Wasomali waja nchini kufunzwa uvuvi wa kibiashara

16Sep 2016
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Wasomali waja nchini kufunzwa uvuvi wa kibiashara

WIKI iliyopita jarida hili lilikuwa na makala iliyohusu samaki walivyo na nafasi katika kukuza uchumi wa nchi, huku kukielezwa mitazamo mbalimbali.

Katika mitazamo hiyo, mojawapo inahusu juhudi za makusudi zinazowahusisha wataalam wa uchumi, masoko na uzalishaji samaki na baadhi ya taasisi.

Semina maalumu ya kitalam ilifanyika mjini Mwanza kujadili suala hilo na wataalam na wadau na wakatoka na ajenda kadhaa.

Kimsingi, uvuvi na ufugaji wa samaki katika mabwawa au pembezoni mwa vyanzo vya bahari, ni kati ya biashara kubwa zinazotegemewa katika baadhi ya nchi na hasa Bara Asia.

Uchumi wa wakazi waishio kwenye fukwe za bahari na maziwa, hutegemea zaidi fursa kubwa zilizopo kwenye maeneo hayo.

Mazao yapatikanayo katika fukwe hizo au mabwawa mara nyingi ni samaki wa aina tofauti.

Inaelezwa kuwa, uvuvi na ufugaji wa samaki si biashara pekee. Pia, ni chanzo cha ajira inayoendana na kutoa uhakika wa chakula na kukidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa.

Hilo ni kwa ajili ya samaki kutumika kama kitoweo kinachotegemewa zaidi, kukidhi mahitaji ya watu na watumiaji.

Pia ni biashara inayozuia kutoweka rasilimali zilizopo majini na hasa viumbe hai.

MAFUNZO YA KIMATAIFA

Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica),hivi karibuni katika Chuo cha Maendeleo ya Uvuvi Mbegani - Bagamoyo kilitoa mafunzo kwa wakufunzi 15 wa sekta ya uvuvi kutoka nchini Somalia.

Mafunzo hayo ya wiki tano yalianza mwezi Mei mwaka huu, yakilenga kuongeza ajira na kupunguza uvuvi haramu na uharamia katika bahari ya Hindi.

Mkurugenzi Mwakilishi wa Jica nchini, Toshio Nagase, katika mafunzo hayo anasema lengo ni kuondokana na uvuvi haramu na
kuongeza wigo na fursa ya ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo.

“Lengo ni kupanua wigo wa ajira kwa vijana na kuwafanya wasijihusishe na makundi ya uhalifu zaidi wajikite katika ajira hii, baada ya kupata ujuzi,” anasema.

Anasema uvuvi ni nyenzo muhimu katika nchi yoyote ambayo ina rasilimali ya upatikanaji wa vyanzo vya uvuvi.

"Somalia ina ukanda wa bahari wa kilomita zipatazo 3000. Maliasili hii ikitumiwa vizuri, ni fursa kwa vijana watajipatia ajira, usalama wa chakula na kutakuwapo lishe bora," anasema.

SERIKALI YA TANZANIA

Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka Wakala wa Elimu ya Mafunzo ya Uvuvi katika Chuo cha Mbegani, Ambakisye Simtoe, anawataka vijana wajiajiri na kuchangamkia fursa katika sekta ya uvuvi, ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira nchini.

Simtoe ambaye pia alikuwa mwezeshaji wa mafunzo hayo, anasema sekta ya uvuvi nchini ina fursa kubwa, ikizingatiwa inahitaji mtaji mdogo.

Anasema kunahitajika uwekezaji mdogo kwa mtu anayeanza ufugaji wa samaki, kwani mahitaji pekee yaliyopo ni vifaranga vya samaki na bwawa lao.

Anasema kwa wanaoanza ufugaji huo wanapewa elimu bure ya ufugaji, ili wamudu kukabiliana na changamoto zinazojitokeza, ikiwamo ugonjwa.

Kuhusu wavuvi wadogo, Simtoe anasema serikali imeanza kuwapa kwa kuwapatia injini za boti 100.

"Vifaa vya uvuvi vikiwa vya kisasa, vinaondoa uvuvi haramu, kwani mvuvi akiwa na injini ya boti itamfikisha mbali kitaalamu. Atafika kwenye ‘pima’ 15 hadi ‘20’ na ndiko kwenye samaki wengi," anasema.

Simtie anasema elimu inahitaji kuendelea kutolewa kwa Watanzania wenye dhana kuwa, sekta ya uvuvi haina faida.

SERIKALI YA SOMALIA

Mwakilishi kutoka Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Somalia, Mohamed Farah, anasema baada ya vita ya muda mrefu nchini mwao, serikali yao imeanzisha mpango wa kuongeza ajira kwa vijana.

Anasema nchini Somalia, asilimia 75 ya wananchi wake ni vijana na kati yao, wengi wenye umri kati ya miaka 14 na 42 hawana ajira. Hivyo, mkakati huo unasaidia kuwaanda vijana kujiajiri.

Mshauri Mwandamizi wa Wizara ya Uvuvi na Rasilimali za Bahari wa nchi hiyo, Omar Abdulle Hayle, anaahidi watahakikisha vijana wanapata vifaa vya kisasa vya uvuvi na kujishughulisha katika sekta hiyo na kuachana na shughuli haramu.

Anasema Sheria ya Uvuvi ya Somalia, inalenga kutoa fursa kwa vijana wanaojiunga na sekta hiyo, wanajiingiza katika makundi yasiyofaa katika jamii na kujipatia ajira, ikiwamo kuongeza usalama wa chakula.

SHERIA ZA BIASHARA

Hivi karibuni, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe alipozindua Chama cha Sheria za Bahari (MLAT), alisema kitasaidia kuweka kanuni, taratibu na sheria za bahari.

Dk. Mwakyembe ambaye pia ni mwanasheria mwandamizi, anasema sheria madhubuti ndizo zitakazodhibiti biashara za magendo na zinazokwepa ushuru na kupitisha bidhaa katika fukwe.

Anasema changamoto kubwa iliyopo katika fukwe nchini, ni uhaba wa vifaa vinavyodhibiti uhalifu, ikiwamo kupitishwa bidhaa za magendo na ujangili.

Anasema majangili wana kawaida ya kuvua samaki kwa magendo katika maeneo yenye samaki wengi na wengine wanachafua fukwe za maeneo hayo.

“Barani Afrika ni nchi tatu tu zilikuwa na chama kama hiki. Tanzania imekuwa ya nne. Hii ni hatua mojawapo ya kudhibiti bahari. Nchi yetu ni lango kuu la bidhaa zitokazo nje kwenda nchi jirani: Malawi, Zambia, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na za Afrika Mashariki,” anasema Dk. Mwakyembe.

Anasisitiza kwamba, serikali itashirikiana na chama hicho katika kuweka sera na kutunga sheria za kudhibiti biashara ya magendo na haramu katika fukwe nchini

Makamu Rais wa MLAT, Ibrahim Bendera, anasema kutokuwapo mtaala unaofundishwa katika vyuo vikuu nchini kuhusu sheria za bahari, ni changamoto kubwa.

Anasema kilichopo sasa ni kwa sheria hizo zinafundishwa hadi katika ngazi ya shahada ya uzamili, wakati wanaochukua shahada wanahitimu bila ua kuzifahamu sheria hizo.

“Tanzania haina chuo kikuu hata kimoja kilicho na mtaala wa sheria za bahari. Hii inasababisha masomo hayo kufundishwa katika ngazi ya juu ya shahada ya uzamili,” anasema Bendera.

Habari Kubwa