WANACHOFUKUA WANAMAZINGIRA KWENYE MAKINIKIA

30Jun 2017
Flora Wingia
Dar es salaam
Nipashe
WANACHOFUKUA WANAMAZINGIRA KWENYE MAKINIKIA
  • Mwanasheria Dk. Nshala: Mikataba tunayotia saini nje ‘tuchomekewa kibano’ cha kisheria
  • *Adokeza maslahi binafsi nayo ‘jipu’; Katiba ya nchi, maazimio ya UN yanakiukwa waziwazi
  • *…mikataba ambayo tumeisaini wote inasema migogoro hii iamuliwe na mahakama au mabaraza ya usuluhishi ya huko nje.

HII ni sehemu ya pili ya mwendelezo wa makala kuhusu ripoti mbili za uchunguzi, kutokana na uamuzi wa kusitishwa usafirishaji wa makontena 277, mchanga wa makinikia ya dhahabu uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli mwezi Mei, mwaka huu-

kupitia tume iliyoundwa kuchunguza uhalisia wa yaliyomo kwenye mchanga huo.

Juni 16, 2017 katika kipindi cha Kipimajoto kinachorushwa kupitia kituo cha ITV Super Brand Afrika Mashariki, Capital Radio na Radio One Sterio kila Ijumaa, swali liliuza: Matokeo Ripoti ya Pili ya Uchunguzi Mchanga, nini fundisho kwa Watanzania? Mtangazaji wa ITV Jacquline Selemu aliwakutanisha Dk. Rugemeleza Nshala, Mkurugenzi Mtendaji, timu ya wataalamu masuala ya sheria (LEAT), Bravious Kahyoza ambaye ni mchumi na Sabato Nyamsenda, mchambuzi masuala ya Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Jacquline: Hii si tume ya kwanza katika sekta hii ya madini. Na hizi tume za mheshimiwa Rais siyo za kwanza pia. Unadhani, kwanini tume hizi zimekuwa na majibu ama zimefuatiliwa sana, zimeibua hisia za Watanzania walio wengi ikilinganishwa na tume zingine zilizopita?

Sabato: Nadhani ya kwanza ni kwamba, Tume zilizoundwa huko nyuma, kwa mfano, tukiangalia wakati wa Rais Jakaya Kikwete, kuna kamati mbili ambazo ziliundwa.

Ya mwisho ambayo ilikuja na marekebisho ya sheria kwamba; ya kwanza tunapokuwa na msisitizo kujaribu kubadili aina ya uchumi wetu, tukiangalia katika utawala wa awamu ya nne kwa mfano, ulikuwa utawala ambao uliheshimu hizi sekta. Pia sera zilizokuwa zinategemea uwekezaji kutoka nje.

MWELEKEO UCHUMI WA KUJITEGEMEA:
Kwa hiyo, kwa sasa hivi hapa nchini awamu hii ya tano, kuna mwelekeo na hasa kwa kiongozi wa juu Rais mwenyewe, wa kujenga uchumi unaojitegemea, uchumi wa kitaifa. Ndio maana, anaongelea hiyo dhana kwamba hatuwezi kuendelea kusafirisha mali ghafi. Lazima tuwe na malighafi ambazo tunazalisha zitachakatwa humu humu nchini. Kuna mwelekeo wa kusema kwamba pato linalopatikana nchini libadili maisha ya kila mwananchi.

Kwa hiyo, nasema huu mwelekeo ulipokelewa vyema na watu ambao kwa muda mrefu walikuwa wakilia juu ya suala hilo. Na kamati hizi zimekuwa maarufu kwa sababu kwa sehemu kubwa, zimeibua mambo mengine ambayo hayakuibuliwa na zile kamati zingine. Hizo kamati hazikwenda mbali sana, Kamati ya Jaji mstaafu Bomani jambo kubwa ambalo ilizungumza ilikuwa ni serikali ianze kumiliki hisa katika madini.

Lakini haikwenda mbali katika kuonyesha aina ya uporaji na kiasi kilichokuwapo kikubwa katika mikataba. Tume hii ya sasa hivi imeonyesha kwenda mbali katika hili, ni kelele za wananchi wetu wamekuwa wakizipigia muda mrefu, kwa hiyo ikathibitika.

Kwa hiyo, uungwaji mkono umekuwa katika sehemu mbili; Ya kwanza aina ya mambo yaliyoibuliwa na tume, ya pili aina ya dira ambayo inajaribu kutolewa na kiongozi wa nchi.

SHERIA MBOVU ZIMETUFIKISHA HAPA:

Jacquline: Dk. Nshala, miongoni mwa mambo ambayo yanatazamwa katika hizi ripoti, ni kwamba yanayoonekana yalisababisha haya yote, ni pamoja na kuwapo sheria ambazo ama kwa namna moja au nyingine, zimekuwa zikichangia mambo haya kutokea. Ninyi ni wanasheria. Mlikuwapo tumeanza kuchimba tokea mwaka 1998 mpaka leo mwaka 2017.

Leo mkiinuka kama wanasheria mkiungana na Watanzania wengine ambao hawakuwa na nafasi ya kuzijua hizi sheria, kwamba pengine siyo nzuri, hata Mheshimiwa Rais alishangaa ni taifa la namna gani lina wanasheria, lina wasomi, nini nafasi yenu katika kuhakikisha kwamba taifa letu haliingii katika matatizo?

Dk.Nshala: Ni kweli kwamba wanasheria walikuwapo. Wanasheria wengine walishiriki katika kuandika sheria hizi, walipewa kandarasi za kushirikiana na hiyo kampuni ya nje ya Clifford Chance. Lakini kwa wanasheria, tulipinga sisi LEAT tulipinga tulionesha kwamba jinsi wananchi kule Bulyanhulu walivyoondolewa.

Tukazungumzia mambo ya Nzega, tukaanza kuzungumzia hata masuala ya Marerani na sehemu mbalimbali. Kwa hiyo, sisi LEAT tulikuwa mstari wa mbele kuonyesha kwamba, kuna tatizo kubwa katika sheria ya madini mwaka 1998.

LEAT ILIPUUZWA MAUAJI BULYANHULU
Tukaenda mbele hata wakati ule Benki ya Dunia mwaka 2001 na 2003, walifanya mapitio mazima ya ufadhili wa Benki ya Dunia katika sekta ya madini. Rais wa Benki ya Dunia wakati ule alikuwa James Wolfensohn. Sisi tulipeleka msafara wetu na watu wa Bulyanhulu kwenda Msumbiji kutoa ushahidi. Na hii ilitokana na uzoefu wetu, baada ya kupeleka kesi katika kusuluhisha migogoro ya kampuni ambazo zinafadhiliwa na Nigar na INC tukaonyesha kwamba wale watu wa Bulyanhulu walionewa.

Tukapeleka malalamiko yetu kule tukazuiwa tusipeleke ushahidi kwamba watu wanafukiwa kule, lakini ripoti ya uamuzi ikasema kuwa LEAT imeshindwa kutoa ushahidi kwamba watu wameuawa. Hii ilitufanya wengine tukajua kwamba hapa tunacheza na watu ambao ni waongo sana.

Nia yao ya dhati wakati unapokaa nao, ni watu ambao wanaokugeuza wewe kwamba ni mwendawazimu. Sasa tulilalamika na kutokana na zile kelele ambazo tulipiga, ule mwaka wa 2001 hadi 2006/7 Benki ya Dunia wao walipoona kwamba katika Afrika nzima kumekuwa na kelele za aina hii, wenzetu wa Zambia waliandika wapata ushahidi mzuri sana kuonyesha jinsi gani madini ya shaba yalivyobinafsishwa.

Kuna mgodi wa Kishansha uliuzwa kwa dola milioni 50 (Sh. bilioni 110) mgodi mzima na Zambia uliambiwa kwamba kama haitabinafsisha madini yake yote, ile Zambia Consolidated Copper Mining isipoondolewa katika serikali ya Zambia, watapewa kampuni za nje, na Anglo-American.

Kwa bahati mbaya, ile miaka ya 2001, bei ya shaba ilishuka chini zaodi. Na wale Anglo-American wakajitoa. Benki ya dunia ikakimbia kutafuta watu wengine ndio zile kampuni za India zilipewa.

Ghafla mwaka 2004, bei ya shaba ilikatika kutoka dola za Marekani 2,000 (Sh.milioni 4.4) kwa tani moja ya mraba kufikia dola 7,400 (Sh. miliioni 16.28) .

Ghafla, migodi ya shaba Zambia ilianza kupata faida kubwa. Sasa unakuta Zambia yenyewe ilikuwa haipati kitu. Zambia mwaka 1992 ilipata dola milioni 400 (Sh. biliioni 880), mwaka 2004 kiwango kile kile cha shaba ambacho kinazalishwa walipata dola laki mbili (Sh. milioni 440)

Jacquline: Wewe ni mwanasheria, nataka kufahamu kutoka kwako. Unadhani ni kwa kiasi gani, sheria za kimataifa katika sekta hii ya madini zimeathiri kile ambacho tunakitizama leo kwa Tanzania?

Dk.Nshala: Sheria za kimataifa ni kwamba inategemea unazielewaje. Sheria za kimataifa zipo ambazo zinasema kwamba, sisi kama nchi zetu tuna umiliki wa milele wa rasilmali zetu; Lipo Azimio Namba 1803 la Mwaka 1962 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Azimio Namba 3281 la 1974 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Haki na Majukumu ya Kiuchumi ya Mataifa, ambayo ni miongoni mwa sheria za kitamaduni za kimataifa tunazopaswa kuziheshimu.

Tunapokwenda kuandika mikataba ya madini, mfano Tanzania imejadiliana na Marekani au Uingereza, badala ya kulinda msingi wa maazimio hayo mawili, tunaandika sheria ambazo zinakinzana nayo. Mwaka 1938, Mexico ilitaifisha mali za kampuni moja ya Marekani, ikaitaka Marekani ilipe fidia na ile faida.
Wakati huo Mexico ilikuwa inadai dola milioni 450 (Sh. bilioni 990). Marekani ikasema hatukatai, dola inayo haki ya kuchukua mali za watu, lakini ilipe fidia kamilifu ya wakati na haraka. Wakasema, hiyo ni sheria ya kimataifa.

Mexico ikawaambia hatujawahi kusikia sheria inayosema kamilifu na ya wakati, ilimaanisha ilipwe fidia na faida ile ambayo ilikuwa waipate kwa miaka yote ya kufanya kazi pale. Mexico walikataa. Na hiyo kampuni ya Marekani ilikuwa inadai dola 450 (Sh. biliioni 990)

Majadiliano yaliendelea mpaka mwaka 1942. Marekani iliipatia Mexico jumla dola milioni 25 kuipatia kampuni ya Standard Voice. Hii ndiyo iliwasaidia watu wa Venezuela.

Venezuela baada ya kusikia Mexico, wamefanikiwa kupambana na kampuni hizo za Marekani na wao wakafanya mabadiliko kwenye sheria yao ya mafuta. Sheria ya Hydro-carbon ya mwaka 1945 wakadai kupitia sheria hiyo ya kimataifa wakidai fidia. Wakati huo waziri wao wa Fedha akiitwa Duani Pablo Alphonso. Huyu ndiye aliyeshawishi nchi za nne za Kiarabu kuungana na Venezuela kuanzisha OPEC mwaka 1960.

Sasa baada ya Venezuela kufanikiwa, Saudi Arabia nao wakaamka mwaka 1949 wakapitisha sheria yao. Mwaka 1933, Mfalme wa Saudi Arabia, alikuwa amegawa asilimia 66 Saudi Arabia. Aliigawia kampuni ya Kimarekani ikiitwa Racco. Watu wa Saudi Arabia, wakaona haiwezekani.

Saudi Arabia ilikuwa tajiri sana, kwa mara ya kwanza serikali ya Saudi Arabia kupata mafuta mengi mwaka 1951, walipata dola za Kimarekani milioni 111 (Sh.bilioni 244. 2).

Sasa haya na mengine ndiyo yanayohusu sheria za kimataifa. Ndio maana nasema, nchi zetu zinapaswa kusimamia sheria za kimataifa, ili kuweza kulinda rasilimali zetu. Tuwe na hali katika kuchimba rasilimali hizo.

Pili, kunapotokea migogoro pengine kukosana na mwekezaji, au mchimbaji, iamuliwe na mahakama zetu. Bahati mbaya hii mikataba ambayo tumetia saini wote, inasema migogoro hii iamuliwe na mahakama au mabaraza ya usuluhishi ya huko nje.

Sasa hii ni kinyume cha katiba yetu kwa sababu Ibara ya 107 (A), inasema kwamba mahakama zetu, mahakama kuu ndizo zinazopaswa kutatua migogoro yetu inayotokea Tanzania. Sasa kama unaheshimu katiba yako, huwezi kukubali usaini mkataba ambao unasema kuwa migogoro ambayo inatokea Tanzania, iamuliwe na watu ambao siyo Watanzania au siyo chombo cha Kitanzania.

Sisi kipekee tunakubali kwamba kuna vyombo vya kikanda kama Mahakama ya Afrika au Mahakama ya Afrika Mashariki, ambako tungesema kwamba, kule tuko tayari kwenda, kwa sababu bado inaendana na katiba za nchi zetu, kwamba baada ya mahakama zetu mwisho wa siku tutakwenda kwenye rufani maalum kwa ajli ya rufani, kwa hiyo hatujakiuka msingi mzima wa katiba ya nchi yetu.

Jacquline: Haya mambo hayajaanza leo wala jana, na hayo yote unayozungumza ni historia tayari yalishatokea tumeshayaona. Napata wasiwasi kwamba nini nafasi ya wanasheria wa Tanzania katika kuhakikisha kwamba haya ambayo unayazungumza leo, ambayo yameliweka taifa sehemu ngumu katika kupoteza mapato yake.

Pengine kuna mikataba ilishasainiwa na kuna suala la usuluhishi kwa mgogoro kati ya mgodi fulani na mahakama za ndani zilipaswa kuishughulikia, lakini mikataba yetu inajielekeza nje ya nchi. Wanasheria mnajua kwamba inakiuka sheria za nchi, nini nafasi yenu katika kusimamia hili?

Dk. Nshala:Inategemea unayemwambia yuko tayari kusikia. Au bahati mbaya wakati mwingine unapozungumzia rasilimali za umma unakuwa ni adui wa watu fulani.

Inategemea wako tayari kusikia au unagusa maslahi yao ambayo pengine ni kinyume na maslahi ya nchi. Sasa sisi tunachopigania ni kwamba bahati nzuri hii kamati ya pili ilisema kwamba hata hii migogoro isuluhishwe hapa ndani.

Nadhani hili ni jambo zuri, lakini mimi ningependa kwamba katika masuala kama haya ya madini, rasilimali zinazokwisha au hata kama anavyosema Sabato kwamba ni nini majaliwa au mwongozo wa uchumi wa nchi yetu.

Sasa katika sekta ya madini lazima tukae chini kama nchi na kuweka mwongozo ambao unaweza kuheshimika. Kwa mfano, wenzetu kama Norway tunayoiona leo mwaka 1900 ilikuwa nchi ya kwanza kwa umaskini Ulaya. Hata yule Mswidishi aliyeanzisha nishani ya Nobel, baada ya kupata uhuru Norway na kuona watu wa Norway wanaanza kuzaliana kama panya ambao ni walevi kila siku.

Lakini akasema, nchi kama hii itakuwa na zawadi gani ya kutoa duniani ndipo akaamua kuikabidhi ile nishani ya amani akalipatia Bunge la Norway. Hizi nishani zingine zikawa zinatolewa na Baraza la Sayansi la Sweden.

Sasa ile nchi ilipogundua mafuta mwaka 1969 , wakasema tusifanye maamuzi ya kukurupuka , tukae chini tuweke miongozo ambayo itaweza kuongoza sekta hii. Mwaka a 1972/73, wakaja na sera za kuendesha sekta ya mafuta ambazo uje mtu wa chama hiki au chama kile ushinde uchaguzi bado utazitii. Ndio maana ule mfuko wa akiba wa maendeleo ya mafuta una dola milioni 850. Kumbuka Norway ina watu milioni nne tu.

Sasa bado ukichimba mafuta yale yote yakaisha, ni kwamba vizazi na vizazi vitaendelea kula ile rasilimali. Ni kwamba watu wamekaa chini, wametafakari wametoa mwongozo kwamba hii sekta ilindwe. Kwa hiyo haitegemei ni nani aliyeko madarakani bali kila mtu aitii.

Kwa hiyo sisi kama Tanzania ni lazima tukubali kukaa chini tutafakari na kuweka mwongozo wa namna ya kuendesha rasilimali zetu zinazokwisha na hata zile zisizokwisha kama wanyamapori, misitu, maji au maziwa na mwisho wa siku ni namna gani tunaweza kulitoa taifa letu hapa lilipo na kulipeleka kule ambako linatakiwa liwepo.

Kwa sababu nchi yetu katika hali ya kawaida, hata kuwa hapa tulipo tulitakiwa tuwe mbele sana ili tukubali kwamba miaka yote 50 na zaidi bado sisi ni ombaomba wakati wenzetu waliokuwa ombaomba katika mika ile ya 1960, siyo ombaomba tena ndio wanaofadhili watu wengine. Kwa hiyo, tuna mchango mchango ambao tuko tayari kuutoa na kama unasikika tuko tayari kutoa mawazo.

Bahati nzuri, ikiwa mtu umekaa na hao watu, hao wazungu tunawafahamu tabia zao, umesoma nao, unawafahamu udhaifu wao au unaona kwenye mitandao yako au unaweza kuzungumza nao, hakuna shida. Lakini kama tutaendelea na mambo yale yale kwamba watu wachache wataweza kuamua nchi yetu itakwendaje bila kuwa na mwongozo wa kukubaliana kitaifa, mwisho wa siku tutakuwa tunarudia pale pale.

*Itaendelea Ijumaa ijayo.

Habari Kubwa