Warudia kilimo kahawa baada ya nyanya na kabichi kuwatelekeza

06Dec 2019
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Warudia kilimo kahawa baada ya nyanya na kabichi kuwatelekeza
  • Waliacha kwa mbwembwe za kung’oa miche
  • Wapiga ‘magoti’ na kurejeshwa kundini

ZAO la Kahawa limekuwa juu katika kuongoza kwa kipato na kuleta maendeleo ya haraka kwa jamii ya wakulima.

Nyanya wilayani Mvomero, zao lililowafanya wakulima kuacha kahawa, lakini wamierudia tena kahawa, baada ya nyanya hizo kukosa soko.

Hapo unataja maeneo kama mkoa Kilimanjaro na Kagera. Pia, kuna wilaya za Mbinga, Ruvuma na Rungwe mkoani Mbeya, kwa kiasi kidogo tarafa za Mgeta wilayani Mvomero, mkoa Morogoro.

Mgeta kunalimwa kahawa tangu miaka ya 1970, na kukaibadilisha maisha ya wananchi wakapata maendeleo ya haraka, lakini ghafla ilikufa katika miaka ya 2,000 wakulima wengi kukimbilia kilimo cha nyanya, matunda na kabichi.

Inadaiwa, wakulima wengi walirubuniwa na vijana waliowahadaa kahawa inawachelewesha kujikwamua kimaisha, kwa kusubiri muda mrefu kupata fedha zake, wakakubali na kuanza kung’oa miti ya kahawa shambani.

WAKULIMA WAELEZA

Anatheti Kambaya, ni mkazi wa tarafa ya Mgeta, anasimulia miaka ya nyuma kahawa lilikuwa maarufu na wasomi wengi walienda shule kwa ada za kahawa, kwa sababu kuu uhakika wa soko na kuwa na bei nzuri, ikilinganishwa na mazao mengine kama mahindi mtama,mpunga na mbogamboga.

“Zamani Tarafa ya Mgeta ilikuwa chini ya Halmshauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini, kabla ya kugawanya kuwa chini ya wilaya ya Mvomero” anasema Anatheti na kuongeza:

“Hivi sasa sisi wakazi wa tarafa ya Mgeta ndio tulikuwa tunachangia mapato makubwa kutokana na kahawa, pia ndio eneo la kwanza kujengwa nyumba bora na kutoa wasomi ukilinganisha na maeneo mengine ya wilaya kutokana na zao hili,”

“ Huku Mgeta hali ya hewa yake ni kama Kilimanjaro, hivyo zao letu kuu lililotutoa lilikuwa kahawa, watu wamesoma huku na kupata maendeleo kwa ajili ya kahawa lakini miaka ya 2000 lililopoingia zao la nyanya tu, vijana wenye tamaa wakaanza kung’oa miti yake ili kupanda nyanya na kabichi,” anafafanua.

Abdul Kalindo, ni mkulima wa kahawa katika miaka 1970, anayesema: “Mimi binafsi unavyoniona hapa niliweza kusomesha watoto wangu mpaka chuo kikuu na leo wana kazi nzuri wananitunza.

“Kwa kuwa kipindi kile nilikuwa nalima kahawa na napata pesa nyingi.Mimi ni mmoja wa watu hapa Mgeta niliyojenga nyuma bora, wakati huo na imedumu mpaka sasa hivi hii yote ilikuwa ni kahawa.”

Anataja ushawishi wa vijana baada ya kuona wenzao katika maeneo ya vijiji vingine kama Mlali na Doma, katika barabara kuu ya Morogoro –Mikum, kuelekea Iringa kulima nyanya.

Mkulima Albert Senga, anasema baada ya kuingia kilimo cha nyanya, kabichi na matunda, walikuwamo katika walioshawishiwa kung’oa miti ya kahawa na kuanza kupanda mazao mengine.

Anakiri sura ya pili, nyanya na kabichi ziliwapatia fedha za haraka kutokana na soko kubwa, wateja wao wengi walitoka mikoa kama Dar es Salaam na Dodoma.

“Soko la Dodoma lilianza kupotea kwa kuwa vijiji vilivyopo barabara kuu ya Dodoma – Morogoro eneo la Dumila, nao wanalima nyanya na barabara vijiji vya barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro na wanalima nyama. Sasa tumejikuta hatuna soko na wakati mwingine tunalazimika kuzitupa nyanya au kuwapa mifugo,” anaeleza.

WARUDIA KAHAWA.

Kutokana na hiko, wakulima wa Mgeta, sasa wameanza kufufua tena kilimo cha kahawa, ikiwa ndio zao pekee la biashara kama ilivyokuwa huko nyuma.

Ni uamuzi uliohamasishwa na Taasisi ya Utafiti wa kahawa nchini (TacRi) kwa kushirikina na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tanzania (CDTF), zilizotoa mbegu, mafunzo na vifaa vya kilimo kwa vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha.

Mwenyekiti wa kikundi cha ujasiriamali wa kilimo cha Tugendelele, Stephen Msimbe, anasema baada ya kupatiwa mbegu na vifaa, tayari wameshazalisha vitalu vyenye miche 60,000.

Anasema miche hiyo ya kahawa wataigawanya kwa wakulima wa tarafa ya Mgeta, wapande shambani na mingine kugaiwa katika taasisi mbalimbali za serikali kama shule za msingi na sekondari, ili waipande katika mashamba yao.

Msimbe anataja matatizo yao kwa sasa ni kuikosa mbolea ya ruzuku na mashine za kisasa za kukoboa kahawa, kukausha ,kupukucha na kuziweka katika madaraja.

Anaiomba serikali, iwasaidie nyavu za kutunzia vitalu vya miche ya kahawa, maturubai na kuwaongezea watalaamu wa kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa.

Ni kauli inayoungwa mkono na Diwani wa Kata ya Bunduki, Prosper Mkunule, anayesema tayari wameshapanda miche 30,000 aina za Arabica na Robusta, katika mashamba ya kata hizo mbili, ikiwa ni mkakati wa kufanya zao hilo kuwa la biashara.

Anasema, kuwa kabla ya kupanda miche hiyo, taasisi ya CDTF iliwapelekea watalaam wa kilimo na kuvifundisha vikundi 35 kutoka kata za Bunduki na Mgeta, walime kwa kuzingatia kanuni bora shambani.

Diwani, anasema kilimo hicho cha kahawa kilikuwa kikisaidia kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji katika tarafa nzima ya Mgeta akini uharibifu na mabadiliko ya tabianchi wameamua kukirudisha tena.

MGETA YASAIDIWA

Mkurugenzi wa CDTF, Henry Mgingi, amesema Taasisi hiyo yenye makao makuu jijini Dar es Salaam, imekuwa ikisaidia tarafa ya Mgeta katika kilimo na mwaka elimu na mpango mkakati uliopo ni kurudisha kilimo cha kahawa kuwa mkombozi wa wananchi kibiashara.

“ Sisi Kama CDTF tumeona wananchi wa Tarafa ya Mgeta kutokana na hali yao ya hewa wanaweza kuendelea tena na kulima zao la kahawa ambalo bado lina umuhimu hapa nchini kutokana na kuwa na soko la uhakika, tofauti na zao la nyanya na kabichi ambao wateja wake ni wa kubembeleza,” anasema.

Anasema baada ya kupanda vitalu vya miche hiyo ya kahawa CDTF ilimua sasa kugharamia mafunzo kwa vikundi 35 vya kata ya mgeta na bunduki ili kujua mbinu za kilimo hicho na shughuli za ujasiliamali zilizotolewa na watalaamu mbalimbali kwa gharama ya Sh. milioni sita.

Mgingi anasema malengo yao ni kuhakikisha wakulima wa tarafa ya Mgeta wanafanya kilimo endelevu cha kutunza mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji, pia kupunguza kasi ya uchomaji moto unaosababisha uharibifu wa mazingira.

Mwenyekiti wa Bodi ya CDTF, Leon Msimbe, anasema: “Hivi sasa nchi inakwenda katika uchumi wa viwanda na mahitaji makubwa ni malighafi zinazotokana na kilimo, ikiwamo hili zao la kahawa ambalo lina soko kubwa ndani na nje ya nchi sasa.

“Sisi kama CDTF tumeona tukirudishe tena kilimo hiki cha zao la kahawa katika Tarafa ya Mgeta ili kuunga mkono jitihada za Serikali.”

Mhandisi Msimbe, anavitaka vikundi kutumia kilimo kurejesha hali ya zamani, iliyochafuliwa na kuathiri mazingira, ikiwamo Mto Mgeta ambao ndio sehemu ya Mto Ruvu.

MIKAKATI TaCRI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI), Dk. Deusdedit Kilambo, anataja mkakati wake kuendeleza zao hilo, tayari wameainisha maeneo mapya ya kupanda, akiitaja ni Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi na maeneo ya milima ya Uluguru, iliyopo wilaya Mvomero wakibaini yana uwezo mkubwa kuzalisha zao hilo.

Mkurugenzi huyo anasema kuwa katika Wilaya ya Tanganyika, baada ya kufanyiwa utafiti wameanza uzalishaji wa miche bora ya kahawa, kazi inayofanyiwa na TaCRI.

Dk. Kilambo anasema, hivi sasa wana aina mpya za kahawa 23 watakazozipanda katika maeneo mapya na zamani.

“Tulifanya utafiti nchi nzima na maeneo mengine ni mapya hayajalimwa, mikoa inayolima kahawa ni Kilimanjaro, Mbeya, Ruvuma na Kagera,” anasema Kilambo.

Waziri wa Kilimo, Jafeth Hasunga, anasema hivi sasa serikali imejipanga kutafuta wanunuzi wa bei nzuri ya kahawa katika soko la dunia na tayari wameshapatikana wanne na walishafika nchini na wameonyesha nia ya kununua kahawa ya Tanzania.

Habari Kubwa