Walio na magonjwa sugu wameathiriwaje kipindi cha mlipuko wa Covid-19?

24Nov 2020
Jenifer Gilla
Dar es Salaam-Tanzania
Nipashe
Walio na magonjwa sugu wameathiriwaje kipindi cha mlipuko wa Covid-19?

IMETIMIA miezi saba sasa tangu Tanzania kutangaza mgonjwa wa kwanza kupata maambukizi ya Covid – 19 akitokea nchini Ubelgiji, Machi 16, 2020. 

Hali hiyo ndio iliyopelekea serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutangaza shughuli zote za kijamii ikiwamo kufunga shule zote kuanzia za awali hadi vyuo vikuu pamoja na mikusanyiko mikubwa.

Kadhalika safari za ndani na nje ya nchi zisizo na ulazima zilizuiwa ili kupisha maambukizi hayo.

Katika kipindi hicho mpaka pale serikali iliporidhika na kuruhusu shughuli hizo kurejea, kulikuwa na kazi moja kuu ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo uliokuwa unaenea kwa kasi. Wizara ya afya, pamoja na kazi kubwa iliyofanya kuhakikisha kuwa jamii inapata kila inachostahili kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, pia ilikuwa na yake makubwa ya kufanya.

Katika wizara hiyo, sekta ya magonjwa ya kuambukiza, wakishirikiana na wagonjwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU), walifanya kazi ya ziada kuhakikisha kuwa hakuna mgonjwa anayepata maambukizi haya.

Agnes Mfulu (sio jina lake halisi), mkazi wa Tabata, anayeishi na VVU ni shuhuda wa juhudi hizo, waliovuka safari hii salama kwa msaada wa madaktari na manesi wa kutoka idara za magonjwa yanayoambukiza jijini Dar es Salaam. 

Akiongea kwa kujiamini, binti huyu anakiri kuwa hakuwa na wasiwasi katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 kwa kuwa madaktari na manesi waliwatengenezea mazingira mazuri ili kuhakikisha hawapati maambukizi ya ugonjwa huu. 

“Kando na kupewa dawa zinazoweza kudumu kwa muda mrefu pia tulifundishwa jinsi ya kuchukua tahadhari kama vile kuepuka msongamano wa watu, kuvaa barakoa na kuepuka kuzurura kama hakuna ulazima ili kuwa salama, “ anasema Agnes akiwa na uso uliojaa furaha.

UTABIRI WA WATU WANAOISHI NA VVU

Kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Kimataifa linalohudumia wanaoishi na virusi vya Ukimwi (UNAIDS) ya mwaka 2018, Tanzania yenye watu milioni 56.32, na wanaoishi na maambukizi ya VVU ni 1,600,000. 

Wanawake wameathiriwa vibaya na VVU katika nchi ya Tanzania: kati ya watu wazima, 880 000 (58.67%) walikuwa wanawake. Maambukizi mapya ya VVU kati ya wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24 walikuwa zaidi ya mara mbili ya wale wa kiume.  Matibabu ya VVU ilikuwa kubwa kati ya wanawake kuliko wanaume, hata hivyo, na 82% ya wanawake wazima wanaoishi na VVU kwenye matibabu, ikilinganishwa na 57% ya wanaume watu wazima.

 

CHANGAMOTO KWA BIASHARA

Pamoja na kupata huduma nzuri ya kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, wapo watu katika kundi hili walioacha kufanya biashara kutokana na hofu ya kupata maambukizi hivyo kuathirika kiuchumi.

Mboni Joseph (si jina lake halisi) anasema alilazimika kuacha biashara ya kuuza mamalishe kwa miezi mitatu kwa kuhofia kupata maambukizi ya Covid-19.

Mama huyu mwenye watoto wawili anasema kabla ya mlipuko wa Covid-19 alikuwa kiuza mamalishe eneo la Buguruni ambapo alikuwa akipata faida ya Sh.10,000 kwa siku iliyokuwa ikimsaidia kuhudumia wanawe.

“Niliishi maisha ya tabu sana kipindi kile sitosahau. Ilifikia kipindi tunakunywa uji tu asubuhi na watoto wangu, nashukuru sasa nimerudi kazini,” anasema.

Dk. Amina Mgunya, ni daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),  anayesema kuwa walifanya kazi kubwa kupambana maambukizi ya virusi vya Covid-19 katika idara hiyo.

Kwa mujibu ya daktari huyo bingwa, tatizo kubwa lilikuwa ni hofu ya kupata maambukizi. Baada ya kugundua tatizo hilo, yeye na timu yake walifanya kazi ya ziada kuwatoa hofu watu wanaoishi na VVU waliokuwa wanahudhuria kliniki katika hospitali hiyo. 

“Wagonjwa hawa walikuwa na hofu sana sio Tanzania tu hata nchi zingine, hata Afrika Kusini tumesikia wakitoka kwenye vyombo vya habari kuongelea hofu zao, lakini tuliwatoa hofu kwamba HIV/TB haikuwa miongoni mwa magonjwa ya hatari ya kupata Covid-19,” anasema Dk. Amina na kuongeza:

“Magonjwa yaliyoonekana kuwa na hatari kubwa ni kisukari, shinikizo la damu, moyo, homa ya mapafu kama COPDs, na magonjwa ya figo. Hatari kubwa ya ugonjwa mkali kutoka kwa Covid-19 pia ni kati ya wale wenye umri wa miaka 85 au zaidi.”

Pamoja na kuwatoa hofu hiyo, Dk. Amina anasema waliwasisistiza kunywa dawa zao kwa wakati ili kuweka kinga ya mwili sawa kwa sababu Covid-19 inashambulia sana mwili ambao kinga zake zipo chini.

HUDUMA MAJUMBANI Wazee na watoto wanaoishi na VVU pamoja na wenye magonjwa mengine kama kisukari katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Covid-19 ni miongoni mwa watu waliopokea huduma nyumbani.

Dk. Amina anasema waliruhusu wasaidizi wa matibabu kuwatembelea wagonjwa hao na kuwapelekea dawa pamoja na kuwajulia hali. Mgonjwa aliruhusiwa kwenda hospitali kama alipata tatizo lililohitaji huduma pamoja na kuwapa elimu ya kujikinga na maradhi hayo.

MSAADA VIFAA KINGAOfisa wa Utumishi wa Mtandao wa Vijana Wanaoishi na VVU (NYP+), Hassan Husein, anasema wamesambaza vifaa vya kujikinga kutokana na Covid-19 jijini Dar es Salaam. 

Kwa kupitia msaada wa fedha kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), wamesambaza vifaa kama vile ndoo ya kunawia mikono, barakoa na vitakasa mikono.

“Tulisambaza vifaa hivyo kwenye vituo tunavyofanya navyo kazi katika Wilaya ya Temeke, Ilala na Kinondoni ili kwenda kuongeza nguvu, na tunashukuru vimesaidia na hatukupata mgonjwa hata mmoja aliyepata maambukizi,” anasema Hassan.

Pamoja na changamoto hizo, Dk. Amina anashukuru juhudi zilizofanywa na wauguzi katika kitengo chao na mwitikio mzuri walioupata kutoka kwa wagonjwa. Hakuna mteja aliyepata maambukizi ya virusi vya Covid-19 kati ya wateja 3,689 wanaowahudumia.

Taarifa ya UNAIDS ya mwaka 2018 inonyesha kuwa vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vimepungua kwa 49%, kutoka 48,000 hadi 24,000, huku idadi ya maambukizi mapya pia ikipungua kutoka 83,000 hadi 72,000 katika kipindi hicho hicho.

Wakati akiongea na vyombo vya habari juu ya hali ya maambukizi ya VVU na Covid-19,  Mkurugenzi Mtendaji  wa UNAIDS , Winnie Byanyima, alisema kuwa kuna ushahidi kwamba idadi ya vifo vinavyohusiana na UKIMWI inaweza kuongezeka mara mbili  katika nchi za  Kusini mwa Jangwa la Sahara  kati ya mwaka 2020 hadi 2021 ikiwa huduma za VVU zitavurugika.

“Lakini sio hivyo tu, maambukizo  kutoka kwa mama kwenda kwa kwenda kwa mtoto yanaweza kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 katika nchi zingine barani Afrika. Na hiyo ni hatari. Kwa hivyo, ni muhimu sana kutoa ujumbe huko nje kwamba tunapaswa kuendelea na mapambano dhidi ya VVU na Covid-19.” 

Vile vile alitoa tahadhari kuwa watu wanaoishi na VVU wanapaswa wasisahaulike wakati mataifa yanazingatia namna ya kukabiliana na janga la virusi vya corona.

________________________________________

Habari hii imeungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti Mgogoro.     

Habari Kubwa