WANASAYANSI: Fursa ya kutoa uzoefu huongeza afya ya wastaafu

16Mar 2017
Raphael Kibiriti
Dar es Salaam
Nipashe
WANASAYANSI: Fursa ya kutoa uzoefu huongeza afya ya wastaafu
  • .Kizazi kilichokula chumvi nyingi hujisikia manufaa ya kiafya kinaporithisha maarifa yake kwa vizazi vingine.
  • . Tendo la kizazi cha zamani kusaidia wanaukoo, hutoa hisia ya utimilifu wa majukumu yao

WANASAYANSI wamesema tendo la kurithisha lulu ya hekima waliyonayo wazee kwa kizazi kipya huwaongezea afya katika uzee wao na kuwapa mtazamo mpya juu ya maisha wanayoendelea kuyaishi.

Matokeo ya utafiti yaliyotolewa hivi karibuni yanaonyesha kwamba wazee wanaoshirikisha ujuzi, maarifa, hekima na siri walizonazo kwa familia, rafiki, majirani zao au hata kwa wageni huyaona maisha yao kuwa na maana zaidi.

Lakini wanasayansi wanaamini kwa upande mwingine kwamba, hali hiyo haiko hivyo kwa wastaafu wasiopata fursa ya kushirikisha uzoefu wao, kwani huona maisha hayana thamani yoyote.

Utafiti huo uliochapishwa kwenye Jarida la Saikolojia ya Jamii nchini Marekani, unahitimisha kwamba, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 wanaonekana kuwa na furaha zaidi wanapopata fursa ya kutoa ushauri wa aina mbalimbali kwenye nyanja tofauti za kimaisha.

Hata hivyo, matokeo yanasema kuwa pamoja na wazee kuonekana kufaidika kwa hili la kutoa ushauri, lakini ni bahati mbaya kwamba linatokea katika umri ambao fursa za kufaidika na huduma ya kutoa ushauri zinakuwa ni adimu.

Profesa Markus Schafer, kutoka Chuo Kikuu cha Toronto anasema kuwa, uhusiano kati ya kutoa ushauri na maana ya maisha, hauonekani kwenye makundi ya umri mwingine.

“Kwa ujumla tunatafsiri matokeo haya yana maana ya uwapo wa mahitaji ya maendeleo kwa watu wenye umri mkubwa, na nia ya kutoa mchango kwa ustawi wa wengine,” anasema Profesa na kuongeza:

“Wakati suala la kutoa ushauri linaonekana kuwa muhimu zaidi kwa wazee, hata hivyo fursa za kufanya hivyo zinaonekana kuwa finyu ama kuyeyuka katika umri wao.”

Profesa Schafer na Mwanafunzi wa Udaktari wa Uzamivu katika Sosholojia, Laura Upenieks, walichambua utafiti kwa watu wazima 2,583 nchini Marekani.

Katika uchambuzi wao walikuta kwamba asilimia 21 ya walio katika umri wa miaka ya 60 na asilimia 27 ya walio na umri wa zaidi ya miaka hiyo, waliripoti kutokupata fursa ya kutoa ushauri wa hata kwa mtu mmoja katika kipindi cha mwaka uliopita, ikilinganishwa na takribani asilimia10 ya wale walio chini ya miaka 60.

Profesa Schafer anasema: “Kanuni katika umri wa kawaida zinaonyesha kwamba, mwelekezaji na mshauri bora ni yule mtu ambaye ana uzoefu mkubwa wa maisha.”

Hata hivyo, anafafanua kuwa kwa kulinganishwa na vijana, watu waliokula chumvi nyingi huwa wana majukumu machache ya kijamii, hawashiriki katika shughuli nyingi za kijamii na pia huwa hawakutani na watu wengi wa kada mbalimbali.

“Kwa hali hiyo wakati mtu mwenye wastani wa umri wa miaka 65 anaweza kuwa na busara zaidi ya kijana mwenye wastani wa umri wa miaka 30, sababu za muundo wa kijamii na idadi ya watu zinatoa fursa zaidi kwa kijana ya kutoa ushauri katika nyanja mbalimbali,” anasema.

Baadhi ya wasomi wanadai kwamba kiini cha mada, yaani wazo kwamba mmoja ni wa maana na ana matokeo chanya dhidi ya watu wengine, huwa ni la hatari katika umri wa kati ambapo watu wengi hustaafu na kuingia awamu isiyo na vingi vya kufanya katika maisha.

Profesa Schafer anasema, mazingira ya mada hiyo yanasaidia kuelezea ni kwa nini katika kipindi hiki cha maisha ya ustaafu huwa ni wakati muhimu kwa watu kujisikia kwamba bado wanaweza kuwa na ushawishi kwa wengine kupitia matendo kama yale ya kutoa ushauri.

“Matokeo haya yanapaswa kuchochea tafakuri juu ya masuala ya kijamii ya jamii za Marekani na namna watu waliokula chumvi nyingi wanavyoingia katika jamii hii,” anasema na kuongeza:

“ Matokeo ya utafiti wetu yanasisitiza juu ya umuhimu wa kuwapa watu wazima jukwaa la kushirikisha busara na uzoefu wa maisha waliyoyapitia.”

Profesa anasema, shule, makanisa, mashirika ya kiraia, na makundi mengine ya kijamii yanaweza kufikiria jinsi ya kusaidia kushirikishana ushauri na uzoefu baina ya vizazi, na hivyo kujenga mazingira yatakayowezesha waliokula chumvi nyingi kuwa watoa ushauri.

Habari Kubwa