Wakulima wa tumbaku wako Hoi, wazidi kuwa maskini

05Jul 2019
Neema Sawaka
KAHAMA
Nipashe
Wakulima wa tumbaku wako Hoi, wazidi kuwa maskini

KINACHOWALIZA wakulima wa tumbaku wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga leo ni hiki: “Tumbaku badala ya kuwa mwarobaini na suluhu ya janga la umasikini linalowakabili inakuwa mwiba unaowatesa kila siku.”

Wakulima wakiuza tumbaku yao kwenye Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) wilayani Kahama.PICHA: MTANDAO

Wakulima hao kila leo wanajiuliza maswali mengi ya namna wanavyokwenda kulipa madeni ya pembejeo na mikopo ya mabenki yenye riba kubwa inayowakabili na kujikuta kwenye lindi la umaskini .

Wakizungumza kwenye mahojiano maalumu hivi karibuni na Nipashe, wakulima wa zao hilo safari Manjara na Jonas Mponya walisema waliamua kwa dhati kuwekeza rasilimali fedha na nguvu kwenye zao hilo kwa lengo la kuongeza uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi na kuongeza kasi ya  maendeleo  katika  mkoa wa  kitumbaku  wa Kahama , lakini badala ya furaha ni kilio.

Wanaongeza kuwa pamoja na dhamira  ya serikali ya  awamu ya tano ya  Rais  John Magufuli ya kuwa na Tanzania  ya viwanda ili wakulima nao wanufaike kupitia  mazao yao ikiwamo tumbaku, hawana tumaini kwa kuwa bei ya kinachozalishwa ni ndogo na gharama ni kubwa.

Jonas  Mponya, anasema mpango huo  na juhudi za  serikali zinakwamishwa na  baadhi ya kampuni zinayojihusisha  na ununuzi  wa  tumbaku, ambazo  zimekuwa zikitoa na kununua  bei za chini  ya wastani wa kitaifa  dola 1.73 kwa kilo ambayo  hailingani na gharama za  uzalishaji  ambayo  iko chini ya  bei  ya  kitaifa  iliyopagwa.

 Safari Manjala   ambaye  anawakilisha   kilio cha wakulima  hao  anasema sera ya  viwanda  haiwezi  kufikiwa   kwasababu  mzalishaji  wa  malighafi  ambaye ni mkulima  atakuwa  hapati  bei  stahiki kwa zao la tumbaku .

“Tumbaku  ina  madaraja 45, la kwanza  mpaka  la 45 ,  Kwa mtazamo  wangu kumekuwepo na  mashinikizo  kutoka  kwenye kampuni ya ununuzi  wa tumbaku mfano TLTC na Alliance One tumbaku  ya daraja  la kwanza  na la pili  hawataki kuziona  zikinunuliwa wanatafuta  sababu  mpaka  zifutwe na wanunuzi  wa  kampuni huwalazimisha ,”wanunuzi wa serikali ambao ni Bodi ya Tumbaku (TTB), kuondoa  madaraja hayo…”Anadai.

“Baada ya kuondoa madaraja hayo na kushusha  bei yake ndipo kampuni zinaanza kuinunua , wanunuzi wananunua  kwa bei ya  chini  ya wastani  wa kitaifa , hali  ambayo  inampelekea mkulima kuishia  kulipa  madeni ya  gharama za pembejeo  alizokopa na baadhi yao kushidwa kulipa madeni” anasema  Safari  . 

Jambo ambalo wanaona ni kitu kigeni na hali hiyo sasa inawafanya wakulima  kuwa wanafanya kazi bure  sawa na kugawa tumbaku zao kwa kampuni wanunuzi.

Anaomba serikali iliangalie  suala hili  kwa upana  pamoja na kuzisimamia na kuzirekebisha  sheria  za tumbaku  kwani kwenye  masoko hali imebadilika  na inakuwa  mwamuzi  wa  mwisho ni kampuni.

Japo bei ya wastani wa kitaifa ni Dola 1.73  lakini wakulima wanauza  masoko  yanayosimamia watani wa Dola 1.5 kwa kilo na hiyo inasababishwa na wanunuzi kutokuzitendea  haki tumbaku za madaraja ya kwanza na ya pili.

Wao wanapenda wakute daraja la tatu kushuka chini hali inayomkwamisha mkulima kujikwamua kiuchumi.

“Sababu kubwa ni kutaka kumkandamiza mkulima na kumnyonya kwa lengo la kujipatia faida kubwa  na hali hiyo iko kwenye kampuni kadhaa (majina tunayo) na kwenye Chama cha Msingi cha  Mkwawa Amcos, wameuza  zaidi  ya kilo 200,000  kwa wastani  wa Dola  1.5  jambo ambalo  halilingani na gharama za uzalishaji”alisema Safari  Manjala .

MAELEZO YA BODI

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, Stanley Mnozya, alisema  jumla ya kilo milioni 61 za tumbaku zimezalishwa  nchi nzima.

 Mnozya alipotakiwa kuzungumzia changamoto hiyo  alikiri kuwapo kwa  changamoto hiyo  kwenye  baadhi  ya  kampuni  za ununuzi  wa tumbaku  na kuongeza Kuwa   TLTC  ilionywa  na bodi kuhusu  kununua bei ya chini  ya wastani  na kuwa na usumbufu kwenye  masoko  na kulazimisha  dosari  kwenye  madaraja ya  tumbaku.

Mnozya alisema mpaka sasa wakulima wamegomea  zaidi  ya  masoko manne, akitoa ufafanuzi alisema  mkulima ana uhuru wa  kukubali  ama kukataa kusaini kuuzia soko ambalo  linampunja.

Alisema Chama cha Amcos  Mishamo  katika mkoa wa Katavi  kiligomea  masoko  na Nsimbahiari   na Msimba Amcos kutoka kampuni ya  TLTC waligomea masoko  yao  yasisainiwe Tabora mpaka uongozi  wa bodi  ulipoingilia kati .

Kwa upande  wake  Meneja Uendeshaji wa Kampuni  ya TLTC  George   Ibrahimu,  anasema tumbaku  inaweza  ikanunuliwa  hata kwa Sh. 300 au  200 na kuongeza kuwa Dola 1.73 kwa kilo ni bei ya wastani wa kitaifa  lakini mambo yaliyoandikwa  kwenye  makaratasi tu .

Mkurugenzi  wa Uzalishaji  wa Alliance One,  Mayunga David, alipotakiwa kujibu malalamiko  hayo alisema wastani  wa bei ya tumbaku unaendana na ubora wa tumbaku na kuongeza kuwa kuna vyama  ambavyo viko  chini na vimeuza  kwa wastani  wa bei ya chini sana, na vyama vingine  kwa wastani  wa juu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa TCB, Stanley Mnozya, TLTC imenunua kilo  milioni 9, Alliance One, milioni 12 na  kampuni  ya  JTI ikinunua kilo milioni 5.5.

Habari Kubwa