Wanaume hunyanyaswa kuitwa ‘mwanaume suruali ni GBV’

07Dec 2019
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Wanaume hunyanyaswa kuitwa ‘mwanaume suruali ni GBV’

SIKU 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ambayo ni kampeni ya dunia ya kuwalinda wanyonge hasa wanawake, watoto, wahitaji na wengine ili wasionewe, inakumbusha watu kujiepusha na ukatili na unyanyasaji kijinsia (GBV).

Mwanamume akipata kichapo mtaani. Kinababa watasema hawapigwi na GBV haiwahusu? PICHA: MTANDAO

Kampeni hiyo ya GBV –Gender Based Violence iliyoanza tangu wiki iliyopita na inayotarajiwa kufikia kilele Jumanne ijayo Desemba 10, mara nyingi wanaume wanaipuuza na kudhani kuwa wanaonyanyasika ni wanawake na kwamba wao mambo hayo hayawahusu.

Kwa ujumla unyanyasaji wa kijinsia unawaumiza wote. Kila mmoja kwenye jamii anaumia bila kujali jinsi yake iwapo ni mwanamume au mwanamke, japo ukatili unaohusisha kubakwa, kulawitiwa, kunajisi watoto, kutukanwa, kupigwa, kukeketwa, mimba na ndoa za utotoni, kupigwa na wenza katika ndoa, kulazimishwa kuacha kazi na pia kutelekezwa kunawaumiza zaidi wanawake kuliko wanaume.

Hii ni kwa sababu wanawake ndiyo wanaobeba mzigo mkubwa wa majukumu ya kifamilia na ukatili unapotokea unakuwa ni dhamana ya mama kuupokea na kushughulikia mateso hayo.

Mathalani, binti akibakwa mama anahangaika naye kuanzia kumfikisha polisi, hospitalini, kumtibu kama ameambukizwa maradhi, kumlea na mtoto iwapo amepata ujauzito na mwisho kumsaidia kwa kila hali ili apate mtoto na kuendeleza maisha.

Wakati huo baba anaweza kuwatukana mama na binti kwa matusi ya nguoni na kashfa dhidi ya tukio hilo na vyote hivyo ni unyanyasaji.

WANAUME WAHUSIKE.

Mara nyingi kwenye harakati za siku 16 za kupinga ukatili, wanaume hawapendi kuhusika moja kwa moja. Wapo wengine wanasema hawanyanyasiki lakini ukweli ni kwamba hata wao wamo.

Kwa mfano, wiki hii wakati Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, anapozungumzia Siku 16 za kupinga unyanyasaji, anawakumbusha wanaume kuwa hata wao ni waathirika watumie madawati ya jinsia kueleza kinachowasibu.

“Nanyi wanaume mlio katika uhusiano ikitokea mmefanyiwa ukatili na mwenza wenu msisite kutoa taarifa,” anawahimiza Mambosasa.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, anawataka wanaume kujitokeza kwani hata wao kampeni hizo zinawahusu na wanaumizwa na GBV kwa kiwango kikubwa.

Anawaambia kuwa wanaume wanapigwa, kutukanwa na kunyanyaswa na wanawake wao, lakini wanakaa kimya na mwisho hukimbia familia na kuwaacha watoto wakiathirika zaidi.

“Kama mtaogopa kwenda kwenye madawati ya jinsia polisi kwa kuwa mnaogopa wanaosikiliza malalamiko hayo ni wanawake njooni hata kwetu sisi viongozi,” anasema Msafiri.

Pia, Mwakilishi wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam, Faiza Suleiman, anapozungumzia suala la ukatili wa kijinsia anasema ingawa jamii inaamini kwamba ukatili wanafanyiwa wanawake , wanaume nao ni waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili, lakini wamekuwa wakijificha.

"Tatizo ni mfumo dume kwamba mwanamume hawezi kupigwa au kunyafiwa ukatili na mwanamke, lakini ukweli ni kwamba wapo tena wengi. Ushauri wangu ni kwamba wanaume hebu fungukeni," anasema Suleiman.

Pamoja na ushauri wa viongozi hao, ni vyema jamii kufahamu kuwa unyanyasaji wa wanaume unafanywa kwa njia nyingi, lakini hata kwa maneno na mara nyingi kuwasema , kuwalaumu muda wote na kuwa na gubu lisilokwisha ndani ya nyumba ni GBV.

Wapo baadhi ya wanawake wanawaambia waume au wapenzi wao wewe ni mwanamume suruali’. Maneno kama hayo ni unyanyasaji kijinsia na husababisha wanaume wengine kujinyonga au kukimbia familia zao.

Kumwambia mwanamume tena mbele za watu au watoto kuwa wewe huna kitu ni au kumkejeli mwenza kuwa ni ‘mwanamume jina’ni kuwaumiza wanaume kisaikolojia na kimwili.

Maneno kama mume bwege ,mume kivuli,’ ‘wanaume wakiitwa utakwenda’ni matusi ambayo hata wanaume hayawafurahishi kwa namna yoyote.

KUSIFIWA KUNYANYASA

Kuna baadhi ya jamii ambazo wanawake husifika katika kunyanyasa wanaume. Hili si jambo la kufurahisha kuwa ‘ninyi’watu fulani ni mabingwa wa matusi, kusuta na kudhalilisha wanaume, kumbukeni kuwa huo ni unyanyasaji na udhalilishaji na wiki hii mnakumbushwa kuuacha.

Jamii ikumbuke kuwa hakuna anayefurahia kufokewa muda wote, kuhojiwa na hata kupuuzwa kila anapofika nyumbani kwake.
Kwa mfano wapo kinamama ambao muda wote kama atapiga simu kwa mwenza na akachelewa kuipokea au asiipokee anaanzisha ugomvi.

Maswali kama mbona hupokei simu yangu lakini ya nyumba ndogo huchelewi kuipokea ndiyo anayokutana nayo baba watoto wako.
Wapo pia baadhi ya wanawake wanapenda kupekua simu za waume zao na kuwauliza mbona hii namba unaipiga sana kuna nini? Au ni nina mwenzangu?

Kuna maneno mengine matusi ambayo huambatana na wanaume wenye kipato kidogo ni pamoja na kukutana na kauli za kuudhi muda wote.

Wakifika nyumbani wanaanza kusalimiwa na maneno ya kashfa kama ‘mwanamume pesa’au ‘kama mtu huna nyumba, gari wala mali ni kama umekufa.’

WATOTO HUTUMIKA.

Baadhi ya wanaume katika soko la Tandale, jijini Dar es Salaam, wanaozungumza na Nipashe kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wanasema wanawake huwatumia watoto kuwatukana baba zao (waume wao) pale wanapoona kuwa hawana kitu,
“Kwa ukali mama anasema nyie mnanililia mnataka chakula kamwambieni baba yenu muulizeni kwanini hana hela . " Nani kamwambia awe maskini’ anasema Albogasti Mushi, anayeuza matunda katika soko hilo.

Mushi anasema wakati mwingine mwanamume anaondoka au anarudi usiku wa manane na kuondoka mapema kwenda kijiweni ili awe na amani.

“Tunatukanwa na watoto na mama zao ndiyo maana tunaamua kuondoka na kuwaambia watakula matusi yao. Tutafanya nini sasa. Lakini ukiondoka mwanamke anakugeuzia kibao kuwa unamnyanyasa na umeitelekeza familia na watoto”anasema Mushi.

Kwa hiyo ni vyema kufunguka na kueleza matatizo ili kupata ushauri nasaha lakini pia jamii ijue kuwa unyanyasaji unamhusu kila mtu.

Habari Kubwa