Wasichana 36 wakimbia ukeketaji Mkoa wa Mara

18Jan 2020
Sabato Kasika
Mara
Nipashe
Wasichana 36 wakimbia ukeketaji Mkoa wa Mara

JUMLA wasichana 36 kutoka wilayani Tarime mkoani Mara, wameepuka na vitendo vya ukeketaji baada ya kukimbilia katika Kituo cha Nyumba Salama.

Baadhi ya watoto wanaokimbia ukeketaji na kulelewa katika vituo vya nyumba salama za Butiama na Mugumu wakiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly. PICHA: MTANDAO

Idadi hiyo ni ya wasichana waliopokelewa kuanzia mwezi Desemba mwaka jana hadi mwaka huu, kulingana na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samuel.

Robi ambaye anamiliki kituo hicho cha Nyumba Salama, anasema miezi hiyo huwa ni kipindi cha ukeketaji kila mwaka.

"Kimsingi ukeketaji ni mila inayopigwa vita kwa sababu una athari kwa mtoto wa kike, ndiyo maana kumekuwapo na jitihada za kuitokomeza, lakini bado tatizo lipo kwenye baadhi ya makabila," anasema Rhobi.

Anasema, Hope for Girls and Women Tanzania, ambayo inamiliki vituo viwili katika wilaya za Butiama na Mugumu wilayani Serengeti, zimekuwa kimbilio kwa wasichana wanaokataa kukeketwa.

WALIVYOOKOLEWA

Rhobi anasema, kila ifikapo mwezi Desemba huwa ni kipindi cha ukeketaji, hivyo muda huo unapowadia wasichana wanaokuwa hatarini wanatafuta marafiki wa shirika hilo kuomba msaada wa kuwakimbiza.

"Ndivyo ilivyokuwa kwa mwaka jana mwanzoni, tulipokea hao wasichana ambao walifika Butiama kwa msaada wa marafiki wa Hope for Girls and Women Tanzania," anasema.

Anasema shirika hilo lina marafiki karibu kila kona ya mkoa wa mara, na ilikuwa ni rahisi wasichana hao kuwafuata na kuwezesha kuepukana na ukatili huo.

"Marafiki zetu wanajulikana, hivyo mabinti, ambao wameshapata elimu kuhusu madhara ya ukeketaji, inakuwa rahisi kuwafuata, na ndivyo ilivyotokea kwa hao wasichana 36 waliokimbia hadi Butiama," anasema.

Mkurugenzi huyo anafafanua kuwa marafiki hao wakawasiliana na viongozi wa Hope na kuelekezwa wawapeleke wasichana hao, katika kituo cha Nyumba Salama kilichopo Mugumu.

"Baada ya kuwapokea tulishirikisha ustawi wa jamii, dawati la jinsia na tukaweka mikakati ya kujenga urafiki na wazazi wao na kuwaelimisha kuhusu madhara ya ukeketaji," anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, lengo la kufanya hivyo ilikuwa ni kutaka wazazi na walezi waelewe madhara ya ukeketaji na kuachana vitendo hivyo na hatimaye kuishi na watoto wao salama.

Anafafanua kuwa shirika hilo lina fomu maalum, ambazo anapewa mzazi kabla ya kukabidhiwa mtoto wake, akiapa kutojishughulisha na vitendo vya ukeketaji.

Rhobi anasema, fomu hizo pia zinasainiwa na viongozi wa serikali wakiwamo wa ustawi wa jamii na dawati za jinsia, hivyo mzazi anayekiuka anajiweka katika mazingira ya kukumbana na vyombo vya dola.

27 WARUDISHWA KWAO

Anasema, kutokana na utaratibu huo, wasichana 27 wamerudi nyumbani kwao, kuendelea na masomo, baada ya wazazi wao kuelimisha na kuelewa madhara ya ukeketaji na kuahidi kutowafanyia watoto wao vitendo hivyo vya kikatili.

"Kwa hiyo hadi sasa wasichana hao wako kwa wazazi wakiendelea na masomo baada ya kuwekeana makubaliano maalum, ambayo ni lazima mzazi ayatimize kwa ajili ya usalama wa mtoto wake," anasema.

Mkurugenzi huyo anasema, wakati wasichana hao wanarudi kwao, wengine tisa wataendelea kuwapo kituoni hapo baada ya wazazi wao kukataa kuwapokea, wakidai mabinti hao wamewadhalilisha kwa kukataa kukeketwa.

"Tutaendelea kuwa nao na tutawasomesha, mpaka wahitimu, watapata mafunzo maaluma ya kuwawezesha kujitegemea hapo baadaye," anaongeza kusema.

Anasema, wataendelea kujadiliana na wazazi wao, huku Hope ikiwapa mafunzo maalum kuwasaidia kujitegemea endapo watarudi kwa wazazi wao.

MADHARA YA UKEKETAJI

Wataalamu wa afya wanasema ukeketaji una madhara kiafya na huweza kusababisha kifo wakati akifanyiwa kutokana na kupoteza damu nyingi.

Aliyekeketwa anaweza kupata uharibifu mkubwa wa mfumo wa nje ya uzazi, matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua.
Pia humsababishia maumivu wakati wa kujamiiana.

Hivyo ni wajibu wa wadau wote wanaopinga vitendo hivyo, kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu ubaya wa ukeketaji.

Habari Kubwa