Watanzania asilimia 60 kupatiwa chanjo

15Jan 2022
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania asilimia 60 kupatiwa chanjo
  • *Elimu yaondoa hofu, mashaka kwa jamii

TAKWIMU zinaonyesha kuwa, hadi kufikia Desemba 18, mwaka jana, jumla ya watu 1,275,795 wamepata chanjo ya UVIKO-19 sawa na asilimia 2.21 ya Watanzania wote.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichakwe, anaeleza takwimu hizo zilitolewa Desemba 21, mwaka jana, wakati wa semina ya Uhamasishaji na Utoaji wa Chanjo kwa Wataalam wanaotekeleza Mpango Harakishi na Shirikishi Awamu ya Pili, unaotekelezwa na Wazara ya Afya, Kitengo cha Elimu kwa Umma.

Dk. Sichakwe anasema hadi mwezi Desemba mwaka jana, kupitia ushirikiano na mashirika mbalimbali (COVAX Facility) na wadau wa maendeleo ambapo nchi ilipata chanjo kwa asilimia 20 ya wananchi na mpaka sasa jumla ya dozi 4,421,540 zimeingia nchini.

“Juhudi mbalimbali zinaendelea ili kuweza kupata kiasi cha chanjo kitakachowezesha kuchanja asilimia 60 ya wananchi ambacho kitawezesha kufikia kiwango cha kinga kinachohitajika kulinda jamii yote,"anasema.

Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi, anasema mpango huo, Harakishi na Shirikishi Awamu ya Pili wa Kampeni ya Uhamasishaji na Utoaji Chanjo ya UVIKO-19, unalenga kuchanja watu 80,000 hadi 100,000 kwa siku.

Anasema kila mkoa utatakiwa kuchanja watu 4,000 hadi 5,000 kwa siku ili kufikia lengo la kuchanja asilimia 60 ya Watanzania.

Anasema awamu ya kwanza ya mpango huo, walikuwa wakichanja watu 20,000 hadi 40,000 na ndio sababu ya kuanzisha mpango huo harakishi na shirikishi.

“Mpango huu utahusisha mitaa na nyumba kwa nyumba na pamoja na kuhamasisha chanjo, wataalam wa afya, watatoa huduma za kupima na matibabu kwa wagonjwa waliopatikana na magonjwa," anasema.

Aidha, anasema tafiti zinaonyesha kuwa, asilimia 70 ya Watanzania wapo tayari kuchanja chanjo ya UVIKO-19.

Anasema pia kwa upande wa Afrika, utafiti unaonyesha asilimia 70 hadi 80 wapo tayari kupata chanjo ya UVIKO-19.

Anasema wameanza kufanya Utafiti wa Chanjo wa UVIKO-19 na magonjwa mengine nchini.

Prof. Makubi anasema Wizara ya Afya, pia inaendelea kutoa elimu kwa jamii ili ielimike na kuanza kuelimishana wenyewe katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.

Anaeleza serikali imetumia mfumo wa afya na serikali za mitaa kuhakikisha elimu inawafikia moja kwa moja wananchi na kupata chanjo.

“Kupitia elimu inayotolewa watu wanaelimika bila kufunga mipaka ya nchini na shughuli za uchumi zinaendelea,” anasema Prof. Makubi.

Anasema awamu ya kwanza ya mpango huo, ilifanikisha watu kujitokeza kwa wingi kupata chanjo na kusababisha chanjo za Johnson & Johnson kumalizika kwa wakati.

Anasema kwa sasa kuna aina mbili za chanjo na wananchi waendelee kuchanja ambazo ni Pfizer na Morderna.

"Hatua hii inaonyesha kuwa Rais Samia anawapenda Watanzania na kuwaona wananchi wanakuwa na afya njema, tumefanya kuwa harakishi kwa sababu ugonjwa wenyewe ni haraka na unaua watu kwa haraka," anasema Prof. Makubi.

Anawahimiza pia kuwapa moyo wananchi na kuwaonyesha umuhimu wao katika kupata chanjo na faida zake.

HAKUNA LENGO BAYA

Aidha, Prof. Makubi, anasisitiza serikali ina nia njema ya kuwatakia afya njema Watanzania kwa kuhakikisha wanachanja kwa asilimia 60.

"Hakuna chanjo iliyofanikiwa kwa kulazimisha bali kwa kuelimishana na wananchi na kuelewa sayansi, hivyo baadae mtu kuamua kuchanja Kwa hiari yake," anasema Prof. Makubi. 

Anasema kampeni hiyo itaenda  kuwatumia viongozi wa mitaa wenyewe na kwamba kampeni ya mtaa kwa mtaa, haileti ulazima bali ni kupeana elimu ngazi ya mtaa na wananchi kwa hiari yao kwenda kuchanja.

Prof. Makubi anaongeza kwamba licha ya chanjo bado wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kwa kunawa mikono mara kwa mara na maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano na kuvaa barakoa.

"Jambo jingine niwakumbushe wananchi kufanya mazoezi pamoja na kula lishe bora, kwani mazoezi ni muhimu na inasaidia mifumo ya hewa kuwa mizuri," anasisitiza Prof. Makubi.

Naye, aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, anasema ni muhimu kushirikishana na viongozi wa dini, mitaa na kimila ili kuwa na namna bora ya kuwafikia wananchi ili kuwalinda wazee waliopo majumbani.

Kadhalika aliwataka viongozi hao kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 na kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Hali ya ugonjwa nchini

Aliyekuwa Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, anasema maambukizi ya UVIKO-19 yanaongezeka nchini, hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari.

Ametolea mfano idadi ya sampuli zinapokelewa Maabara Kuu za Taifa ni 47 kwa siku, tofauti na siku za nyuma zikiwa zinapokelewa sampuli 14 kwa siku, hali inayoonyesha idadi ya maambukizi inaongezeka.
 
Dk. Gwajima anasema, wananchi wamekuwa hawachukulii suala hilo kwa uzito unaotakiwa na ndio sababu hawaendeleai kuchukua tahadhari.
           
"Kasi ya kujikinga na maambukizi bado ni ndogo la licha ya kuwa wananchi wanaendelea kuchanja bado wanaohitaji msukumo," anasema Dk. Gwajima.
 
Akizungumzia hali ya wagonjwa wa UVIKO-19, anasema kati ya wagonjwa 10 wanaofariki dunia, saba kati yao ni wale ambao hawajachanja na wengine watatu ni wale waliochanja lakini waliozidiwa na magonjwa mengine kama Shinikizo la Damu, kisukari na wazee.
 
“Tunataka tusikilizane kila mtu achukue tahadhari na serikali haitaki kutumia nguvu kuwasihi wananchi na kutoa makatazo ya kusherekea sikukuu, bali jamii inatakiwa kuchukua tahadhari zote," anasema.

Habari Kubwa