Wananchi nguzo muhimu ujenzi wa miundombinu ya elimu-1

15Jun 2019
Reubeni Lumbagala
DAR
Nipashe
Wananchi nguzo muhimu ujenzi wa miundombinu ya elimu-1

ILI kutoa elimu bora yenye manufaa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, suala la miundombinu bora ya kutolea elimu linapaswa kutekelezwa kwa vitendo.

Wanafunzi na walimu wanapaswa kujifunza katika mazingira bora yatakayochochea kujifunza wenye tija. Vyumba vya madarasa, maabara, maktaba, nyumba za walimu, vyoo na ofisi ni miongoni mwa miundombinu muhimu ya kufanikisha kujifunza na una matokeo chanya.

 

Hivyo, shule zote zinapaswa kuwa na miundombinu bora ya kutolea huduma ya elimu, ili kuifanya iwe bora kwa wanafunzi wanaoipata.

 

Gharama za kujenga, kuboresha na kukarabati miundombinu ya shule nchini ni kubwa sana, ambayo serikali haiwezi kuifanikisha pekee yake.

 

Hivyo, mchango wa jamii katika kusaidia kufanikisha shughuli hizo, unapaswa kutolewa ili kuwasaidia wanafunzi kujifunza katika mazingira bora yatakayowavutia kupenda shule na kujifunza.

 

Serikali inatekeleza kwa vitendo sera ya elimu msingi bila ya malipo. Kila mwezi ni takribani Sh. bilioni 24 zinatolewa kugharamia utekelezaji wa sera hiyo.

 

Katika kuondoa urasimu wa fedha hizo, serikali inaingiza fedha hizo moja kwa moja katika akaunti za shule, ili zisaidie shughuli mbalimbali kama vile uendeshaji taaluma, utawala, michezo, mitihani, ukarabati au matengenezo madogomadogo, ununuzi wa madawa baridi kwa wanafunzi.

 

Pia, serikali imetoa fedha nyingi katika ukarabati wa shule kongwe na vyuo vya ualimu kote nchini.

 

Sambamba na hilo, serikali inatoa fedha katika kufanikisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika shule nyingi za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.

 

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara, alilitaarifu Bunge kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019, serikali imetoa Sh. bilioni 29.9 kukamilisha maboma 2,392 ya madarasa nchini kote.

 

Naibu Waziri Waitara, alisisitiza kuwa: “Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya elimu kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.”

 

Yote hayo yanafanywa na serikali na yanathibitisha nia njema ya serikali kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma katika mazingira mazuri, ili kupata elimu bora.

 

Kwa kuwa serikali imejipambanua kugharamia utekelezaji ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu, wananchi hawana budi kuunga mkono juhudi hizo, ili watoto wao wanaosoma katika shule hizo, wajifunze katika mazingira yanayovutia.

 

Kuvutia huko kunaelezwa ni kuhakikisha wanachangia rasilimali fedha na nguvu kazi, ili kujenga maboma ya madarasa, ofisi, vyoo, maktaba, maabara na hatimaye serikali kukamilisha maboma hayo.

 

Msingi wa wananchi kuhamasika kuchangia fedha na nguvukazi katika ujenzi wa miundombinu ya shule wilayani Kongwa, inatokana na elimu inayotolewa na mbunge Job Ndugai, kwa kushirikiana na viongozi wengine wilayani humo.

 

Hao anawataja ni Mkurugenzi wa Halmashauri na Maofisa Elimu, kwa kuwaambia wananchi kuwa, shule za msingi na sekondari ni mali yao kwa kushirikiana na serikali, hivyo wana wajibu wa kushiriki katika maendeleo yake.

 

Kutokana na hamasa hiyo, wananchi wamejitolea fedha na nguvu kazi katika ujenzi wa maboma ya madarasa, hali iliyosababisha serikali kuunga mkono juhudi hizo za maendeleo kwa kutoa fedha za kumalizia ujenzi ulioanzishwa na wananchi.

 

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kongwa, Nelson Milanzi, serikali imetoa Sh. milioni 25 kwa Shule ya Sekondari Kibaigwa, kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili.

 

Pia, imetolewa fedha kusaidia shule sita, kila moja ilipatiwa Sh. milioni 25 kukamilisha madarasa yake mawili, ambazo ni katika Sekondari za Makawa, Pandambili, Ng’humbi, Banyibanyi, Mnyakongo, Hembahemba.

 

Aidha, kuna shule nyingine mbili ambazo kila moja ilipatiwa Sh. milioni 50, kukamilisha madarasa manne kila moja. Hizi ni sekondari za Ngomai na Songambele.

 

Ofisa Elimu Ufundi Wilaya ya Kongwa Emmanuel Factory, aliongoza kikao cha kujadili ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Laikala na wananchi wakakubali kujitolea nguvukazi.

 

Pia, ahadi yao ni kuwa boma la vyumba viwili na ofisi vinakamilika, ili kuunga mkono ahadi ya Mbunge wa Kongwa Job Ndugai, ya kutoa mifuko 50 ya saruji mara tu wananchi watakapojitolea kuchimba msingi.

 

Katika hali ya kufurahisha, mafundi wameamua kupunguza gharama za ujenzi, pia kuahidi baadhi ya kazi zitakavyofanyika bure, kwani wao na watoto wao ni zao la Shule ya Msingi Laikala.

  • Reubeni Lumbagala, ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali, iliyoko wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

Anapatikana kwa namba: (+255) 764666349. Itaendelea Jumamosi ijayo.

Habari Kubwa