Wanaosomea digrii wabuni nyenzo kwa mgonjwa moyo bila daktari

30May 2019
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
Wanaosomea digrii wabuni nyenzo kwa mgonjwa moyo bila daktari
  • Roboti inayotekeleza kazi ya bingwa
  • Michakato tiba imepatiwa ‘short cut’

WAKATI serikali inawekeza kupata madaktari bingwa wa kutibu magonjwa ya moyo nchini, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, Kitengo cha Uhandisi wa Umeme na Mawasiliano, jijini Dar es Salaam, kimebuni teknolojia mpya ya kukabiliana na uhaba huo wa matabibu bingwa.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Joseph, wakielezea mradi wao wa kutatua changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa wa moyo nchini. Wa kwanza kushoto ni mhadhiri, Dk. Dk. Lawrence Kerefu.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inasema tangu kuanza kutoa huduma ya matibabu ya moyo mwaka 2015, imeshaona wagonjwa zaidi ya 200,000, huku idadi ya madaktari bingwa walioko hawazidi 50.

Wanafunzi wa Chuo cha Mt. Joseph, Kitengo cha Uhandisi Umeme na Mawasiliano, kimeanzisha teknolojia hiyo ya matibabu, ikilenga kukabiliana na changamoto ya uhaba wa bingwa hao.

Mukrim Omary, ni kati ya wanafunzi wanne waliobuni tekenolojia tajwa, anayetaja sababu ya kufikia uamuzi huo, kwanza walipobaini kuwapo changamoto hiyo.

Anaifafanua katika lugha ya tahadhari kwamba iwapo haitatafutiwa ufumbuzi, itaongeza idadi ya vifo nchini vitokanavyo na magonjwa ya moyo.

Omary anasema ameona vyema kutafuta mbadala wa kutoa huduma ya matibabu, ili kuharakisha maamuzi ya kibunifu, mbadala ya kutegemea pekee kwa madaktari wanaotumia miaka minane kusomea ubingwa wa kutibu magonjwa hayo.

Kwa mujibu wa mtaala wa mafunzo hayo, inawachukua miaka mitano darasani na mmoja wa mafunzo kwa vitendo kutihimu shahada ya kwanza, kisha miaka miwili ya shahada nyingine ya ubobezi katika eneo tajwa; moyo. 

Anataja sababu nyingine waliyoiona ni kuwapo ongezeko la wagonjwa wanaotokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, yanayosababisha kuibuka magonjwa mengi ya moyo.

“Tulijiuliza kama madaktari bingwa waliopo nchini wapo 20 na wagonjwa wanaougua magonjwa hayo ni zaidi ya 60,000 kwa mwaka, ina maana ni tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka. Tukaamua kubuni teknolojia ya kutibu ugonjwa huo kwa njia ya roboti,” anasema Omar.

Anasema kwamba, waliona vyema kutengeneza mfumo usio wa kibinadamu, kwa ajili ya kuchukua vipimo vya wagonjwa, kuupima ugonjwa na kutoa tiba kwa wanaoumwa moyo.

Omary anaeleza kuwa, kuna roboti waliowatengeneza wenye hisia au kitaalamu ‘sensor’ zitakazoupima moyo, kiwango cha damu na msukumo wa damu, mapigo ya moyo na joto la mwili.

Anasema, vipimo hivyo vinawezesha kubaini kama moyo una tatizo na kueleza tiba za ugonjwa ulipo katika moyo, hivyo kuanza matibabu haraka.

Mwanafunzi huyo anasema, pia wametengeneza mfumo wa moyo kwenye kompyuta, ambao utachukua taarifa zote za mgonjwa, kama vile jina, umri na taarifa nyingine muhimu kwa matibabu.

Omary anasema, urahisi wa mfumo huo ni kutoa huduma katika maeneo ambako wananchi hawafikiwi na huduma, mfano hao ni vijijini.

Anataja faida zake ni kuokoa muda, gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma, kupunguza msongamano wa wagonjwa hospitalini, foleni za wagonjwa wanaosubiri huduma kwa muda mrefu.

Utakavyofanya kazi.

Mwanaidi Lulanga, anasema roboti huyo atafungwa katika ofisi za wilaya na mikoa, wakati mfumo huo utakuwa katika kila halmashauri katika hospitali zote za serikali.

Anasema, wakati mgonjwa huyo anapimwa na sensa hiyo inayowekwa mwilini na kuchukua dakika saba kutoa majibu, itaunganishwa moja kwa moja na roboti iliyopo ofisi ya wilaya au mkoa kutoa majibu ya mgonjwa huyo na maelezo ya tiba yake.

Mwanaidi anasema, mtoa huduma za afya atachukua taarifa za mgonjwa na vifaa hivyo, kisha kuvifunga katika mwili wa mgonjwa na wakati vinafungwa, mfumo utakuwa unachukua taarifa za mwili.

“Mfumo huu unachukua taarifa ndani ya dakika saba na kutoa majibu kulingana na ugonjwa uliogundulika na kueleza nini tiba halisi,” anasema Mwanaidi.

Pia, anasema kifaa hicho kinaweza kumilikiwa na mtu yeyote aliye na upeo wa kielimu na uzoefu wa kupata huduma hiyo.

Anafafanua kwamba, namna ya kuunganisha mfumo huo ni kutumia simu ya mkononi aina ya ‘smartphone.’ Anasema gharama ya mfumo mzima, kuutengeneza hadi akatoa huduma ni Dola za Marekani 5,000 sawa na Sh. milioni 11.5.

Mwanaidi anasema, makisio ya gharama ya kumtibu mgonjwa, yanaweza kupungua kulingana na kifaa kitakapofungwa kwenye vituo vya afya vya serikali inaweza kuwa bure, kama itamiliki mifumo yake.

Anasema watu binafsi wanaweza kuchangia gharama kidogo, kulingana na matakwa ya mtoa huduma, lakini haziwezi kulingana na zile ambazo mgonjwa angetumia kufuata huduma hiyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

Mwanataaluma afafanua

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Joseph, Dk. Lawrence Kerefu, ameiambia Nipashe kuwa wanafunzi wa Kitengo cha Ubunifu na Ujasiriamali Teknolojia, walioamua kuibua wazo hilo wanalolifanyia kazi ni sehemu ya mradi wao na kujiajiri.

Anasema, chuo kilianzisha kitengo cha kuwawezesha wanafunzi kujiandaa, kwa ajili ya kujiajiri na kuendelea kukuza uchumi wa Taifa, ili wanaohitimu masomo wajiajiri na kuwaajiri vijana wengine.

“Tuliona mbali na chuo kutoa elimu bora inayomfanya mhitimu kuwa mfanyakazi bora katika idara zote. Ni vyema, pia kuangalia namna ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa kuwawezesha wanafunzi kujijengea msingi wa kuajiri wanapohitimu masomo,” anasema Dk. Kerefu.

Anasema, badala ya mwanafunzi kutoka chuo asubiri kupata ajira, anapaswa atoke akiwa na mtazamo wa kujiajiri na kufungua kampuni yake.

Dk. Kerefu anasema, wanafunzi wanapaswa kuangalia jamii, matatizo yanayowagusa jamii, ili iwe fursa ya kibiashara kwa kuyatatua matatizo yao, badala ya kuwa sehemu ya matatizo, ilhali wamepata elimu.

Mhadhiri huyo anasema, wanawapa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali, hali inayowapatia ufahamu wa kuanzisha kampuni zao wenyewe.

Anasema, kupitia mradi walioanzisha, wanategemea kupitia vituo vya afya na hospitali zote nchini, madaktari na watoa huduma za afya watakaopewa mafunzo ya kutumia teknolojia hiyo, inayoenda kukabiliana na uhaba wa watoa huduma za afya.

Utekelezaji wake

Dk. Kerefu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Ubunifu na Ujasiriamali Teknolojia, anasema moja ya jukumu la chuo kilichomwajiri ni kuwasimamia wanafunzi hao kuhakikisha wanatimiza lengo hilo, mara wanapohitimu masomo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Katika hilo, anasema watahakikisha wanawawezesha kwa fedha za kujikimu, ili waendelee kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Anafafanua hatua hizo ni kuwafuatilia kwa hatua, kuhakikisha wanasajili kampuni yao, biashara na kupata wafadhili, kabla ya kuwaruhusu kuendelea kusimamia mradi huo.

Anasema, pia wanaingia nao mkataba wa kuendelea kufanya kazi katika kipindi hicho cha miezi sita hadi mwaka watakaokuwa nje ya chuo, wakiendelea na shughuli za mradi huo.

Mkurugenzi anaahidi endapo watakamilisha mradi huo, wataomba kampuni tarajiwa ikilipe chuo asilimia moja ya faida wanayopata, ili kuwezesha miradi mingine kwa wanafunzi wa baadaye.

Dk. Kerefu, anazidi kueleza: “Tunawaambia kabisa kujiajiri ni kuendeleza ndoto zao, lakini kwenda kuajiriwa ni kuendeleza ndoto za watu wengine. Hivyo, wanapaswa kujitahidi kuendeleza ndoto zao, ndio maana tumeamua pia kuwasimamia wakati ambao watakuwa wamemaliza chuo.”

Mtaaluma huyo anasema, katika mradi huo wameshaishirikisha Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ambayo wameahidi kushirikiana nayo.

Aidha, anasema katika ukuzaji vipaji vya wanafunzi wanaosoma chuoni hapo na kusukuma ajenda ya kufikiaTanzania ya Uchumi wa Kati wa Viwanda ifikapo 2025, chuo kimejikita kuelimisha  nadharia kwa wanafunzi wake, ili kuwapa ujuzi wa kutosha.

Kulivyo nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi, anasema kwa siku wanawaona wagonjwa 300 hadi 400 na madaktari wanaowahudumia wanaohitajika ni 50, ingawa katika uhalisia wako chini ya 20.

Pia, anasema, kuna viashiria vya ongezeko la idadi ya wagonjwa wa moyo kila mwaka, takwimu zikionyesha idadi ya wagonjwa kuongezeka kila mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu za asasi hiyo, mwaka 2015 walipoanza rasmi kutoa huduma, waliwaona wagonjwa wa nje 23,000; mwaka 2016, wagonjwa 53,000; mwaka 2017, wagonjwa 60,000; na mwaka jana wagonjwa 76,00.

“Ukijumlisha hii miaka mitatu tumeshahudumia wagonjwa wa nje zaidi ya 200,000, tumelaza wagonjwa zaidi ya 11,000, tumefanya upasuaji wa kufungua kifua kwa kusimamisha moyo wagonjwa 800,” anasema.

“Tumeshawafanyia upasuaji kwa tundu dogo wagonjwa 2,056. Kiujumla tumehudumia wagonjwa zaidi ya 250,000.” anasema Prof. Janabi katika taarifa zake na vyombo vya habari.

WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kuwa jumla ya watu milioni 18 kila mwaka wanaopoteza maisha, kutokana na ugonjwa wa moyo sawa na asilimia 31 ya wagonjwa wote.

Pia, WHO  inasema, asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo, vinatokea  barani Afrika. Kwingineko ambako hali si nzuri ni Latin Amerika na barani Asia.

Habari Kubwa