Walemavu Zanzibar wanapoambiwa wakache udako badala ya kushiriki siasa

02Mar 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Walemavu Zanzibar wanapoambiwa wakache udako badala ya kushiriki siasa

KILA kinapofika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wadau mbalimbali hujitokeza kutaka kutoa elimu ya uraia kwa makundi tofauti wakiwamo walemavu.

Fatma Abubakar Ali.

Ni jambo zuri kwa kuwa linajaribu kufungua vichwa na mawazo ya jamii nzima na kuiweka tayari kuingia katika uchaguzi.

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Uwakilishi katika jimbo la Kikwajuni visiwani Zanzibar kupitia Chama cha TADEA, Fatma Abubakar Ali, anasema machache kuhusu nafasi ya walemavu katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana.

Fatma anasema bado jamii inawanyanyapaa watu wenye ulemavu Zanzibar na kwamba wakati anagombea nafasi hiyo aliambiwa maneno ya kumdhalilisha utu wake.

“Ni kweli nilijisikia vibaya siku moja kabla ya uchaguzi wa Oktoba 25, kipindi cha kampeni nilipita eneo la Raha leo nikawakuta akinamama wamekaa barazani na kuanza kuomba kura, lakini nilijibiwa kwaba kwa nini naacha kwenda kucheza mdako nagombea uwakilishi," anasema.

Mchezo wa mdako huchezwa na watoto kwa kutumia mawe moja linarushwa juu huku mwengine yakitolewa ndani ya shimo na kuyarudisha.

Fatma ambaye ni mlemavu wa viungo anasema bado kuna kuna vikwazo vingi vinavyowakabili watu wenye ulemavu hasusasani wanapotaka kugombea nafasi za kisiasa.

Anasema hakukata tamaa na badala yake aliendelea na kampeni zake kama kawaida kwani alijua hayo yalikuwa maneno ya makusudi ya kumkatisa tamaa.

Fatma ni mgombea pekee mwanamke ambaye ni mlemavu aliyejitosa kupigania nafasi hiyo ya kisiasa katika visiwa hivyo.

Anataja vikwazo vilingine alivyokumbana navyo na miundombinu haikuwa mizuri kwake ili kumuwezesha kutoka eneo moja kwenda lingine.

Anasema alishindwa kupanda juu ya nyumba za ghorofa kwa ajili kufanya kampeni za nyumba na kwamba hatua ambayo ilikwamisha ndoto zake za kuwa kiongozi wa kisiasa.

“Wagombea wezangu ambao hawana ulemavu waliweza kupita nyumba kwa nyuma kuomba kura lakini mimi nilishindwa kutokana na hali yangu”anasema.

Kikwazo kingine anachokiona ni uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kufanyia kampeni ikiwamo kuandaa mikutano kampeni.

Fatuma anasema kwamba ugumu mwingine wa kufanya kampeni hizo ulitokana na kujitegemea mwenyewe kwa kila kitu kwa kuwa chama chake hakipati fedha za ruzuku.

Kutokana na mazingira ya kampeni kuwa magumu mara kadaa alilazimika kutumia vyombo vya habari ili kuwafikia wapigakura na kuomba wamchague.

“Sikufanya mkutano wa hadhara hata mmoja kwa sababu nilikuwa sina fedha na mkutano unahitaji gharama niliomba kura kupitia vyombo vya habari na siyo watu wote wanaosikiliza vyombo hivyo,”anasema.

Kuhusu wanawake kumuunga mkono, Fatuma anasema jambo hilo ni gumu kwa kuwa hakuona ushirikiano wowote hatua iliyomfanya apate kura 30.

Uchaguzi uliofanyika octoba 25 mwaka jana ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), kutokana na sababu mbalimbali na sasa unarudiwa mwezi ujao.

Hata hivyo, Fatuma anasema licha ya kuwapo vikwazo mbalimbali ambavyo vilimfanya ashindwe kufikia malengo yake bado anataka kujaribu tena kipindi kingine.

Mwanasiasa huyo anaiomba ZEC kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kuwawezesha watu wenye ulemavu katika uchaguzi wa marudio ambao utafanyika Machi 20, mwaka huu.

Licha ya changamoto na vikwazo vingi vilivyomkuta mgombea huyo katika kampeni za uchaguzi uliopita lakini anasema bado hajakata tamaa na ana imani kubwa kwamba atashinda katika uchaguzi wa marudio.

Analenga kuwa mtetezi mzuri wa watu wenye ulemavu na wanawake ndani ya Baraza la Wawawakilishi akama atafanikiwa kushinda katika uchaguzi.

“Kwa miaka mingi tumekosa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kututetea sisi watu wenye ulemavu, lakini pia sisi watu wenye ulemavu hatujapata nafasi ya kuchaguliwa majimboni ili kwenda kuwawakilisha wananchi," anasema Fatma.

Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar, Mwandawa Khamis anasema, bado ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika siasa ni mdogo.

Anasema hatua hiyo inatokana na inatokana na uwezo mdogo wa kifedha walionao wanawake wenye ulemavu na kukithiri kwa rushwa katika mchakato wa kugombea nafasi za uongozi katika siasa.

Mwandawa anasema bila ya kuwa na pesa jamii au wafuasi wa vyama vya siasa hawakuelewi maana siasa za siku hizi lazima uwe na fedha angalau za kuwapa wapiga kura ili wakusikilize na kukuchagua.

Habari Kubwa