Wananchi jiepusheni na tabia ya kujichukulia sheria mkononi

25Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wananchi jiepusheni na tabia ya kujichukulia sheria mkononi

DUNIA kwa hivi sasa inakumbwa na tatizo la jamii kujichukulia sheria mkononi.

Kwamba umezuka mtindo wa watu kuchukua hatua ya kumwadhibu au kumshambulia mtu ama jamii kuchukua hatua juu ya jambo fulani bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Tanzania ikiwa ni sehemu ya dunia imeshuhudia matukio kama ya wananchi kumshambulia mtu hadi kumuua au kumwacha akiwa na kilema cha kudumu kwa kisingizio kuwa ni mwizi au ametenda uhalifu fulani.

Aidha, matukio mengine ni ya mauaji yanayotendwa na baadhi ya watu kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi au ulevi.

Matukio ya aina hii ndiyo yanatokea mara kwa mara na yanachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matukio ya mauaji hapa nchini.

Matukio mengine ya kujichukulia sheria mkononi ni yale yanayotendwa kutokana na imani za kishirikina ambapo wana ndugu, ukoo, majirani, wanakijiji au watu wengine tu mtaani wanamtuhumu mtu kuwa ni mchawi na mara nyingi watuhumiwa wanakuwa ni wale wazee.

Matokeo yake wanawavizia na kuwaua au kuwashambulia kwa silaha mbalimbali hadi kuwaua.

Vilevile, migogoro ya wakulima na wafugaji nayo imekuwa ikisababisha wananchi kujihusisha na vitendo hivyo vya kujichukulia sheria mkononi, kwani badala ya migogoro hiyo kusuluhishwa kwa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa au katika katika vikao vya kusuluhisha, wengine wanakiuka na kujichukulia sheria mkononi kwa kutekeleza mauaji au kusababisha majeraha na vilema kwa wengine.

Wakati akihojiwa na mwandishi wa makala haya, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Kamishna Msaidizi Mwadamizi wa Polisi SACP David Misime amesema kuwa, vitendo vya kujichukulia sheria mkononi ni ukiukwaji wa sheria za nchi na kwa wale wanaobainika hukamatwa na wanapopatikana na hatia mahakamani sheria inaelekeza kuwa adhabu yake ni kifo.

Vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vimekatazwa na sheria mama ambayo ni Katiba ya nchi na sheria nyingine pamoja na vitabu vya dini navyo vimekataza vitendo hivyo.

Akitoa wito kwa wananchi juu ya vitendo vya kujichukulia sheria mkononi, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SACP Misime, alieleza kuwa ili kuondokana na matukio haya ambayo yanaleta madhara makubwa kwa jamii na kwa familia kubaki yatima, kujenga chuki na uhasama na baadhi ya wanajamii kubaki vilema ni vyema wadau wote na jamii kwa ujumla kukemea vikali vitendo hivyo pamoja na kusimamia malezi na maadili kuanzia ngazi ya familia kwani ngazi hiyo ikisimamiwa vizuri matukio kama haya yatapungua kwa kiasi kikubwa.

Matukio mengine ya kujichukulia sheria mkononi ni mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi.

Ni matukio ambayo hayawezi kuzuiwa na doria za askari Polisi mitaani kwani hutendeka wakati mwingine ndani ya nyumba, majumba ya starehe au mashambani.

Hivyo ni vyema jamii ikashirikiana kutoa elimu kwamba suluhisho si kujichukulia sheria mkononi, kwamba ukifanya hivyo nawe hutabaki salama, bali utakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Na matokeo yake kuhukumiwa kunyongwa au kifungo cha maisha jambo ambalo litakutenga na familia yako na kupoteza muda wako muhimu wa kufanya kazi zako za kujiletea maendeleo.

Kama ni suala la wivu wa mapenzi kwa kugundua kuwa mwenzako ana mahusiano ya pembeni utatuzi si kuchukua sheria mkononi bali ni kufungua kesi ya madai mahakamani dhidi ya unayemtuhumu ili kudai fidia.

Jambo hilo litakufanya uendelee na uhuru wako na kazi zako za kujiletea maendeleo, badala ya kukosa vyote (Uhuru, familia na mali zako) na mshahara utakuwa kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Pia, alitoa mfano kuwa zipo nchi ambazo matukio kama hayo ni machache sana na hilo limewezeshwa na jamii kutambua thamani ya uhai, thamani ya kuishi na familia ukiwa huru, thamani ya kuwa huru na kufanya kazi zako za kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Pia wametambua dawa ya tatizo sio kulitatua kwa kutengeneza tatizo lingine na pengine kubwa zaidi.

“Dawa au ufumbuzi ni kufuata sheria, kanuni na taratibu na kutambua thamani yako kama binadamu, utu na thamani ya muda,” anasema msemaji wa Jeshi la Polisi.

Wananchi kwa namna moja ama nyingine hawana budi kufuata sheria za nchi kwa kuwakamata wahalifu na kuwakabidhi kwa Jeshi la Polisi ama mamlaka zingine za kisheria ili waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwamba kuwaadhibu ni jambo ambalo linaweza kusababisha majeruhi hata mauaji kwa watu wanaotuhumiwa kutenda uhalifu ndani ya jamii.

Tuachane na tabia ya kujichukulia sheria mkononi, ina hasara kubwa kwa maisha yako.

Imetolewa na:-

Kitengo cha Uhusiano,

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi,

Dar es Salaam,

[email protected]

Habari Kubwa