Walimu tuna fursa nje ya ufundishaji

09Nov 2019
Reubeni Lumbagala
Dodoma
Nipashe
Walimu tuna fursa nje ya ufundishaji

NI jambo muhimu linalotamaniwa na kila mtu kufanya shughuli zaidi ya moja kwa ajili ya kujiongezea mapato. Ni kutokana na ukweli kuwa hakuna chanzo kimoja cha kipato kinachoweza kutosheleza mahitaji yote ya binadamu.

Ndiyo maana wanauchumi wanashauri mtu kuwa na vyanzo ya kujiingizia kipato zaidi ya kimoja ili kuweza kutimiza mahitaji ya msingi na kufanya maendeleo mengine muhimu kwa ajili ya ustawi wa maisha.

Walimu kama watu wengine kwenye jamii, nao wanapaswa kuwa na shughuli za ziada za kujiongezea kipato nje na kazi yao ya ufundishaji ili kuweza kumudu kuendesha maisha yao kwa mafanikio.

Na ndiyo maana baadhi ya walimu wanajishughulisha na kilimo, ufugaji, biashara, kuandika vitabu na kufundisha masomo ya ziada (tuition) ili kuweza kupata kipato cha ziada.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina utaratibu wa kusimamia na kuratibu Mashindano ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara (Umisavuta) ili kuweza kuibua na kuendeleza vipaji vya walimu kupitia mashindano hayo.

Ufunguzi wa mshindano haya kwa mwaka huu, umefanyika mwezi uliopita (Oktoba 27, 2019) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Katika ufunguzi huo Waziri wa Habari Dk. Harrison Mwakyembe, alikuwa mgeni rasmi, akimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Mashindano hayo yaliyofanyika kwa takribani wiki moja yalishuhudia washiriki zaidi ya 5,600 kutoka katika vyuo vya umma vya ualimu 35.

Mashindano ya Umisavuta yamejumuisha michezo ya aina mbalimbali kama vile mpira wa miguu, wavu, kikapu, pete na riadha.

Kwa upande wa sanaa, imejumuisha ngoma, uchoraji, kwaya, maonyesho mbalimbali. Baada ya ufunguzi wa mashindano hayo, viwanja vya michezo vya vyuo vya Ufundi cha Ualimu Mtwara vilitumika kuendesha michezo na sanaa hizo kwa walimu washiriki.

Pamoja na walimu kusomea taaluma ya ualimu ambayo wanawajibika moja kwa moja katika kuwafundisha wanafunzi na kuwapatia maarifa, ujuzi na stadi mbalimbali lakini wanayo fursa ya kutumika vipaji vyao walivyojaliwa na Mungu katika kujiongezea kipato nje na mishahara yao ya ualimu.

Mashindano hayo si tu kwa ajili ya kujenga afya na burudani lakini pia ni njia mojawapo ambayo walimu wakiitumia vyema inasaidia katika kuwapatia walimu fursa za kiuchumi. Mashindano haya huwashirikisha wadau mbalimbali ambao kwa njia moja au nyingine wanatafuta wanamichezo na wasanii wa sanaa mbalimbali.

Hivyo basi, Umisavuta ni njia ya kujinadai na kujitangaza kwa wadau wanaotafuta vipaji mbalimbali. Mathalani, walimu wenye vipaji katika michezo ya mpira wa miguu, pete, kikapu wavu au riadha wanaweza kuchukuliwa na kujiunga na timu mbalimbali.

Fursa hii inawapa walimu wasaa wa kuendelea na kazi yao ya ufundishaji huku wakitumia muda wa ziada katika michezo hiyo.

Aidha, walimu wenye vipaji vya uchezaji na upigaji wa ngoma za asili, uimbaji, uigizaji na uchoraji, wanaweza kujipatia kipato cha ziada kupitia sanaa hizi.

Halikadhalika walimu wanaweza kutafuta fursa katika magazeti na majarida mbalimbali katika uchoraji wa picha na katuni ili kutoa elimu kupitia uchoraji.

Vipo vikundi vya uimbaji na wachezaji wa ngoma ambavyo vinatumbuiza katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiserikali, walimu wenye vipaji vya uimbaji, kucheza au kupiga ngoma wanaweza kupata fursa hii adhimu na kutunisha mifuko yao.

Kwa hiyo, walimu wawapo vyuoni wakijifunza taaluma ya ualimu, watambue kuwa wanaweza kutumia vipaji vyao katika kuongeza thamani ya maisha yao kwa kupata kipato ziada nje na ufundishaji shuleni au vyuoni.

Mashindano haya yawe chachu na yawaamshe walimu katika kutumia vipaji na karama walizonazo kujitangaza kibiashara badala ya vipaji vyao kutumika kama burudani pekee.

Wanamichezo na wasanii ni watu wenye vipato vikubwa duniani na kupitia michezo na sanaa wanazozifanya, wamejikuta wakiwa mabilionea na mamilionea.

Kwa mantiki hii, walimu nao wanaweza kuwa mabilionea na mamilionea kama watatumia vipaji vyao ya michezo na sanaa badala ya kubaki na kazi moja ya ufundishaji huku wakiwa wamebarikiwa kwa kuwa na vipaji lukuki vinavyohitajika katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu na nje ya nchi.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ihakikishe Umisavuta inakuwa endelevu ili kuendelea kuwatengenezea fursa walimu na kukuza umoja baina ya vyuo vya ualimu.

Pia serikali ivishirikishe vyuo binafsi vya ualimu ili nao waweze kushiriki na kuibua vipaji vya walimu. Walimu nao wasibaki nyuma katika kushiriki kikamilifu katika mashindano haya na kuchagua michezo na sanaa ambazo wanaweza kufanya vyema kitaifa na kimataifa. Tutafakarini walimu.

Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Maoni: (+255) 764 666349.

Habari Kubwa