Wanasiasa jifunzeni kimsingi kuwa na akiba ya maneno

01Nov 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Wanasiasa jifunzeni kimsingi kuwa na akiba ya maneno

JUMATATU wiki hii aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lazaro Nyarandu alitangaza kukihama chama hicho tawala huku akitoa sababu mbalimbali zilizomfanya afikie uamuzi huo.

Lazaro Nyalandu (Aliyeshika kipaza sauti), ametangaza kukihama chama chake cha Mapinduzi (CCM).PICHA: MTANDAO

Miongoni mwa sababu hizo ni kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu na ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania.

Sababu zingine alizozitaja ni za kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru uliainishwa na kuwekwa bayana kikatiba.

“Mimi naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi (CCM), nikiwa nimekitumikia kuanzia ngazi ya uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,” anasema na kuongeza:

“Kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliopo Tanzania sasa, CCM imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia serikali kama ilivyokuwa hapo awali.”

Kwa ujumla Nyalandu alitoa sababu nyingi zilizolenga kuilaumu CCM ambayo kwa maelezo yake mwenyewe, ameitumikia kwa muda mrefu akiwa ameshika nafasi mbalimbali za uongozi.

Binafsi sina tatizo na hatua yake ya kuhama chama hicho na kwenda kwingine kwa sababu ni haki yake ya kidemokrasia na huwa haingiliwi au kuzuiwa na mtu yeyote, ila ninasikitishwa na hizo tuhuma alizokirushia chama chake hicho.

Yeye kama kiongozi nilitegemea kuwa angetumia nafasi ya vikao halali kuelezea kero zake hizo kuliko utaratibu aliotumia ambao kimsingi unasababisha baadhi ya watu kuwa na maswali mengi kwake.

Anaamini kuwa kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna moja au nyingine, eti CCM nayo imekuwa chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika hatamu na kuikosoa serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere!

Inawezekana alichokisema kikawa sahihi, lakini sio kwa njia hiyo bali alitakiwa kutumia vikao ndani ya chama na kama ni kuhama angeondoka tu pengine kwa sababu ya kubadili upepo badala ya 'kushambulia' kule alikotoka.

Hii imekuwa ni kama tabia ya baadhi ya wanasiasa hapa nchini wanapohama vyama vyao huvishambulia kwa maneno makali, lakini baadaye wanapoona mambo yamewashinda kule walikohamia hurudi tena kwa vyama vyao vya zamani walivyovishambulia wakati wanahama.

Ni vizuri nieleweke kuwa mimi sio mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila sio vibaya kueleza kile ninachoamini kwamba kinaweza kuwasaidia wanasiasa.

Nyalandu amehama kutoka CCM ikiwa ni wiki chache tangu aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi Taifa wa Chama Cha ACT Wazalendo, Samson Mwigamba kutangaza kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwigamba alitoa sababu za kuhamia CCM kwamba chama hicho kwa sasa ndicho kinachoakisi kwa karibu itikadi, falsafa na sera za ACT – Wazalendo ambazo yeye Mwigamba) na wenzake walishiriki kuziasisi.

Kama alivyofanya Nyalandu, Mwigamba naye alirushwa madongo kwa upinzani akisema anajiunga katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ili kujitenga na upinzani unaokerwa na mafanikio ya serikali.

Swali kwa wanasiasa hawa nikianzia kwa Nyalandu, je, CCM ikirudi kwenye mwelekeo atarudi kutoka alikohamia? Na kwa upande wa Mwigamba, je Serikali ikishindwa kufikia mafanikio anayosema atarudi upinzani?

Wanasiasa mjifunze kuwa na akiba ya maneno.

Nyalandu analaumu CCM, Mwigamba analaumu upinzani, sasa wananchi wa kawaida waamini chama kipi kama hali yenyewe ndio hiyo?

Kwani mwanasiasa analazimishwa kuweka hadharani matatizo ya chama anachohama?

Nakumbuka mwaka 2011 wakati aliyekuwa mbunge wa Kishapu mkoani Shinyanga, Fred Mpendazoe alipotangaza kuhama CCM na kujiunga na chama kipya cha CCJ na kisha Chadema, waliibuka makada wakongwe wa CCM na kubeza hatua hiyo.

Miongoni mwao ni aliyekuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa ambaye alisema kuwa Mpendazoe hajaacha pengo hata kidogo na alishangaa BBC kutangaza habari za kuondoka kwa mtu huyo ndani ya CCM.

Akasema kuondoka kwa Mpendazoe ilikuwa ni sawa na kuchotwa kwa ndoo moja ya maji katika mto Rufiji halafu ukasema maji yamekwisha, na hiyo sio sahihi na kwamba CCM ina wanachama wengi, mashabiki na wakereketwa.

Kwa upande wake Yusuf Makamba akasema kuwa CCM ilikuwa na wengi wakiwamo akina (Augustino) Mrema, Seif Sharif Hamadi na Hamad Rashid, hivyo Mpendazoe si lolote.

“Ya Mungu apewe Mungu na ya Kaisari mpeni Kaisari jamani CCM ndio chama imara Tanzania na kitaendelea kushika hatamu,” akasema Makamba alipokuwa akizungumzia kuhama kwa Mpendazoe ambaye sasa amerejea CCM.

Wanasiasa hao walifikia hatua hiyo kufuatia maneno ya Mpendazoe ya kukirushia tuhuma mbalimbali chama hicho tawala zikiwamo za kudai kwamba CCM kutoa vyeo kwa upendeleo, lakini mwisho wa siku akarudi tena CCM.

Wakati wanasiasa wakihama vyama na kutoa lawama nyingi dhidi ya kule wanakotoka, wapambe, wakereketwa na wafurukutwa wa vyama vya siasa nao wako mstari wa mbele kutoa kila aina ya matusi kwa hao wanaohama.

Mfano mmojawapo ni kwa Nyalandu ambaye ametukanwa kila aina ya matusi kwenye mitandao ya kijamii na hata kutuhumiwa na kuhumikiwa kwa makosa mbalimbali badala ya kuachia vyombo vya dola kufanya kazi.

Sio Nyalandu tu hata Mwigamba naye alikaririwa na vyombo vya habari akilalamika kuwa baada ya kutangaza kujivua uongozi baadhi ya viongozi wa ndani ya chama waligeuka vichaa wakimtukana kila aina ya matusi.

Kimsingi siasa za aina hii hazina mashiko, hivyo ni vyema wapambe, wakereketwa na wafurukutwa wakaacha tabia hii, ambayo ni ishara kwamba hawajakomaa kisiasa.

Mwanasiasa kuhama kutoka upinzani kwenda CCM au kuhama CCM kwenda upinzani ni haki yake ya kidemokrasia, kwa hiyo hakuna sababu ya kumtukana kila aina ya matusi kama ambavyo wapambe, wakereketwa hao wamekuwa wakifanya.

Vilevile wanasiasa nao watambue kuwa sio vizuri kuhama vyama na kuanza kurusha tuhuma kule walikotoka, kwani ni hao hao ambao mwisho wa siku hurudi kwenye vyama hivyo hivyo walivyovihama kwa mbwembwe na matusi.

Habari Kubwa