Wanawake vinara kuacha waume uzeeni

13Jan 2019
Flora Wingia
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wanawake vinara kuacha waume uzeeni

MPENZI msomaji, tunaendelea na sehemu ya pili ya makala yetu iliyoanza wiki iliyopita ikibeba kichwa cha maneno kinachouliza; Kwanini wanandoa waachane uzeeni?

Leo nizame zaidi; Je, nani vinara katika eneo hilo, wanawake au wanaume na kwanini?

Mengi nilieleza wiki iliyopita hasa tafsiri ya ndoa nikijaribu kuonyesha kuwa ndoa ni muungano kati ya mume na mke unaowafanya kuwa mwili mmoja. Pia nikasema kuwa ndoa ni muunganiko wa mwanaume na mwanamke kuishi pamoja kama mume na mke muda wote wa maisha yao.

Na hii ipo hata katika ahadi ya ndoa ya kidini madhabahuni au ya kiserikali pale wawili walioamua kuunganisha koo kufunga ndoa. Miongoni mwa maneno ambayo yamo kwenye ahadi ni pamoja na, ”… nitakupenda siku zote za maisha yangu, kwa shida na raha hadi kifo kitutenganishe…”.

Sasa mtu aweza kujiuliza; je, ahadi hii inatekelezwa kweli? Mbona ndoa zinavunjika, tena wakati mwingine kwa mambo ambayo hayana mashiko? Na kibaya zaidi zinavunjika uzeeni.

Nilikuwa natafuta vyanzo au sababu za wanandoa kuachana uzeeni nikagundua mambo ya ajabu sana. Wapo watu waliotengana lakini hawajaachana ila kila mmoja anaishi kivyake.

Pia wapo waliotengana lakini wako kwenye mchakato wa kupeana talaka ili kila mmoja ahangaike kivyake japokuwa ni wazee. Yaani badala ya watu kutimiza ile ahadi ya kuishi kwa shida na raha hadi kifo kiwatenganishe, wao wanaivunja ahadi hiyo uzeeni.

Jambo linalotia mshangao ni sababu zinazotajwa kuwa chanzo cha kutengana au kuachana. Busara zaidi zingetumika kwamba maadam haya yameshatokea, basi wasameheane ili uzee wao uwe na kheri.

Kama Mungu anatufutia dhambi wala hazikumbuki, kwanini nasi tusisameheane? Isaya 43:25 anasema, “Mimi, naam, mimi ndimi niyafutaye makosa kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako’. Lingine; Wakolosai 3: 13 “mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi”.

Wapo baadhi ya wanandoa ambao sasa ni wazee, wameshapata wajukuu lakini wako katika hatua za kuachana na wengine tayari wameachana kabisa. Na wanaong’ang’ania kuachwa ni wanawake huku wakiwa na sababu zao.

Moja ya sababu inayotajwa ni eti mume kafilisika, uchumi umeanguka hivyo mwanamke akatafuta mazingira ya kujinyanyua kiuchumi na kumuacha mumewe njiapanda.

Sasa kama mume amekwama kiuchumi, kwanini mama asimsaidie waendelee kushikamana kwa shida na raha hadi kifo kama ahadi ya ndoa waliyoapa kuitimiza inavyotaka?

Yupo jamaa yangu mmoja ambaye mkewe alimtelekeza baada ya kuanguka kiuchumi. Mama akatimkia zake ulaya kwa mwanaye anayefanya kazi huko. Nyumbani alibakia baba na kijana wao mkubwa.

Mama huyu baada ya kuona maisha ulaya safi, akaanza mchakato wa kudai talaka uzeeni. Kijana huyu mkubwa alipofikia kuoa, ilibidi mama aje toka ulaya kwa harusi hiyo.

Mpenzi msomaji, hebu pata picha, baba na mama wako harusini wanalishana keki kwa heshima ya maharusi lakini moyoni kila mmoja anawaza yake. Halafu wote ni watu wazima sana kimuokekano wanapendezeana lakini katika roho hawapo pamoja.

Wanandoa wengine niliowahi kupata habari zao ni kwamba ilitokea baba aliteleza akazaa mtoto nje ya ndoa. Mkewe alipojua akaudhika akadai talaka. Lakini hawa nao ni wazee sana hata kwenye utumishi wa umma walishastaafu.

Mama huyu naye yuko ulaya kwa wanawe na alipojua jambo hilo na kumuuliza mumewe alikiri na ndio ukawa mwisho wa ndoa yao. Mwanaume hakuwa na jinsi ikabidi atoe talaka wakaachana kwa namna hiyo.

Mwingine nilisimuliwa hivi majuzi baada ya mwanaume kufariki dunia. Ni familia iliyokuwa na uwezo mkubwa kiuchumi lakini ukatokea mtafaruku ambao hawekwi wazi, wengine wakidai ni ugonjwa wengine uchumi kuanguka. Mama naye akatimkia ulaya.

Mwanaume akaamua kuishi kwenye jumba lao la kifahari mwenyewe bila msaada wowote. Akawa mdhoofu kwa mawazo na kutopata msaada, ikatokea jamaa yake mmoja alimkubuka akamtembelea.

Cha ajabu akamkuta katika hali mbaya ikabidi amkimbize hospitalini. Kumbe alikuwa hapati chakula ipasavyo. Wanaomfahamu mkewe wakamtafuta kwenye mitandao, akajulishwa hali mbaya ya mumewe.

Mwanamke huyo akaandaa safari kuja nyumbani, akaweza kufika lakini hali ya mumewe ilikuwa mbaya kwani alifariki siku mbili baada ya kuwasili kwake. Ama kweli maisha ndivyo yalivyo.

Mpenzi msomaji, angalia mifano hiyo niliyotoa, yote ilihitaji kinamama hao wawe na busara wajifunze kusamehe kwani duniani hapa sote tunapita. Wanaume hawa wamedhoofu kimaisha kwa kukosa ulinzi wa wake zao. Yeremia 31:22 …”Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume”.

Siyo ajabu hata wanaume hawa walitetereka kutokana na kukosa ulinzi toka kwa wake zao. Huo ndio ukweli!

Je, unalo suala la kifamilia/ndoa/mahusiano linalokutatiza? Wasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]

Habari Kubwa