Wananchi acheni kutumiwa kisiasa

24Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Wananchi acheni kutumiwa kisiasa

NI ukweli kwamba taifa lolote duniani lenye maendeleo linachagizwa zaidi na msukumo wa uwepo wa amani na utulivu pamoja na utii wa sheria.

IGP Sirro akizungumza na wananchi pamoja na polisi katika mikutano mbalimbali wakati wa ziara yake. PICHA:JESHI LA POLISI.

Amani ndiyo maendeleo, ni maisha hivyo chochote kinachofanywa kwenye jamii kinatokana na amani iliyopo kwenye eneo husika kwa mantiki kuwa watu wanapaswa kuitunza ili kufikia malengo wanayoyatarajia.

Mapema mwezi huu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, anakutana na kuzungumza na baadhi ya wananchi wa eneo la Dareda mjini Babati mkoani Manyara, ambapo aliwataka kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo pia kuacha kutumiwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa ili kuepuka kujiingiza kwenye vurugu zitakazopelekea uvunjifu wa amani.

Ziara ya IGP Sirro, anayoifanya mkoani Manyara ni miongoni mwa kazi zake za kawaida zenye kulenga kufanya ukaguzi, kuzungumza na maofisa na askari wa ngazi mbalimbali, kujua utendaji wao na utekelezaji wao wa majukumu ya kazi za kila siku za kipolisi na namna wanavyotoa huduma kwa wateja.

Hatua ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Sirro, kuzungumza na wananchi kila anapokuwa kwenye ziara zake za kikazi kinazidi kufungua ukurasa mwingine mpya zaidi hususan suala la ukaribu wa jeshi hilo na wananchi wake wa ngazi ya chini katika mrengo wa kuendelea kuhamasishana juu ya kuitunza amani ya nchi yetu.

Katika ziara hiyo, IGP Sirro anazungumza na wananchi na kuwataka wazazi na walezi kuendelea kuimarisha malezi ya familia zao kwa kuwajenga watoto kwenye maadili yanayofaa jambo ambalo litasaidia kuwaepusha kujiingiza kwenye matendo ya uhalifu na kuwa kero kwa wananchi.

'Niwatake wananchi wenzangu tuzingatie malezi ya watoto wetu kwani ni aibu kuwa na mtoto mwizi, na ni aibu pia kuwa na mtoto anayefanya vitendo vya ukatili’ anasema IGP Sirro.

Anaiambia jamii kuwa inawajibu wa kutunza amani iliyopo sambamba na kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama huku akiwahamasisha watumiaji wa miundombinu ya barabara pamoja na vyombo vya moto kuendelea kutii na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni IGP Sirro alifanya ziara ya ukaguzi katika jumla ya mikoa mitatu ikiwemo Manyara, Arusha na Kilimanjaro ambapo katika mikoa hiyo anazungumza na wananchi pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari na kutolea ufafanuzi masuala kadhaa kuhusiana na hali ya amani ya nchi yetu.

Ofisi ya Uhusiano, Makao Makuu ya Polisi- Dodoma

Habari Kubwa