Wanakijiji Masawi warejesha uoto asili kutokana na hifadhi ya msitu

04May 2017
Beatrice Philemon
Kondoa
Nipashe
Wanakijiji Masawi warejesha uoto asili kutokana na hifadhi ya msitu

KIJIJI cha Masawi kipo katika Kata ya Salanga, Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma. Kilianzishwa mwaka 1976 na mpaka sasa kina jumla ya wakazi 2,500 ambapo kati yao wanaume wako 1,200 na wanawake 1,300.

Kabla ya wanakijiji na viongozi wa kijiji hikikupata mafunzo juu ya uhifadhi wa misitu ya jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na utawala bora katika Usimamizi Shirikishi wa Misitu miaka mitano iliyopita, hali ya misitu katika kijiji hiki ilikuwa mbaya sana kutokana na uharibifu wa misitu.

Asilimia 80 ya uharibifu wa misitu ilitokana na ukataji miti kwa ajili ya shughuli za kilimo, uchomaji mkaa na tofali, kuni na mbao.

Uharibifu huuulioendeshwa hasa nawanavijiji kutoka Kanda ya Mashariki, katika Kijiji cha Kandaga, Kata ya Hitololo Wilaya ya Kondoa.

Akizungumza na Nipashe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Masawi, Issa Swalehe Gwandi (67) anasemamafunzo ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USM)kupitia Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa kutokana na Ukataji na Uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) na Mabadiliko ya Tabianchi,yameleta mabadiliko chanya katika kutunza vizuri misitu ya kijiji hicho.

“Baada ya kupata mafunzo kama viongozi wa vijiji, tuliitisha vikao na wanakijiji tukawapa elimu ya usimamizi shirikishi wa misitu na mabadiliko ya tabianchi jinsi yanavyosababisha ukame kutokana na ukataji wa misitu,” anasema.

Gwandi anasema, baada ya hapo waliitisha tena vikao vingine nakuchagua Kamati ya Mazingira ya Kijiji yenye watu sita pamoja na askari wa kufanya doria kwenye Msitu wa Hifadhi ya Salanga ili kusaidia kuzuia uharibifu wa msitu.

“Kwa mfano hivi sasa hali ya uingizwaji wa mifugo ndani ya msitu, ukataji miti kwa ajili ya kuni, mkaa, kuchoma tofali na mbao kumepungua kwa kiasi kikubwa,” anasema na kuongeza:

“Hali ya uoto wa asili katika msitu wetu imeanza kurudi katika hali yake na uyoga wa aina mbalimbali, mweupe, mwekundu na njano umeanza kuota.”
Anafafanua kuwa kwa hivi sasa wanakijiji wanakwenda kuokota kuni kwa mikono bila kutumia shoka au panga na hairuhusiwi kuingia na shoka wala panga kwenye msitu.

“Lakini ni lazima pia upate kibali kutoka kwa Afisa Misitu aliyepo kwenye kijiji chetu na asipokuwepo, kibali lazima kitoke kamati ya mazingira au serikali ya kijiji,”anasema.

UPANDAJI WA MITI

Mbali namafunzo ya uhifadhi wa misitu,Gwande anasema kwamba kupitia mafunzo hayo wameweza kupanda miti ya aina mbalimbali katika sehemu zilizoharibika kutokana na ukataji miti.

Anasema wamepanda miti katika shule ya sekondari Masawi, shule ya msingi Masawi, sehemu zenye mabonde, misikitini, Vituo vya afya na kuotesha miche kwa kutumia mfuko wa ECOPRC.

“Tunawashukuru sana Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa kutuwezesha kupata mafunzo ambayo yameweza kuletea mabadiliko chanya katika kijiji chetu kwenye eneo la uhifadhi na usimamizi wa msitu,” anasema.

Mafunzo hayo yalitolewa na MJUMITA kwa msaada wa Serikali ya Kifalme ya Norway, kupitia Mradi wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa Kutokana na Ukataji na Uharibifu wa Misitu (MKUHUMI) na Mabadiliko ya Tabianchi.

MKAKATI KUKABILIANA NA MABADILIKO TABIANCHI

Akielezea mkakati wao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Gwande anasema wamejiandaa kwa kutunza misitu zaidi na maporomoko ya maji pia kwa kuanzisha mradi wa ufugaji nyuki katika Hifadhi ya Msitu wa Salanga.

Mradi wa ufugaji nyuki utasaidia kulinda msitu kwa sababu mara kwa mara watakuwa wanatembelea maeneo yaliyotundikwa mizinga ya ufugaji nyuki.

KATIBU WA KIKUNDI
Naye Katibu wa Kikundi cha Pambana na Mabadiliko ya Tabianchi (PAMATA)Mohamed Khatibu anasema kuwa,usimamizi shirikishi wa misitu umewasaidia kwa asilimia 70 kuondoa uharibifu wa misitu.

Aidha, anasema vyanzo vya maji vilivyokuwa vimeharibiwa na mifugo, hivi sasa vipo salama na hakuna mwananchi anayeingiza mifugo kwenye msitu hali ambayo imesababisha mvua zianzekunyesha kwa wingi.

“Kijiji chetu kina vyanzo vingi vya maji, lakini vingi viliharibiwa na wanavijiji wanaotokea vijiji vilivyopo pembezoni mwa Hifadhi ya Msitu wa Salanga, wenye hekta za mraba 8,333,anasema.

Khatibu anasema, chemchem kubwa ya Kichemka iliyokuwa inatumiwa na wanakijiji wa Masawi ilikauka kabisa na kubaki chemchem ndogo ya Mawe ya Fisi na Chemchem ya Kwa Mala.

Anaendelea kufafanua kwamba, maeneo mengine yaliyokuwa yameharibika sana kwa uharibifu wa misitu ni mpakani mwa kijiji cha Saranka karibu na Msitu wa Hifadhi ya Salanga.

Anasema mafunzo yaliyoandaliwa naMJUMITA yamewawezesha kuboresha vyanzo vya maji vilivyopo na maji yameanza kuongezeka na kupatikana kwa urahisi kuliko hapo awali.

“Mwanzoni chemchem zote zilikuwa zimekauka na kuwa na maji kidogo, lakini sasa hivi maji yameongezeka na pia tumeboresha maeneo yake hakuna tena mifugo kuingia katika maeneo hayo na hali ya uoto wa asili iliyokuwa imeharibika imerudi upya,” anasema.

Anaongeza kwamba kwa sasa hali ya misitu imeboreka, ukataji wa miti umepungua, wanaendelea kupata mvua, hali ya mashamba imeboreka kuliko maeneo mengine tofauti na hapo awali walipokuwa wanapata mvua chache na zisizotabirika.

Khatibu anasema uyoga sasa unapatikana kwa wingi na kwa aina mbalimbali kama uyoga wa njano, mweupe na mwekundu kwa ajili ya matumizi ya wanakijiji.

WAWEKA UTARATIBU

Akielezea mkakati waliouweka kuendeleza sekta ya misitu na kupunguza uharibifu wa rasilimali hiyo, Khatibu anasema wamejiwekea utaratibu mzuri wa kuokota kuni siku za Jumamosi na Jumapili tu.

Anasema awali kila mwanakijiji alikuwa anaenda mwenyewe kukata kuni jinsi anavyotaka, lakini sasa hivi baada ya utaratibu huu, mwanakijiji haruhusiwi kuingia kwenye msitu akiwa na shoka wala panga kukata miti, matawi wala na kuni.

“Mtu akitaka kukata kuni au mti lazima apate kibali kutoka kwenye uongozi wa kijiji au kamati iliyoundwa kwa ajili ya usimamizi wa msitu na anatakiwa kuokota matawi yaliyokauka na kudondoka tu,” anasema.

CHANGAMOTO
Akielezea changamoto zinazowakabili katika usimamizi wa misitu, Khatibu anasema kuwa ni siasa kuingilia shughuli za uhifadhi wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Kwa mfano mwaka 2015, wanasiasa walikuwa wanasimama jukwaani na kuwaambia wananchi, mkinichagua mimi, nitaruhusu matumizi ya misitu kama kuchunga mifugo hasa ng’ombe na hili jambo lilidhohofisha shughuli za Kamati za Mazingira na Jumuia ya Hifadhi ya Mazingira, Tarafa ya Bereko na Kolo,” anasema.

Aidha, anasema katika harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika kijiji cha Masawi, wamejipanga kutunza misitu yao, kuboresha sehemu ambazo zina mianya kwa kupanda miti na kuanzisha vitalu kwa kuotesha miche ya miti ya aina mbalimbali.

“Mpaka sasa tumeanzisha kitalu cha miche chenye miche 2,500 ya miti ya aina mbalimbali, na tayari tumeanza kuipanda katika baadhi ya maeneo yaliyoharibiwa kutokana na ukataji miti, pia tunafanya biashara ya kuuza miche kwavijiji jirani kwa bei ya shilingi 500 kila mche,” anasema.

Mbegu za miche wamepata kwenye mashamba yao na elimu ya uoteshaji na upandaji wamepata kutoka kwa wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Idara ya Maliasili.

MWEKA HAZINA ALONGA

Naye Mwekahazina wa Jumuiya ya Hifadhi ya Mazingira, Tarafa ya Bereko na Kolo, Hawa Abdi Ndui, anasisitiza kuwa changamoto mbaya zaidi inayowakabili hadi kufikia misitu kuharibika ni ile ya wanasiasa kuingilia mambo ya uhifadhi wa misitu.

“Kwa mfano mwaka 2016, walipokuwa wanaomba kura kwa wananchi wao, walitegemea misitu kuomba kura kitu ambacho ni kinyume cha sheria,” anasema na kuongeza:

“Walikuwa wanawaambia wananchi kuwa wakiwapa kura watawaruhusu kuingia kwenye misitu kuchoma mkaa, mbao, kuendesha shughuli za kilimo na mambo mengine.”

Aidha, waliwaambia wananchi kuwa watafukuza kamati ya mazingira pamoja kitu ambacho kinarudisha juhudi za uhifadhi na usimamizi wa misitu.

Habari Kubwa