Wataalamu wanapotafuta elimu ya kujitegemea kwa wastaafu

24Mar 2020
Nimi Mweta
Dar es Salaam
Nipashe
Wataalamu wanapotafuta elimu ya kujitegemea kwa wastaafu

WAHENGA walisema dunia ni mviringo, siyo tu kwa sababu ukizunguka dunia kwenda mashariki utaishia magharibi na mwishowe kurudi ulipotoka, ila kwa maana yake pana zaidi kimaisha.

Mzee mstaafu akisaidiwa kupata huduma mbalimbali. PICHA: MTANDAO.

Ndiyo hali inayoonekana katika suala zima la maana halisi ya Elimu ya Kujitegemea, kuwa kama ulivyo ‘mtego wa panya,’ wanaingia waliokuwamo na wasiokuwamo.

Awali walikuwa ni watoto wa shule wakifikia ujana waelekezwa kujitegemea si kutaka ajira mijini; sasa ni wastaafu.

Tena wastaafu wa kipindi hiki ndiyo zaidi walikuwa shule za msingi wakati wa Azimio la Arusha, ambako mada ya Elimu ya Kujitegemea ilifuata wiki kadhaa baadaye, ikiambatana na insha ya Ujamaa Vijijini.

Machapisho hayo matatu kimsingi yaliweka kwa upana kiitikadi na kisera dhana nzima ya Ujamaa hapa nchini, hadi ilipoondolewa kimyakimya miaka ya 1990 mwanzoni. Ila insha hizo hazikuwahi kupoteza umaarufu wake licha ya kutekelezwa ‘ndivyo sivyo’ awali.

Kinachoshangaza ni jinsi mazingira ya kiuchumi na maisha kwa jumla hasa kuanzia miaka ya 1990 yalivyobadilika, na hatua kwa hatua kundi linalohitaji elimu ya kujitegemea linakuwa si la vijana tena, ila wazee.

Suala ni kwamba kwa upande wa vijana suala la kujitegemea lilikuwa mwelekeo wa ziada kwa kile ambacho walikuwa wanakitafuta, yaani kuendelea na masomo hadi sekondari na hata elimu ya juu. Endapo wasingefika hapo, wasione ni mwisho wa matumaini.

Hivyo elimu ya kujitegemea haikuwa inahoji mwelekeo wa kuinuka kimaisha kupitia elimu ila dhana kuwa bila ajira ya ofisi suala zima la kwenda shule ni kama lilikuwa halina maana.

Hali hiyo ilikuwa tayari inaleta mvutano kijamii kwani mwaka 1968, ambako mazingira yanafanana na kipindi insha ya Elimu ya Kujitegemea inaandikwa, ni watoto 13 tu waliokuwa wanaingia sekondari pindi wakimaliza shule ya msingi. Familia zilikuwa zinawaona wamefeli kimaisha, n.k.

Kwa maana hiyo elimu ya kujitegemea aina ya kwanza, au maana yake halisi, ni kutumia elimu ya msingi (hadi kumaliza madarasa ngazi hiyo) kama njia ya kuelewa stadi za maisha, ikiwamo kilimo, ufundi wa ngazi tofauti na hasa unaohusu ujenzi, uashi, cherehani, randa, plau, kilimo bora, n.k. Jitihada hizo zilitakiwa ziwe sehemu ya mafunzo shuleni ili wanafunzi wakimaliza ngazi hiyo ya maisha waendelee na uelewa huo vijijini. Wasianze kukata tamaa kwa ‘kufeli.’

Stadi hizo kimsingi zimeendelea kuwa muhimu ila hazianzii moja kwa moja shule za msingi ila baada ya hapo, licha ya kuwa baadhi ya masomo ya stadi za maisha yaliingizwa hatua kwa hatua katika mitaala.

Baadhi ya wataalamu wanaona hatua hiyo ilisaidia kuvuruga uelewa na undani wa kufikiri wa wanafunzi, kwani muda ambao ungetumiwa kuitafakari dunia, sayansi au historia unatumiwa kujifunza na kushona. Si mwanafunzi atajifunza kivyake baada ya shule, akitafuta maisha?

Katika miaka ya 1990 wakati serikali inapunguza idadi ya wafanyakazi enzi za kuanza kutumika kwa kompyuta na kuondolewa ‘mafaili’ lukuki katika maofisi, umuhimu wa stadi za maisha ndipo ulipoanza.

Ila haukujikita katika akili au hisia za watu wa njia hiyo, ila kama shughuli za kibiashara, na ghafla Tanzania ikaanza kuwa taifa la wachuuzi wadogo wadogo wanaokaa mijini. Sehemu ya bidhaa, hasa mazao na mbogamboga ilikuwa inatoka vijijini, na nyingi zaidi kutoka viwandani mijini na nyingine kutoka nje, hasa mitumba – eneo pana zaidi la ajira ya vijana.

Walioendelea kufanya kazi katika sekta ya umma na hata binafsi hatua kwa hatua wakaingia katika biashara, hasa baada ya kuondolewa ‘miiko ya uongozi’ kupitia Azimio (au |Tamko) la Zanzibar, 1991.

Ilikuwa ni hatua ya pili ya kuondoa mfumo wa Ujamaa katika shughuli za uchumi, hatua ya kwanza ikiwa ni kulegeza masharti ya kuingiza bidhaa nchini au kuuza nje, ikiendana na kuondolewa kwa vijiji vya ujamaa, kila mtu alime kivyake.

Hatua ya pili ikawa ni ubinafsishaji, kulegeza upatikanaji wa fedha za kigeni, na kuruhusu waajiriwa kumiliki biashara.

Kinachoonekana katika mada za miaka ya karibuni kwa mfano mijadala kuhusu mifumo ya kuondoa akiba baada ya kuacha kazi, ni hali halisi kuwa wanaofikia umri wa kustaafu mara nyingi zaidi wanauona umaskini ukiwanyemelea.

Ina maana hapakuwa na uwezo wa kutosha miongoni mwa wafanyakazi walio wengi kuingiza fedha katika shughuli za ziada ambazo zinawakinga na umaskini,na hiyo ni kweli kwa walio wengi. Licha ya kuwa watalaamu wanasema kuwa wengi waliwekeza katika familia zao, kudai umaskini unatoka hapo ni kuongeza chumvi.

Kutokana na hulka ya kawaida ya kuoneana haya, mhadhiri Dk. Godson Lema wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi hakuzungumzia kuna uhusiano gani kati ya starehe za ujana na hata utu uzima, na umaskini uzeeni.

Umaskini umekuwa ukizungumziwa zaidi kuhusu wanawake na watoto, na kwa kiasi fulani vijana ingawa hapo kinachojadiliwa ni ajira na siyo umaskini wenyewe – wakati hali ya wazee inakuwa somo tofauti.

Si umaskini kwa jumla ila kustaafu, na kuondoa hali hiyo kinachohitajiwa siyo tena stadi za maisha kwani zinahitaji uwezo wa kufanya kazi. Ni mpangilio sahihi wa kustaafu, kujiwekea akiba, n.k.

Hapo, kuna kitendawili kwani mishahara wanayopata walioko kazini, hata wa ngazi za juu, haitoshi kuweka akiba inayoweza kutumika kwa njia endelevu? Suala hapa ni kujiwekea mazingira ya kuwa na uwezo wa kumudu maisha ya kijijini baada ya kustaafu, kwa kuwa na nyumba, shamba na mifugo, na itazamiwe kuwa maji pia yatakuwa yanapatikana.

Ila mtu anaweza kujizalishia chakula, huku bei ya mazao kama mbogamboga pale ambapo kuna soko, ni ya kutupa, isiyofaa mstaafu jijini.

Habari Kubwa