Wakulima waandaliwa mazingira masoko ya nje

21Sep 2016
Mary Geofrey
Nipashe
Wakulima waandaliwa mazingira masoko ya nje

SERIKALI imeandaa mafunzo yatakayowawezesha wakulima wa viungo na mboga nchini wanapata soko la mazao yao nje ya nchi kwa kutumia vifungashio ili kuongeza ubora na thamani ya bidhaa wanazozalisha.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacqueline Maleko (katikati).

Hatua hiyo imelenga kuhakikisha wakulima hao wanapata soko la mazao yao nje ya nchi.

Mafunzo hayo ambayo yatatolewa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), yatatolewa kwa wakulima zaidi ya 200.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma wa Tantade, Theresia Chilambo, katika taarifa jijini Dar es Salaam jana alisema wameandaa warsha hiyo ili kuwajengea uwezo wakulima kuhusiana na vifungashio na lebo vitakavyowasaidia kuzingatia nyenzo na viwango vya ufungaji ili kuboresha ubora na uwasilishaji wa bidhaa za ndani.

Alisema mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa wakulima wa vijiji vya Matombo, Mkuyuni, Mgeta na maeneo ya Bonde la Mto Ruaha mkoani Morogoro, yatalenga pia kuimarisha viwango vya kimataifa vya ufungaji na kupata masoko ya kikanda na kimataifa.

Chilambo alisema mafunzo hayo yaliyoanza juzi na yatamalizika Septemba 24, mwaka huu, yatahusu pia masuala ya ubora na vifaa vya kiwango cha ufungaji wa bidhaa za viungo na malimbichi kama vile mdalasini, karafuu, pilipili manga, nyanya na vitunguu.

"Katika siku hizo sita mafunzo ya kina yatakayofanyika, yatawaelimisha wakulima wa malimbichi jinsi ya kutambua aina mbalimbali za ufungaji wa bidhaa zao, kulebo bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi na kutoa taarifa kwa uwazi juu ya upatikanaji wa vifaa vya ufungashaji," alisema Chilambo.

Mbali na hilo, mpango wa mafunzo hayo utasaidia kuongeza uwezo wa wazalishaji wa malimbichi, kuboresha maarifa katika ubora wa wazalishaji na kubaini soko la kuaminika ndani ya nchi kwa wingi, kampuni ya usindikaji, hoteli na mengine ya kuuza nje.

"Ushirikiano baina ya TanTrade na washirika/wadau wa kimkakati ambao ni Sido, TBS na Mviwata, utaimarisha fursa kwa wakulima kuzalisha kitu cha thamani ili kuleta ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi," alisema.
Pia aliwataka wakulima waliolengwa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kuwasaidia kushughulikia mahitaji na matakwa ya ufungaji, uwekaji na kulebo bidhaa zao kwa kiwango.