Sekondari na vyuo mbalimbali wakajifunze tukio hilo kwa vitendo,” anahimiza Mkuu wa Mkoa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Ulimboka Mwakilili, anasema hadi sasa zaidi ya shule za msingi na sekondari 30 za kutoka Jiji la Mbeya, zenye uwezo wa kujisafirisha, zilipewa barua za mwaliko kuhudhuria tukio hilo.

Ulimboka anataja baadhi ya taasisi za kitaaluma zilizoalikwa ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mkoani Mbeya (Must), ambacho kimeshathibitisha kupeleka zaidi ya wanafunzi 60 kwa ajili ya kujifunza.

Pia anasema kamati hiyo ilishapekeka taarifa kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, kwa ajili ya kuhamasisha shule zote jirani na eneo la Rujewa, kwenda kujifunza tukio hilo.

Mwakilili anasema kuwa, shule za mikoa ya jirani ya Njombe, Iringa na Songwe ambazo zina uwezo wa kuwa na usafiri kufika eneo hilo, zijitokeze kwa wingi.

“Tunaendelea na kazi ya kuhamasisha shule mbalimbali, kwa ajili ya kwenda kujifunza tukio hilo kwa vitendo, mpaka sasa zaidi ya shule za msingi na sekondari 30 ambazo tunazifahamu kuwa zina uwezo wa usafiri.

“Tumezipelekea barua za kuzitaka zihudhurie tukio hilo. Pia, kuna baadhi ya vyuo tumevipelekea barua,” anasema Mwakilili.

“Kwa zile shule za Mbarali, tumeuomba uongozi wa halmashauri hiyo kusaidia kuhamasisha shule za huko kujitokeza. Pia, tunahitaji hata zile shule za kutoka mikoa ya jirani zenye uwezo wa kufika Rujewam ziwalete wanafunzi kujifunza,” anasema.

Kwa mujibu wa mhadhiri wa Must, Wilson Kihunsi, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi, jua linapatwa na linakuwa na mionzi mikali ambayo ni hatari.

Kihunsui ambaye ni mtaalam wa fani hiyo, anasema mtu anapoangalia bila ya kuwa na miwani maalumu ya kuchuja mionzi, anahatarisha macho yake.

Anatumia fursa hiyo kutoa tahadhari kwa watu watakaofika eneo hilo kutoangalia jua moja kwa moja, bila kuvaa miwani hiyo maalum, ili kuepuka hatari ya kupata madhara ya papo hapo kwa macho kuanza kutoa machozi au kupata upofu baadaye.

Anasema ili kuepuka athari hizo, ameagiza miwani ya kuchuja mionzi ya jua hilo ambayo itauzwa kwa bei ya Sh. 500, ili kusaidia watu wote watakaoenda huko, wakiwamo wanafunzi kumudu kuinunua.

Mjumbe mwingine kamati hiyo, Ipini wa Ipini, anasema licha ya tukio hilo kutumika kwa ajili ya wanafunzi kujifunza, pia linavutia wanasayansi kutoka mataifa mengi duniani.

Anasema zaidi ya wageni 3000 kutoka mataifa mbalimbali duniani, wanatarajiwa kuhudhuria tukio hilo na itakuwa ni fursa ya kibiashara kwa wenyeji wa mkoa wa Mbeya ,hasa wilaya ya Mbarali.

L Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu: +255 764 232876 au anwani ya Barua pepe: [email protected]

Habari Kubwa