Wanaoleta 'unga', kuuza wanaogopwa Z’bar?

28Feb 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Wanaoleta 'unga', kuuza wanaogopwa Z’bar?

TATIZO la dawa za kulevya limekithiri na huwezi tena kuliita tishio ila ni janga, baa na msiba mkubwa kadri siku zinavyokwenda mbele.

Dawa za kulevya.

Inasikitisha sana ukipita katika mitaa maarufu ya mji wa Zanzibar na kushuhudia vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa afya zao zikiwa zimedhoofika.

Si kitu cha ajabu kuwakuta wamelala vijiweni kama watu walio kwenye matanga ya msiba huku wengine wakiwa wamekaa wakiwa wamesinzia na sigara zao mkononi.

Mitaa yenye 'wateja' (watumiaji) wengi wa dawa hizo kwa kiwango kikubwa ni pamoja na mtaa wa Kundemba, Mikunguni, Jang’ombe, Miembeni, Gulioni, Mfenesi Maziai, Kikwajuni, Mwembetanga, Mtendeni na Mchangani. Aidha, mitaa ya Mji Mkongwe ya Mkunazini, Kiponda, Shangani, Hurumzi na Soko Muhogo hali ni mbaya pia.

Matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa visiwani Zanzibar na kuathiri vijana wengi wanaopata matatizo ya ugonjwa wa akili, maambukizi ya VVU, kushiriki vitendo vya uhalifu pamoja na kuvurugika kwa mielekeo ya maisha yao.

Pamoja na kuwepo kwa mamlaka za dola katika serikali za mitaa, biashara ya dawa za kulevya imekuwa ikifanyika hadharani, mchana kweupe, bila kimeme wala kificho.

Kwa bahati mbaya, watu wazima nao sasa wameanza kuwa wanatumiaji wazuri wa dawa hizo hali inayochochea vijana kuona kushiriki jambo hilo ni kitu cha kawaida.

Nyumba zinazouza 'unga' Zanzibar zinajulikana pamoja na wahusika lakini jamii na viongozi wa serikali za mitaa (masheha) wameshindwa kuchukua juhudi za kuondoa tatizo na kuacha nguvu kazi ikiendelea kupotea kwa kasi visiwani.
Kama wateja 'wanaobembea' wako mitaani, ni kitu gani kinachozuia wasikamatwe na kutakiwa kuonyesha mahali walikonunua?

Zanzibar imebahatika kuwa na vikosi vingi vya Ulinzi na asilimia 90 ya askari wake wanaishi uraiani. Lakini cha ajabu wameshindwa kusadia kuondoa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na sasa mambo yanafanyika hadharani licha ya wauza unga wa jumla na rejereja kufahamika mitaani.

Kama wapo askari wa kutosha kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Chuo cha Mafunzo, Kikosi cha Valantia (KVZ), Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KZU), Usalama wa Taifa, Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Polisi, kwanini hakuna ufumbuzi wa tatizo hilo?

Kama askari wa vikosi hivyo wangeweza kushirikiana kama wanavyoshirikiana wakati wa Uchaguzi Mkuu kuimarisha usalama wa raia na mali zao tatizo la Dawa za kulevya lingebakia historia Zanzibar.

Wakati tatizo la matumizi ya dawa za kulevya likiwa na mjadala mkubwa katika jamii, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha asilimia 25 ya wagonjwa wa akili wanaofikishwa katika hospitali ya Kidongochekundu ni watu walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya.

Kutokana na waathirika wengi kukabiliwa na hali ngumu ya kipato wameanza kutumia vidoge vya usingizi na kusababisha vijiwe vingi kugeuka kama watu wapo matangani katika msiba wakichapa usingizi mchana na usiku.

Biashara ya dawa za kulevya imekuwa kubwa kiasi kwamba badala ya unga kuingizwa Zanzibar kutoka nje, sasa unasafirishwa kutoka Zanzibar kwenda nje ya nchi na tayari kuna vijana wawili wamefungwa baada ya kukamatwa nchini China.

Tume ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar imesema katika ripoti yake ya Mwaka 2013/2014 kuwa watu 22 walikamatwa kwa makosa ya dawa za kulevya na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Tume hiyo ambayo ipo chini ya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, imeonyesha uwezo mdogo katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya Zanzibar, hata hivyo.

Tume hiyo imeleza kuwa watu 342 wanaotumia dawa za kulevya walipewa ushauri nasaha juu ya madhara ya matumizi dawa za kulevya Mwaka 2015/2016.

Tume kutoa ushauri nasaha badala ya kuwakamata wanaoingiza na kuuza mitaani unga sio ufumbuzi wa tatizo la dawa za kulevya Zanzibar kwa sababu ni sawa na kukata tawi badala ya shina.

Malengo matatu ya Tume hiyo yalikuwa kupunguza matumizi ya dawa za kulevya, kupunguza usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya pamoja na kuweka mazingira bora ya kazi, lakini bado tatizo la dawa za kulevya limendelea kuongezeka Zanzibar.

Hatua ya serikali kuwa na kamati za udhibiti wa dawa za kulevya katika ngazi ya serikali za mitaa (shehia) ni mpango ambao unaonekana wazi umeshindwa kuleta tija baada ya vijana kuendelea kuathirika na tatizo hilo.

Uwapo wa rushwa katika biashara ya dawa za kulevya kwa muda mrefu umekuwa ukilalamikiwa kuwa kikwazo kikubwa katika usimamizi wa sheria na kusababisha biashara hiyo kufanyika mitaani bila ya wahusika kuhofia vyombo vya dola.
Kwanini biashara ya dawa za kulevya na matumizi yake yafanyike hadharani bila ya wahusika kuchukuliwa hatua wakati hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar?

Jibu ni kwamba rushwa imeendelea kuathiri mfumo mzima wa kupambana na biashara ya dawa za kulevya na kusababisha wahusika kuonekana na kuishi kama wafalme.

Nguvu zao za kiuchumi zimekua kikwazo kikubwa katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya na kusababisha vielelezo vya kesi kubadilika vikiwa katika mamlaka yenye dhamana, na kuwa unga wa sembe au saruji badala ya dawa za kulevya.
Mamlaka za kusimamia sheria ikiwemo na Ofisi ya Mkemia mkuu lazima wabadilike katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufanikisha mpango wa kupambana na tatizo la dawa za kulevya Zanzibar.

Zanzibar bila ya dawa za kulevya inawezekana kama serikali itapambana na tatizo la rushwa kwa vitendo pamoja na wananchi kuwa tayari kutoa mashirikiano katika kupambana na tatizo hilo, ikiwemo kuwafichua wahusika na kuwafikisha mahakamani .

Habari Kubwa