Walima mpunga wapigwa msasa maji, ardhi ‘kiduchu’mavuno kibao

07Dec 2018
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Walima mpunga wapigwa msasa maji, ardhi ‘kiduchu’mavuno kibao

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo inayoshirikiana na Benki ya Dunia, ina mpango wa kuwainua walima mpunga waboreshe kilimo chao, hadi kufikia kilimo cha kibiashara, ikiwa na sura pana ya manufaa kitaifa

Ofisa Kilimo, kutoka Wizara ya Kilimo nchini Henry Urio, anasema kupitia mradi huo wa kuongeza tija na uzalishaji wa zao la mpunga kwa wakulima (ERPP) mkoa wa Morogoro kwa Tanzania Bara na kwa Unguja na Pemba, kwa upande wa Visiwani, kuna mpango wa kujenga maghala matano katika maeneo ya skimu za umwagiliaji.

Anasema, skimu hizo zipo katika maeneo ya mradi na lengo ni kufanya wakulima waweze kuhifadhi mazao yao ghalani, wakutanishwe na masoko.

Urio anasema, mpango huo unalenga kufungua dira inayomwonyesha mnunuzi mazao yakiwa pamoja, sambamba na kutoa elimu ya utunzaji salama mpunga au mchele kwa wakulima na kuwapa taarifa za masoko zilivyo kwa wakati.

Mtaalamu huyo kilimo anaeleza kwamba hilo litasaidia kujenga wepesi katika upatikanaji wa masoko tofauti na hali iliyoko hivi sasa, kila mkulima anabaki na mazao yake akiwa na maamuzi binafsi

Kwa mujibu wa Urio, skimu zitakazowekewa maghala mapya ni Njage na Msolwa Ujamaa zilizoko wilayani Kilombero, Mvumi wilayani Kilosa, pia Kigugu na Mbogo kwa Mtonga wilayani Mvomero.

Urio anasema, ni mpango unaobeba dira ya kuhakikisha kunakuwapo kilimo cha kibiashara, kwa wakulima kuendelea kupata mafunzo, Urio anasema wana mpango wa kukarabati barabara za kuelekea ziliko skimu za Mvumi wilayani Kilosa na Njage, Kilombero, ili kusaidia usafiri na usafirishaji wa mazao kabla na baada ya mavuno,

Pia, kuna maboreho katika skimu nne za umwagiliaji ambazo ni: Kigugu (Mvomero), Mvumi (Kilosa), Njage na Msolwa Ujamaa (Kilombero) na Shamba la Mbegu la Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA) jambo litakaloisaidia taasisi hiyo kuwa na eneo kubwa litakalokidhi mahitaji ya mbegu kwa wakulima.

Anataja manufaa hayo ni kusaidia wakulima kutumia maji kwa ufanisi ikitoa faida ya kuongeza uzalishaji na kuboresha mapato, ukuaji kilimo biashara.

Urio, pia anakumbusha kwamba wizara yake ina kipengele cha kutoa ‘ruzuku kwa wakulima’ katika kuchangia gharama za mbegu na mbolea ili kuboresha kilimo hicho.

“Kwa mfano, mfuko wa mbolea unauzwa Sh.60,000 mkulima atatakiwa kuchangia Sh. 30,000.Mradi utachangia Sh.30,000 ili kumfanya mkulima kuweza kumudu kilimo hicho, kwani kinahitaji utaalamu, mbegu bora na mbolea” anaeleza Urio.
Kilmo Shadidi

Urio anasema, hadi sasa wameshatoa mafunzo ya Kilimo Shadidi cha mpunga kwa wanavyuo wa sekta hiyo, ikiwemo Chuo cha Kilimo Mkindo, wilayani Mvomero na wamewapata wakulima viongozi wanaoendelea kuwafundisha, kufanya elimu iwafikie wengi zaidi.

Akizungumzia Kilimo Shadidi kwa wakulima 64 watokao katika wilaya saba za mkoani Morogoro, wakiwa jijini Arusha, Meneja Uzalishaji wa Wakala wa Mbegu Tanzania (ASA),Mkoa wa Morogoro, Charles Levi, anaeleza umuhimu wa kilimo cha biashara.

Levi anasema, wameamua kuwapeleka wakulima hao kujifunza ili kupata elimu kwa vitendo kupitia mashamba darasa ya Arusha ikiwemo skimu ya Umwagiliaji ya Lekitatu.

Levi anasisitiza kwamba Kilimo Shadidi ni kisasa zaidi katika mpunga na kinatumia eneo dogo, mbegu kidogo, maji kidogo lakini kinatoa mavuno mengi.

Anasema wakulima wengi wanaegemea mbinu za kilimo cha kizamani, zinazowafanya watumie mbegu nyingi huku maji mengi yanaruhusiwa yaingie shambani muda wote.

Kwa mujibu wa Levi, hiyo ni kimyume na sasa, Kilimo Shadidi, maji yanaingia kwa wakati na kutolewa kupisha hewa kuingia kwenye mpunga ukiwa shambani.

Hivyo, ushauri wake kwa wakulima hao wa Morogoro, Kilosa, Ulanga, Kilombero, Malinyi, Mvomero na Gairo, wabadilike kupisha kilimo cha mazoea na kujiunga na Kilimo Shadidi.

Pia, anawaasa wataalamu wenzake wa kilimo kuwasaidia wakulima, hasa wakati wanapokumbwa na changamoto za kilimo, ikiwemo wakati sahihi wa kuweka mbolea shambani.

Anasema msaada unahitajika sana katika uchaguzi wa mbegu, hasa kutoka wakala wa mbegu wa serikali na uchaguzi unafafanua kuhusu mbolea, kwamba ichaguliwe kulingana na uhalisia wa udongo

Levi anasema, Morogoro ni mkoa unaojihusisha na kilimo cha mpunga kwa miaka mingi na sehemu kubwa ya wakulima wake wanatumia mbegu za kienyeji na baadhi wanarudia mbegu zilezile na kupoteza masoko.

Ushahidi wa mkulima

Mkulima anayeendesha Kilimo Shadidi cha mpunga kutoka Skimu ya Umwagiliaji Lekitatu, Arusha, Kapteni Mstaafu, Rogart Mrema (78), anasema kwa kutumia mbegu sahihi na kufuata kanuni za Kilimo Shadidi, amefanikiwa kuinuka kiuchumi.

Mrema anasema kabla ya kwenda mafuzoni, walianza kulima kwa vijaruba vidogo, vilivyomwezesha kuvuna kati ya gunia 16 na 18 kwa ekari, lakini baada ya mafunzo anavuna maradufu.

Anasema katika ya mwaka 2017/18 akifuata kanuni za kilimo shadidi, amevuna kati ya gunia 35 na 46 kwa ekari.

Pamoja namafanikio hayo,mkulima huyo anatoa angalizio muhimu kwa kilimo shadidi, kwamba kinahitaji kuzingatia kalenda, kuanzia upandaji miche na uwekaji mbolea, jambo litakalomfanya kwenda sambamba na ratiba ya maendeleo ya shamba.

Wataalamu shambani

Sphora Masha, ni Ofisa Kilimo wa Kata ya Usa River, wilayani Meru, anayewataka wakulima kuona umuhimu wa kuweka mbolea, hata kama ni ya samadi siku chache baada ya kupanda miche yao ya mpunga ili kuongeza uzalishaji na shambani.

“Wakulima wa huku mna tabia ya kuuza majani yote yanayobakia wakati wa uvunaji na jambo hilo hufanya shamba kuwa tupu kabisa na kuzidisha shamba kukosa rutuba. Sasa ili kufanya mazao yawe na rutuba mbolea lazima” alisema Masha.

Aisha anawashauri wakulima, kutotumia sumu kila wanapohitaji na wasipige dawa kila wakati wanapowaona wadudu, ili dawa zisizidi na kuleta athari ya sumu kuvu inayotisha afya ya walaji.

Masha anasema, wanaendelea na utafiti wa mbolea na sumu wanazotumia kuepusha athari za sumu kuvu kwa mlaji na usalama wa chakula kwa jumla.

Mshauri wa Kilimo Mkoa wa Morogoro, Dk. Rozalia Rwegasira, anawataka wakulima kuzingatia elimu ya uhifadhi mazao ghalani wanayopewa kuwaepusha na hasara, kwa kuuza mazao kabla ya bei kupanda.

Dk. Rwegasira, ambaye pia ni Mratibu wa mradi huo mkoani Morogoro, anawashauri wakulima kushirikiana ili kuwa na sauti moja, hasa wanapokumbwa na tatizo.

Pia, anawataka wasiegemee kilimo cha mpunga pekee, bali watanue wigo kwa kuwa na shughuli nyingine, ikiwemo kilimo cha mboga baada ya msimu wa mavuno ili iwaongezee kipato.

“Tamaa ya pesa na kuuza mpunga mapema bila ya kusubiri soko kupanda, ni wazi utashindwa kuona maendeleo ya kilimo. La muhimu, ni kuzingatia kutouza mpunga mapema na kuitikia wito wa serikali kwa kuweka mpunga kwenye maghala, hivyo msiuze wala msipate tamaa ya kuuza,” anasema Dk. Rwegasira.

Wakulima Moro

Wakulima kutoka mkoani Morogoro, wanashukuru kupewa fursa ya mafunzio kwa vitendo kuhusu elimu ya kilimo shadidi cha mpunga, akiwamo Juma Gwalu kutoka Mkindo mkoani Morogoro.

Anakiri kilimo cha umwagiliaji kwa kufuata kanuni za kilimo shadidi cha mpunga ni bora kuliko walivyolima zamani, kabla ya elimu hiyo kutolewa.

Gwalu anasema, walikuwa wakipata magunia 22 hadi 25 kwa hekta moja na baada ya elimu wameweza kupata gunia 48 hadi 47 kwa hekta, hivyo kupata zawadi kwa kuwa wakulima bora kwa kuongeza mazao mwaka 2017/.

Salima Selemani, kutoka Duthumi wilayani Morogoro, anasema wamehamasika na kilimo hicho na kujipanga kuanzisha kilimo biashara, lakini wanashindwa kuwa makini, kutokana na kukabiliwa na changamoto ya kukosa maji ya kutosha kwa ajili ya kuanzisha skimu za umwagiliaji.

Anasema, kilimo hicho kinaendeshwa kwa msimu tu licha ya kuwa na mabonde ambayo hayana maji muda wote. Hivyo, ameomba wadau wawasaidie katika uandaaji mabwawa ya umwagiliaji, kunufaika na kilimo hicho.

Ofisa Kilimo Wilaya ya Gairo, Misibo Ntirangiza, anasema wanatumia mbegu anazoziita ‘Mpunga wa Mlimani’ kuwasaidia kuchimba mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua na kuhifadhi kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, ili wafaike zaidi na kilimo shadidi cha mpunga.

Ofisa Kilimo - Urio, anasema mradi huo ulianza kutekelezwa katika maeneo hayo mwaka 2015 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.