Wananchi waitumie vyema fursa hii iliyotolewa na NEC

17Jul 2019
Reubeni Lumbagala
Nipashe
Wananchi waitumie vyema fursa hii iliyotolewa na NEC

TUME ya Taifa ya Uchaguzi hapa nchini (NEC) ipo kazini kuhakikisha kila mwananchi mwenye sifa za kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura anapata haki ya kujiandikisha ili baadaye ashiriki siku ya uchaguzi kuwachagua viongozi bora kwa maendeleo.

Wananchi wakijipanga tayari kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura. PICHA: MTANDAO

Mkoa wa Kilimanjaro umepata heshima ya kuwa mkoa wa kwanza nchini ambapo kesho Julai 18, kutafanyika uzinduzi wa shughuli ya uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo inayotarajiwa kufanyika katika uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi.

Kazi hiyo ya kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura itaendelea hadi Julai 24, ili kutoa nafasi kwa wananchi kujiandikisha na hivyo kuwawezesha kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na uchaguzi mkuu Oktoba mwakani.

Hii ni nafasi muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka ambao watashirikiana nao katika juhudi za kuleta maendeleo nchini.Kimsingi, wananchi wanapaswa kuthamini fursa hiyo ya kutumia haki yao ya kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Zoezi la kuwachagua viongozi hao linaanzia kwenye kujiandikisha ili kuweza kupiga kura siku ya uchaguzi.

Hivyo, kujiandikisha ndiyo mwanzo wa kupata viongozi bora. NEC inatumia vyombo mbalimbali vya habari kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari hilo la kudumu la wapigakura.

Hivyo basi, ni vyema wananchi kuitumia elimu kwa umma inayotolewa na NEC pamoja na wasanii mbalimbali ili kuona umuhimu wa kujiandikisha.

Wananchi wa Kilimanjaro wazitumie vizuri siku saba za kujiandikisha ili muda ukifika wachague viongozi wao. 

Kila mwananchi anayepata elimu ya kujiandikisha katika daftari hilo ahakikishe anaitumia elimu atakayoipata katika kuwahamasisha wengine kwenda kwenye vituo vilivyoainishwa na NEC kujiandikisha.

Hatua hiyo itawezesha kupatikana viongozi bora wa serikali za mitaa na mwakani madiwani, wabunge na Rais bora kwa ustawi wa maendeleo.Pamoja na wananachi kuwa na shughuli nyingi za uzalishaji mali, wanapaswa kuhakikisha hawaiachi fursa hii adhimu ya kujiandikisha kupigakura.

Wananchi wahakikishe kuwa wanatenga muda wa kazi na muda wa kwenda katika vituo vya kujiandikisha.

Upo utamaduni mbaya miongoni mwa wananchi ambao inapotokea fursa kama hii huzembea kwenda kujiandikisha katika siku za mwanzoni na hatimaye kusubiria siku ya mwisho ndipo hujitokeza.

Ni vyema wananchi wa Kilimanjaro kuzitumia vizuri siku hizo saba kujiandikisha ipasavyo pasipo kusubiri huruma za tume ya uchaguzi kuongeza siku.

UANDIKISHAJI WANANCHI KATIKA MIKOA MINGINE

Baada ya kumalizika zoezi la uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapigakura mkoani Kilimanjaro, zoezi hilo litaendelea katika mikoa mingine ya Tanzania.

Hivyo basi, wananchi wa mikoa mingine wajiandae kisaikolojia katika kuhakikisha muda utakapofika katika mikoa, wilaya na kata zao, wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.

Wananchi kubaki nyumbani bila kujiandikisha, hakutawasaidia kutatua kero zao zinazowasibu.

Kura zao zina maana kubwa katika kuchangia kutatua kero zao kupitia kupata viongozi bora watakaokuwa chachu ya kutatua kero za wananchi.

Aidha, Tume ya Uchaguzi ina wajibu si tu kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura, lakini pia kuhusu nguvu ya kura zao katika maendeleo.

Baadhi ya wananchi hujiandikisha ili kupata vitambulisho kwa matumizi yao binafsi na si kwa kipaumbele cha kushiriki kuwachagua viongozi katika uchaguzi.

Tathmini ya chaguzi nyingi hapa nchini zinaonyesha uwiano usioendana kati ya wanaojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na wanaojitokeza siku ya uchaguzi kupiga kura.

Kwahiyo, ni vizuri elimu kwa umma inayotolewa na NEC kuhusiana na kujiandikisha, isisitize pia agenda ya nguvu ya kura za wananchi katika kupata viongozi bora na makini.

Wananchi waelimishwe kuwa wasiishie tu kujiandikisha, lakini pia washiriki kupiga kura siku ya uchaguzi.

Muhimu ni NEC kuwekeza katika elimu kwa umma ili kuwaelimisha zaidi wananchi kuhusu umuhimu wa ushiriki wao katika uchaguzi.

Kwa mujibu wa katiba yetu, uchaguzi wa serikali za mitaa na ule uchaguzi mkuu unafanyika kila baada ya miaka mitano.

Hii inaonyesha kuwa uchaguzi si tukio la kila siku, ni tukio linalojitokeza mara moja ndani ya miaka mitano, achilia mbali chaguzi ndogo za kujaza nafasi zilizo wazi.

Kutokana na upekee wake, wananchi watumie fursa hii katika kujiandikisha, kuwasikiliza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na mwishoni kuwachagua viongozi bora wanaokidhi matarajio yao.

Jambo jingine la msingi ni wananchi kutunza shahada zao za kupigia kura ili wazitumie siku ya tukio lenyewe. Kadi yako, kura yako, kajiandikishe na kuboreshe taarifa zako.

Mimi nipo tayari kujiandikisha na kupiga kura, Wewe je? Tafakari.

Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa Jijini Dodoma.Maoni: (+255) 764 666349.