Wapumua baada kuhamishia shambani pesa za Tasaf

26Feb 2016
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Wapumua baada kuhamishia shambani pesa za Tasaf

MAISHA ya wakazi wengi hasa waishio vijijini hutegemea zaidi kilimo. Lakini kutokana na hali ngumu ya kiuchumi wengi wamekuwa wakishindwa kulima kisasa kwa lengo la kujipatia kipato. Badala yake wanaishia kulima kilimo cha ‘kuganga njaa.’

Kutokana na changamoto ya ukosefu wa mitaji ya kununulia pembejeo za kilimo zikiwamo dawa na mbegu bora, kuna wananchi masikini wenye ardhi ambayo ingewasaidia kuongeza uchumi wao.

Baadhi ya wakulima wa Bukoba wameamua kubadilisha matuimizi ya fedha za kutumia kukimu umasikini wao walizopewa na Mfuko wa Tasaf, kwa kuzihamishia katika kufadhili kilimo, ili wainuke zaidi kimaisha.

Kwa kawaida, ufadhili wa Tasaf hutoa ufadhili wake kwa kaya masikini sana ili kupata fedha za matumizi ya maisha ya kawaida.

MAFANIKIO YA WANUFAIKA

Gertrude Gasper ni mkazi wa kijiji Kiziru Kata ya Karabagaine, Bukoba vijijini. Yeye ni mnufaika wa ruzuku zinazotolewa na Tasaf III na anasema alipopewa fedha hizo, alizitumia kulima nyanya na akanufaika kupata faida mara tatu ya kiasi alichopewa.

“Baada ya kupata fedha za Tasaf, nilikwenda gulioni kuwanunulia watoto wangu wanne viatu vya shule.

“Nilipofika nikaambiwa bei ya mwisho kila jozi moja ya viatu ni Shilingi 15,000. Nikaona hata hela niliyo nayo haitoshi kuwanunulia wote nilirudi nyumbani nalia,” anasema.

Mama huyo anasema baada ya kurudi nyumbani alipata ushauri kuwa fedha hizo Shilingi 56,000 asizitumie tena na badala yake alizitumia kuanzisha kilimo cha nyanya.

Getrude anasema kiasi hicho aliingiza shambani kwa kupanda miche ya nyanya zaidi ya 1,000.

“Nilizitumia kulima nyanya kwa kununua mbegu na dawa na Mungu akasaidia zikastawi vizuri. Nilipoanza kuvuna, nilianza kuuza kilo moja kwa Shilingi 1,500.

“Lakini baadaye bei ilipanda nikauza kwa Shilingi 2,000. Fedha nilizozipata zilinisaidia kununua mahitaji ya watoto ya shule,” anasema Getrude.

Ni mafaniko anayojigamba sasa yamewezesha kurekebisha nyumba yake na mumewe ambaye ni mshirika wake katika kilimo. Nyumba ilikuwa inavuja na haikuwa na madirisha.

Mnufaika mwingine wa mradi wa Tasaf, ni Edina Balilemwa, ambaye pia ni mkazi wa kijiji anachoishi Getrude, anasema kabla ya kupewa fedha hizo, hali yake illikuwa mbaya sana na alikuwa na madeni lukuki.

“Mara ya kwanza nilipata Shilingi 44,000, nikatoa shilingi 10,000 nikapunguza deni. Kuna mtu alikuwa ananidai fedha nyingi, kiasi kilichobaki nilikitumia kuanzisha kilimo cha mchicha ambao niliuza na kupata faida zaidi ya kiasi nilichopewa,” anasema Edina.

Anasema, sasa amelima shamba la nyanya chungu lenye miche zaidi ya 1,000 na anongeza kuwa:“Tasaf imenisaidia sana, kwa kweli siwezi kuacha wanaosema fedha zinazotolewa na Tasaf ni kidogo hawajui namna ya kuzitumia,” anasema.

“Fedha zote ninazozipata kutoka Tasaf nitaziwekeza katika kilimo maana nikivuna napata faida kubwa, ambayo itanisaidia kutunza familia yangu baada ya kutengana na mume wangu, naishi mwenyewe na nina watoto watatu” anasema Edina.

Usemi “umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu” umewafanya baadhi ya wanufaika wa Tasaf katika kijiji cha Kiziru kuunda kikundi cha watu sita, ambacho baada ya kupata fedha za mpango huo wanafanya shughuli za kilimo kwa pamoja.

Elias Mushema ni mwanakamati wa Tasaf katika kijiji Kiziru, anayesema aliona muhimu kuunda kikundi cha kuwawezesha kunufaika zaidi kijijini kwao.

“Nililazimika kuwashawishi na kufanikiwa kuwaunganisha, tunafanya kazi ya kulima mazao mbalimbali ikiwamo nyanya, pilipili hoho, nyanya chungu, mchicha, maharage na mihogo, wengi wamekwishanufaika maana mazao tunayolima yanakomaa katika muda mfupi,” anasema.

Mushema anasema, walijiwekea utaratibu wa kikundi chao wanakutana ila Jumatatu na Jumanne asubuhi na jioni kwa utaratibu maalum.

“Tunapokwenda kwa mtu hakuna ulazima wa kutuandalia chakula. Mhusika hupaswa kuandaa maji ya kunywa tu kwa mwenye uwezo kidogo anaweza kutuandalia chai na mihogo, tukishashika jembe hatutoki shambani hadi jioni,” anasema.

“Hizi siku mbili kwa wiki tunazopumzika za Jumatano na Jumamosi, wana kikundi waliolimiwa hutakiwa kuzitumia kufanya marekebisho kidogo katika mashamba yao ikiwamo kuchoma moto majani au magugu na kwenda kuwasalimia ndugu na jamaa” anasema.

“Pesa ya Tasaf sio ndogo kama wengine wanavyosema. Ina uwezo wa kumuinua Mtanzania kimapato. Wanaosema ndogo wanahitaji elimu bado ya namna ya kunufaika nayo, kwa sababu pesa kubwa huanza na ndogo. Kinachotakiwa ni mipango mizuri ya kuitumia na kuifanya kuwa mtaji endelevu,” anasema.

Kuhusu wana kikundi wasio na ardhi, anasema huchukua hatua ya kukodi ardhi ambayo hawaitumii.

Audax Zacharia ni mnufaika kutoka kijiji Minazi Kata ya Bujugo, anayesema kuwa fedha aliyoipata kwa awamu ya kwanza, Sh. 36,000, aliongezea na kununua nguruwe mmoja kwa Sh. 45,000 kwa ajili ya kufuga.

“Pesa nyingine nilizopata nilinunua mbolea ya chumvi chumvi, maana huwa napenda sana kilimo cha bustani. Naona ndicho kitakachoniongezea kipato badala ya kufanya biashara nyingine,” anasema.

Zacharia anatoa mfano, aliwekeza Sh. 36,000 kwenye kilimo cha nyanya chungu na ndani ya miezi mitatu hadi mine, inapatikana wastani wa Sh. 150,000, mtaji unaoweza kumsaidia kusonga mbele.

Ismail Hamidu ni Mratibu wa Tasaf III Bukoba vijijini, anasema baada ya kuwatembelea walengwa, anakiri malengo ya mpango huo yanaelekea kutimia, maana lengo la Tasaf ni kuziinua kaya maskini ili ziongeze kipato na lishe na watoto kunufaika nayo kwa mahitaji kama ya shule.

Hamidu anasema, wananchi hawawezi kujiinua kiuchumi kama hawana afya njema na kuwa ndiyo maana wanawahamasisha walengwa wote kutumia sehemu ya ruzuku wanayoipata kujiunga na bima ya afya.

Anasema hivi kuna sasa walengwa 5,700 kutoka kaya maskini zinazopata ruzuku kupitia mpango huo wamejiunga na CHF, ili kuepuka kukosa kupata matibabu kutokana na kutokuwa na kipato.

Mratibu huyo anasema kuwa kaya 230 zimeondolewa katika orodha ya wanufaika, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo udanganyifu uliofanyika wakati wa uandikishaji na ulevi.

Kwa mujibu wa mratibu huyo, kaya ambazo zimegawiwa fedha kwa awamu ya Januari hadi Februari mwaka huu ni 8,487.

Habari Kubwa