Walioangukia mkopo Ligi Kuu hawa hapa

12Aug 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Walioangukia mkopo Ligi Kuu hawa hapa

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kutimua vumbi Agosti 23, timu zote 20 zimekamilisha usajili na sasa kilichobaki ni kusubiri Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuwaidhinisha kwa ajili ya kutumika.

Mohamed Ibrahim akishangilia bao alilofunga kwenye moja kati ya mechi zake akiichezea Simba. Amepelekwa kwa mkopo Namungo ya Lindi.

Kuna wachezaji waliosajiliwa kutoka timu moja kwenda nyingine kwa kumalizika mikataba yao, wengine wakitoka nje ya nchi.

Hata hivyo kuna baadhi ya wachezaji wamejiunga kwenye timu kwa mkopo. Baadhi ya timu zimewatoa wachezaji hao kwa klabu nyingine kwa sababu wana wachezaji wengi, hivyo baadhi kukosa nafasi.

Wakati mwingine klabu huwatoa wachezaji kwa mkopo kwa sababu wachezaji hao wameshuka viwango, hivyo wanawapeleka kwa ajili ya kupandisha viwango vyao na huenda baadaye wakawarudisha.

Hawa ni baadhi ya wachezaji ambao wametolewa kwa mkopo kutoka klabu moja kwenda nyingine...

1. Ditram Nchimbi (Azam FC kwenda Polisi Tanzania)

Straika huyu wa zamani wa Klabu za Mbeya City, Majimaji na Njombe Mji, msimu ujao ataonekana akiwa amevaa jezi za timu mpya iliyopanda Ligi Kuu, Polisi Tanzania.

Msimu wa 2018/19 aliichezea Mwadui FC, lakini kwa sasa ameondoka kwenye klabu hiyo na kutua kwa maafande hao. Nchimbi ni mchezaji wa Azam FC aliyesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili.

Hata hivyo, baada ya kuona kuwa hawezi kupata namba kwenye kikosi chao msimu uliopita, Azam ilimpeleka kwa kopo Mwadui FC kwa mwaka mmoja na mwaka huu imeamua kumpeleka kwa mkopo JKT Tanzania.

2. Marcel Kaheza (Simba kwenda Polisi Tanzania)

Itakumbukwa kuwa mchezaji huyu alisajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Majimaji ya Songea.

Kabla ya kuwapo Majimaji alikuwa mchezaji wa kikosi cha pili cha Simba. Ilimrudisha tena kwenye himaya yake, lakini baada ya kuona ina wachezaji wengi kiasi cha baadhi kukosa namba, ikampeleka AFC Leopards ya Kenya kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Tayari amemaliza mkopo wa mwaka mmoja na kurejea nchini. Mwenyewe akadai kuwa hataki tena kurejea Kenya na anataka kama ikiwezekana atafutiwe timu hapa hapa nchini.

Klabu yake ya Simba imeamua kumpeleka kwa mkopo wa mwaka mmoja kwa mara nyingine kwenye klabu ya Polisi Tanzania ambayo imeonekana kujizatiti baada ya kufanikiwa kupanda Ligi Kuu.

 

3. Sixtus Sabilo (KMC kwenda Polisi Tanzania)

Ni mchezaji wa zamani wa Stand United ambaye baadaye alisajiliwa na Klabu ya KMC iliyopanda daraja msimu uliopita.

Hata hivyo, klabu ya KMC imeamua kumtoa kwa mkopo kumpeleka Polisi Tanzania. Sabilo amebakisha miezi sita tu amalize mkataba wake na KMC, kabla ya kuwa huru.

Ina maana kwenye kipindi cha dirisha dogo msimu wa 2019/20 atakuwa huru kuchagua timu anayoitaka, kama kuendelea kwa Polisi Tanzania itabidi waingie mkataba kwani wa mkopo na KMC utakuwa umemalizika, au kwenda timu nyingine itakayokuwa inamhitaji.

 

4. Mohamed Ibrahim (Simba kwenda Namungo FC)

Misimu miwili iliyopita akiwa na Simba alikuwa moto wa kuotea mbali. Mohamed Ibrahim ni mmoja wa wachezaji wenye kipaji cha hali ya juu. Alikuwa ndiye tegemeo kubwa kwenye kikosi cha Simba mara alipojiunga akitokea Mtibwa Sugar.

Kwa siku za karibuni kiwango chake kimekuwa hakiridhishi na hata kukosa kabisa namba kwenye kikosi hata cha wakaa benchi.

Kutokana na usajili mkubwa uliofanywa msimu huu, Klabu ya Simba imelazimika kumtoa na kumpeleka kwa mkopo kwenye Namungo FC iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.

5. Mohamed Rashid (Simba kwenda JKT Tanzania)

Ni straika wa Simba ambaye aliichezea timu hiyo kwenye michuano ya Kagame Cup tu msimu uliopita. Ni baada ya kusajiliwa kutoka Prisons ya Mbeya. Baada ya hapo iliamua kumtoa kwa mkopo kabla hata Ligi Kuu msimu wa 2018/19 haijaanza na kumpeleka KMC ambako amecheza kwa msimu mmoja.

Simba imemtoa tena kwa mkopo kwenda JKT Tanzania kumalizia mkataba wake wa mwaka mmoja uliobaki, hivyo kuanzia Agosti 23 ataanza kuonekana akiwa na timu yake hiyo mpya.

6. Paul Bukaba (Simba kwenda Namungo FC)

Ni beki mwenye mwili mkubwa anayetumia nguvu nyingi katika kudhibiti mastraika wakorofi. Amekuwa na Simba kwa kipindi cha misimu miwili. Hata hivyo, hakuwa vizuri sana msimu uliopita na alifanya makosa mengi ambayo kwa kiasi fulani yaliigharimu klabu yake ya Simba kwenye mechi kadhaa hasa za kimataifa.

Kutokana na kusajiliwa kwa mabeki wengi kwa msimu ujao wa ligi na mechi za kimataifa, Simba imeamua kumpeleka kwenye klabu ya Namungo kwa mkopo.