Wanasiasa katika Jiji la Mbeya  walivyochuana mbele ya JPM

15May 2019
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Wanasiasa katika Jiji la Mbeya  walivyochuana mbele ya JPM

APRILI 26 mwaka huu, Rais John Magufuli, alifanya Mkutano wa Hadhara katika uwanja wa CCM, Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kihistoria katika Mkoa huo tangu alipochaguliwa kuongoza taifa  mwaka 2015.

Rais John Magufuli.

Mkutano huo ulipambwa na sare za vyama vya siasa hasa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho ndicho chama Kikuu cha Upinzani nchini.

Mbali na sare za vyama hivyo kupamba mkutano, lakini pia kulikuwa na vijembe na kejeli za chini chini kati ya wanachama, wafuasi na wakereketwa wa vyama hivyo viwili, ambapo wanachama wa CCM walikaa mbele na wa Chadema walisimama nyuma.

Wanachama wa Chadema walikuwa wanalalamika kutengwa kwenye mkutano huo ambapo Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alilisema suala hilo mbele ya Rais, akidai Wanachadema wamewekwa nyuma ili wasionekane.

Ukiacha mbwembwe hizo za wanachama wa vyama hivyo pamoja na vituko vingine vilivyokuwa vinaonekana kwenye mkutano huo, uliohudhuriwa pia na mawaziri na manaibu waziri kadhaa, wanasiasa wenye nguvu katika Jiji la Mbeya nao walionekana kuchuana.

Viongozi hao wenye nyadhifa tofauti za kitaifa, kila mmoja alikuwa anaonyesha kujifagilia binafsi na kuwasaidia wananchi kuwasilisha kero zao kwa Rais.

DK. TULIA

Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ndiye aliyekuwa wa kwanza kujimwaga jukwaani ambapo alianza kwa kumshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuwa mmoja wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha akachaguliwa kuwa Naibu Spika.

Alisema wananchi wa Jiji la Mbeya wanafurahia heshima waliyopewa na Rais Magufuli ya kumteua katika nafasi hiyo kwa madai kuwa baadhi ya wananchi hao yeye ni mtoto wao, dada yao, mama yao na baadhi ni shangazi yao.

“Mheshimiwa Rais, jana (Aprili 25) ulipokewa kwa kishindo na ulisimama maeneo mbalimbali kwa sababu wananchi hawa walitamani sana wakuone na wazungumze na wewe,” alisema na kuongeza:

“Hata hivyo kutokana na muda, wanafahamu wazi kuwa fursa inaweza ikawa ndogo… kwa sababu hiyo mimi kijana wao, dada yao na mtoto wao nitawasilisha salamu zao.”

Baada ya salamu hizo aliwasilisha changamoto za wananchi akianzia na za wananchi wa Kata ya Nzovwe ambao waliathirika kufuatia mafuriko yaliyotokea hivi karibuni kutokana na mvua zilizokuwa zikiendelea kunyesha.

Dk. Tulia alisema zaidi ya kaya 100 ziliathiriwa na mafuriko hayo na kwamba ameshafuatilia na kubaini kuwa kuna mipango ambayo Serikali inaendelea kuifanya ili kudhibiti sababu za mafuriko katika eneo hilo.

“Taarifa zilizopo ni kuwa itachukua miezi 18 kutengeneza mitaro ili maji yasiingie kwenye makazi,” anasema.

Mbali na taarifa hiyo, pia Dk. Tulia aliwasilisha kilio cha wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu ‘machinga’, akidai kuwa kundi hilo linakabiliwa na changamoto ya kukosa maeneo ya kufanyia biashara zao.

Alimuomba Rais Magufuli kuwasaidia wafanyabiashara hao kwa kuidhinisha eneo la Uwanja wa Ndege wa Zamani libadilishwe matumizi na kuwa la wafanyabiashara hao kufanyia shughuli zao.

“Nianze kwa kumpongeza Mkuu wa Mkoa (Albert Chalamila) kwa kazi anazofanya hapa jijini Mbeya na Mkoa mzima, lakini sisi machinga tumepata changamoto kidogo, tunaomba mheshimiwa Rais useme neno nasi tutapona,” alisema Dk. Tulia.

Aidha akasema, wananchi wa Jiji la Mbeya wanamshukuru Rais Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha sekta ya Afya, hasa katika vituo vya afya vya Kata za Nzovwe na Iyunga ambavyo kwa ujumla vilipatiwa zaidi ya Sh. Bilioni 1.1.

MBUNGE MBILINYI (SUGU)

Baada ya Dk. Tulia kumwaga sera zake aliyefuata alikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye alianza kwa kukumbushia tukio la kufungwa jela mwaka jana.

Akitumia lugha ya kisanii, Sugu alisema wakati akiwa gerezani alipata taarifa kuwa Rais Magufuli yuko Iringa na hivyo akawaza kuwa pengine akitoka huko angefanya ziara mkoani Mbeya na hivyo angemkosa.

“Niliposikia kuwa umeondoka na Mbeya utafanya ziara baadaye, nikasema inshallah ukija utanikuta na nashukuru umenikuta niko nje Mungu ni Mwema sana,” alisema.

Hata hivyo, wakati Sugu akitoa maelezo hayo wafuasi wa CCM walisikika wakisema ‘ulifungwa kwa matakwa yako…endelea hivyo hivyo.’

Baada ya kukumbushia masuala hayo Mbunge huyo alianza kuusaka umaarufu kwa kutaja changamoto zinazowakabili wananchi wa Jiji la Mbeya, akianza na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.

Alisema kwa mujibu wa taarifa alizozipata wakati anafuatilia katika mamlaka ya Maji ya jiji hilo ni kwamba ni asilimia 60 tu ya wananchi wa Jiji la hilo ndio wanaopata maji na asilimia zilizobakia hawapati kabisa.

Sugu alisema wataalamu walipofanya tathmini walikuja na suluhisho la kudumu kwa kutaka kuchukua maji kutoka chanzo cha Mto Kiwira ambalo lingemaliza changamoto hiyo katika Jiji hilo na maeneo ya jirani.

“Wataalamu walishafanya upembuzi yakinifu wa mradi ule na walisema zinahitajika Sh. bilioni 70… sasa nakuhakikishia endapo utawezesha mradi huo kukamilika, hakuna legacy (urithi) kubwa utakayokuwa umeacha kama hiyo kwa jiji letu,” anasema.

Alibainisha kwamba kwa mujibu wa wataalamu, endapo mradi huo utatekelezwa kuna uwezekano maji hayo yakapelekwa mpaka Mji wa Tunduma mkoani Songwe, umbali wa zaidi ya Kilomita 100 kutoka Mbeya Mjini.

Aidha, Sugu aliungana na Dk. Tulia kuwasemea wamachinga akisema hata yeye aliwahi kufanya biashara ya umachinga katika Soko la Mwanjelwa baada ya kuhitimu kidato cha nne kabla hajaingia kwenye mziki.

Mbunge huyo alibainisha kuwa wamachinga ni tofauti na wafanyabiashara wengine na hivyo hawatakiwi kuwekewa eneo maalumu la kuuzia biashara zao na badala yake wanatembeza biashara zao barabarani.

“Kwenye ‘ishu’ ya wamachinga nakuunga mkono kwa asilimia 100 mheshimiwa Rais, kama ulivyosema jana barabara tumejenga wenyewe na wewe ulikuwa Waziri wa Ujenzi… ulisimamia vizuri na ukasema wamachinga wako huru… machinga si wa kuwekewa eneo maalumu,” alisema.

Alisisitiza kuwa kwenye miji iliyoendelea duniani kama New York Marekani, Beijing China, Tokyo Japan na miji mingine iliyoendelea machinga wanatembeza bidhaa zao barabarani na kwamba kinachotakiwa ni kuwekewa utaratibu mzuri.

Vilevile alimuomba Rais Magufuli kuwezesha upanuzi wa barabara Kuu ya Tanzania na Zambia (Tanzam), katikati ya Jiji la Mbeya na kufanywa kuwa yenye njia nne.

Alimsisitizia Rais kuwa wananchi wa Jiji la Mbeya wanamkubali tofauti na taarifa ambazo zimekuwa zikizushwa kuwa kuna mgawanyiko wa kisiasa na akaomba yeye atumike kuandaa majadiliano ya kisiasa kuondoa mafundo fundo hayo ya kisiasa.

DK. MARY MWANJELWA

Baada ya Mbunge Mbilinyi mtaalamu wa muziki wa ‘Hip Hop’ kujimwaga, alifuata Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Mbeya (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa ambaye alianza kwa kumwaga sera zake mithiri ya mhubiri.

Mwanjelwa alimumwagia sifa mbalimbali Rais Magufuli kuwa ni Rais wa wanyonge, kipenzi cha Watanzania na akamshukuru kwa kufanya ziara katika Mkoa wa Mbeya kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa mwaka 2015.

Kama ilivyokuwa kwa Naibu Spika, pia alimshukuru kwa kumteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa madai kuwa uteuzi huo ni heshima kwa wana Mbeya.

“Mtunosisye bha kukaja, Mheshimiwa Rais tunakushukuru kwa heshima uliyotupa wana-Mbeya, kwanza kwa kufanya ziara ya siku nane ambapo utapita katika wilaya zote… ulipokuwa unaingia ulipokewa na umati mkubwa akiwamo mbunge wa Jimbo hili na madiwani wote,” alisema Dk. Mwanjelwa.

Baada ya kumwaga sifa hizo alimuomba Rais Magufuli kuharakisha mradi wa upanuzi wa barabara katikati ya Jiji la Mbeya ili kupunguza msongamano wa magari.

Vilevile aliomba mradi wa ujenzi wa barabara ya mchepuko kwa ajili ya magari ya mizigo kutoka Uyole mpaka Songwe uharakishwe ili kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

CHALAMILA ANG’AKA

Kabla ya Kumkaribisha Rais Magufuli kuhutubia umati wa wananchi waliokuwa wamehudhuria Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa Albert Chalamila, alizungumzia masuala mbalimbali.

Chalamila alitoa takwimu za miradi mbalimbali pamoja na fedha zilizotumika kuitekeleza, ikiwamo miradi ya barabara, elimu na afya ambapo alisema serikali imetoa fedha nyingi.

Alikumbushia ufisadi uliofanywa na baadhi ya watendaji wa Soko la Kimataifa la Mwanjelwa ambalo alidai kuwa ni miongoni mwa masoko katika Afrika Mashariki na Kati ambayo yalijengwa kwa ufisadi mkubwa.

Aliwataka wafanyabiashara wa Jiji la Mbeya kuendelea kuitumia fursa ya soko hilo licha ya ufisadi uliofanyika na waache kutaka kupanga bidhaa zao chini kuzunguka soko hilo.

“Unapoamua kujenga choo kizuri ndani basi ubaki humo humo ndani, lakini ukianza tena kwenda kwenye migomba watu watakuona kama mchawi… soko lile lilijengwa kwa Sh. Bilioni 19.5 lakini hiyo si sababu ya watu kulikimbia,” alisema Chalamila.

Hata hivyo, alionyesha kumkuna zaidi Rais Magufuli alipotoa takwimu za ukusanyaji wa mapato katika Jiji la Mbeya ambapo alisema makusanyo yamepanda kwa kiasi kikubwa.

Alisema kabla hajateuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Jiji la Mbeya lilikuwa linakusanya Sh. milioni nane mpaka 10 kwa mwezi, lakini baada ya kuingia yeye na kudhibiti mianya ya upotevu soko hilo linaingiza milioni 40 mpaka milioni 42 kwa mwezi.

Aidha, alisema katika Soko la Sido vilijengwa vibanda zaidi ya 900 baada ya Soko la Mwanjelwa kuungua mwaka 2007 na kwamba wafanyabiashara hao walikuwa hawalipi kodi na kwamba wakihojiwa wanadai wao ni wahanga.

“Nilisema huo uhanga una mwisho wake na mpaka sasa ninapozungumza kodi iliyokwishawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Jiji ni milioni 422, lakini kodi ambayo imekusanywa na TRA, wakiwa hawajawahi kukusanya huko nyuma ni Sh. milioni 687,” anasema.

JPM ANENA

Baada ya Chalamila kumaliza kujimwaga alimkaribisha Rais Magufuli awahutubie wananchi ambapo mbali na mambo mengine alianza kwa kuwahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuwa hawezi kumuondoa Chalamila katika Mkoa huo.

Alisema kiongozi huyo anafanya kazi nzuri na wote wanaompiga vita wamekwama na akamtaka aendelee kuchapa kazi ya kuunyosha mkoa huo kama alivyokuwa ameomba mwenyewe awali.

Vilevile aliwashukuru wananchi mkoani humo kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (Sia) mpaka alipoingia mjini wakiongozwa na viongozi mbalimbali akiwemo mbunge Sugu pamoja na madiwani wa upinzani.

Alimtania Sugu kuwa anaonekana ni mpinzani kwa sura lakini moyoni ni CCM na kwamba ndio maana alishiriki mapokezi na kumsindikiza mpaka Ikulu ndogo.

Hata hivyo, alikata kiu ya wamachinga kwa kuidhinisha eneo la Uwanja wa ndege wa zamani ambalo waliombewa na viongozi litumike kwa ajili ya wamachinga na akaagiza miundombinu muhimu iwekwe na Serikali, tamko ambalo linasababisha shangwe kulipuka uwanjani hapo.

Habari Kubwa