Wakazi Babati katika tabasamu mradi maji tangu kupata uhuru

08Apr 2021
Jaliwason Jasson
Babati
Nipashe
Wakazi Babati katika tabasamu mradi maji tangu kupata uhuru

NI tendo la kihistoria kwa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, baada ya wananchi wake tangu Uhuru kupata maji kwa mifumo rasmi.

Hasa mwaka 2019, ndio kumeanzishwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Babati, ikianza na vijiji 69 kati ya 102 vilivyokuwapo.

Meneja wa RUWASA, Mhandisi Bakari Mwanyiro, anasema taasisi hiyo ilianza na vijiji 69 na hadi sasa imefikia 75 vimeshapata huduma ya maji, ikiwa sawa na asilimia 73 ya wahitaji wote.

Mhandisi Mwanyiro anasema, upatikanaji maji uko sahihi na kuna zaidi ya wakazi 200,000 kutoka vijiji 75 wanakopata maji, matarajio ni ifikapo mwaka 2025 watafikia asilimia 85 vijiji vyote.

Anaitaja RUWASA kuwa mkombozi wa wananchi, kwa kuwa imeleta matokeo makubwa ndani ya muda mfupi, wastani wa mwaka mmoja.

Ili kulinda vyanzo hivyo vya maji, sheria inataja anayethibika mahakamani kuharibu miundombonu ya maji, yuko hatarini kukabiliwa na faini isiyopungua Sh. milioni tano au kifungo cha miaka mitano jela au vyote kwa pamoja.

MIFUMO INAYOTUMIKA?

Mtaalamu huyo anasema, wanatekeleza miradi kwa kutumia Mfuko wa RUWASA wakirithi miradi iliyokuwa inasimamiwa na halmashauri za wilaya.

Anaitaja mifumo mingine kwa majina ‘P4R’ na Programu ya Lipa Malipo kwa Matokeo (PBR), inayolenga kuboresha huduma ya maji, iliyoanzishwa na wafadhili kwa ajili ya ukarabati wa miradi chakavu, iweze kuendelezwa.

Meneja huyo anasema wilaya ya Babati wana miradi mitano inayotekelezwa, na fedha za wahisani, ikilenga kurekebisha miradi chakavu na mtarajio ni kukamilika kabla ya Juni 30 mwaka huu.

Programu ya ‘P4R’, anaitaja inaangalia kwa jicho endelevu ikifadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), ili kuimarisha miradi iliyoasisiwa na RUWASA, mmoja ni katika kijiji cha Endakiso ni kati ya miradi sita iliyopo.

MIRADI ILIYOKAMILIKA

Meneja huyo anataja miradi mingine 10 inayoendelea katika mwaka wa fedha uliopo, ikiwamo kijijini Gidas uliokwishakamilika, kati ya mitatu waliyoirithi kutoka Halmashauri ya Wilaya Babati.

Mradi wa maji wa Kijiji cha Endakiso, Mhandisi Mwanyiro anasema wameutekeleza kwa miezi sita kuanzia Juni 2020 hadi Desemba 30 mwaka huo, ujenzi wake ulikadiriwa kugharimu Sh. milioni 234 na walitumia Sh. milioni 172 hadi kukamilika. Hivyo, wameokoa Sh.milioni 62.

Mhandisi Mwanyiro anasema katika mradi huo, wamejenga vituo vinane vya kuchota maji na tanki moja lenye ujazo wa lita 90,000, kwa sasa unatoa maji kwa wakazi zaidi ya 2000.

Gharama zake anasema, walitumia bajeti anayoiita "force account" yaani mafundi jamii na wataalamu wa ndani.

Kijijini cha Gidas, wamerithi mradi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Babati, walioupokea mwaka 2018. Baada ya kukosekana chanzo cha maji, walitafuta mbadala kwa kuchimba kisima cha lita 8000 kwa saa.

Meneja anasema, mradi uliipangiwa bajeti ya Sh. milioni 354, mkandarasi akalipwa Sh. milioni152 na kisima kikachimbwa kwa Sh. milioni 64 mradi ukaanza kutumika tarehe 16, mwezi uliopita, ukiwa umeokoa Sh. milioni 138.

Mhandisi Mwanyiro anasema, tayari wameshajenga vituo 18 vya kuchota maji, wameweka umeme na kujengwa tangi la lita 100,000 na kisima. Tayari mradi unawahudumia wakazi zaidi ya 4,000 wa vijiji vya Gidas na Endiamet.

Anataja mradi mwingine ni waliourithi kutoka Halmashauri ya Wilaya Babati, uliokamilika katika eneo Shaurimoyo na sasa imejengewa tangi la lita 50,000.
            
WANANCHI WANENAVYO

Mkazi wa kijiji cha Gidas, Rebecca Joshua, anaishukru RUWASA kuwaletea maji safi na salama, kwani awali waliugua tumbo na maradhi kama amiba, kwa kutumia maji ya madimbwi.

Anakiri ni jambo ambalo hawakulitegemea kupata maji hadi mlangoni. Anasema:"Tulikuwa tunatumia maji ambayo watu wanajisaidia na mifugo wanatumia ila sasa hivi tuna raha sana unaweza ukachota hata ndoo mbili ukakaa."
 
Mkazi mwingine, Gidas Valian mwenye umri miaka 69, anaendeleza ushahidi kwamba walipata shida ya kuamka saa 9.00 usiku kwenda kuchota maji, kwani mchelewaji hakupata maji.

"Usiku tulikuwa tunatembea na tochi. Nilikuwa nikichota maji naficha kwanza, halafu mchana nilikuwa nachota maji ya mifugo," anasema.

Mkazi wa kijijini Endakiso, Halima Dai, bila ya kutaja umri, anajitambulisha alifika kijijini hapo mwaka 1973, hakukuta huduma ya maji, akieleza: "Huko nyuma tulikuwa tunauziwa ndoo moja ya lita 20 Sh. 500, hivi sasa pipa Sh.100 ( ndoo 13).”

Mkazi wa Kijiji cha Maweni, Zuwena Kimaro, anasimulia shida zao hata kuishia kunywa maji ya makorongoni kwa watu maskini, lakini sasa mradi umewakomboa, kwani nyuma aliugua tumbo, Typhod na Amoeba kwa kuwa alikuwa anatumia maji machafu.

WASIMAMIZI VIJIJINI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji Maji wa Kijiji cha Endakiso, Said Issa, anasema jukumu lake ni kusimamia mradi uwe endelevu na kupanga bei kwa kuwashirikisha watumiaji.

Issa anasema, mradi unawaonyesha matokeo mazuri pale hata wananchi wanaposhangaa kununua maji ndoo moja ya lita 20 kwa bei Sh. 10.

"Leo tuna uhakika kila mtu kufikishiwa maji nyumbani kwake," anasema Issa, huku akihamasika na wenzake kudhibiti uharibifu wa miundombonu ya maji.

Diwani wa Kata ya Kisangaji, Adam Ipingika, anaahidi kuendelea kutoa elimu ya utunzaji miradi, huku akiazimia kuzisimamia tozo ili kufikia malengo," anasema.

Diwani huyo ana rai kwamba RUWASA isichoke ‘wamtue mama ndoo kichwani; walau kila mita umbali 400, ambayo ndio mtazamo wa kisera nchini.

Mwakilishi huyo wa wananchi, anasema walipata athari za kuugua magonjwa kama homa ya matumbo (typhoid) na amiba kutokana na kutumia maji machafu na idadi ya wagonjwa waliongezeka katika zahanati yao, hali iliyobadilika sasa idadi hiyo inashuka.

Anasema, iliendana na taarifa za wanandoa wengi kugombana kwa kisa kuchelewa kuchota maji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Shaurimoyo, Dismas Morembwa, anasema kabla ya RUWASA kuwajengea mradi wa maji, wananchi walikuwa wanaenda milimani na walikutana na wanyama wakali.

Morembwa anaaihidi kuitunza miradi, akifafanua wataongeza vituo vya kuchota maji baada ya kukusanya mapato.

Habari Kubwa