Watanzania bega kwa bega na viwanda 2019

06Jan 2019
Zuwena Shame
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Watanzania bega kwa bega na viwanda 2019

HONGERENI wasomaji wa Nipashe kwa mwaka mpya 2019. Wengi mna njozi na maono mengi ikiwamo kuanzisha viwanda na kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati unaosimamishwa na viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), liKIhamasisha viongozi wa wilaya zote nchini

Ni wazi kuwa ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda Watanzania wanahitaji kuelimishwa, kuhamasishwa na kuunganishwa ili kufahamu masuala ya kilimo chenye tija, usindikaji, biashara, kuongezea mazao thamani, utafutaji na ufikiaji masoko baada ya uzalishaji.

Lakini, pamoja na kuelimishwa wanataka nyenzo na mashine za kufanikisha uzalishaji viwandani ili kufikia azma hiyo ya kutengeneza bidhaa kwa walaji wa nje na ndani, ndiyo maana taifa linapoanza mwaka mpya, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) linawataka wananchi kujiunga pamoja na kuanzisha viwanda vidogo wakiwa ndani ya vikundi vya ushirika wa uzalishaji ili iwafikie na kuwasaidia kutimiza malengo yao.

Nipashe inayapata hayo mwishoni mwa mwaka jana wakati wa kongamano la Sido la kuwapa wajasiriamali mbinu mbalimbali za kujiinua kiuchumi lililoambatana na maonyesho vyote vikifanyika mkoani Simiyu. Katika kusanyiko hilo , gazeti hili lilizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji wa Sido, Shoma Kibende, anayefafanua lengo la kongamano hilo.

Anaanza kwa kuwahamasisha Watanzania kuwa wabunifu kwani ndiyo mkakati wa maonyesho hayo ya kongano (clusters) za viwanda kutoka mikoa mbalimbali ili kuwe na uibukaji wa mambo mapya katika sekta mbalimbali wenye kusukuma myororo mzima wa thamani katika maeneo yanayoibuliwa mfano kwenye mazao ya kilimo na viwanda vingine kama vya chuma, madini na utalii.

Kibende anataja mfano wa mkakati huu wa kongano za Sido akisema unaanzia kwa mzalishaji na Sido inahakikisha kuwa malighafi inayopatikana inasindikwa ipasayvo kuongezewa thamani lakini inafungashwa kikamilifu na inapata ubora na inaingia sokoni.

Anaeleza kuwa kwa kujiunga kwenye vikundi taasisi mbalimbali zinakuwa na urahisi wa kuwapatia huduma wajasiriamali kwa hiyo mwana kikundi anapata fursa nyingi kupitia kongano za uzalishaji kwenye maeneo  tofauti.

Kwa mfano Kibende anasema wako katika maeneo tofauti mfano kuna makongano ya watengenezaji bidha za vyuma ambao wanahitaji wazalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na vyuma , hawa wanakuja pamoja wanaweza kutengeneza bidhaa ya vyuma ambazo ni bora.

Kibende anasema Sido ina kongano nyingine za usindikaji wa mafuta ya alizeti zinazoanzia katika kumshawishi mkulima awe ndani ya kikundi na kumuingiza ndani ya kongano na kuanza kupewa elimu, ushauri wa kilimo bora ili kupata mazao bora huku akifunzwa kutumia mbegu bora na hatimaye kuzalisha mafuta yenye viwango.

Aidha, Sido inaingilia kati kuhakikisha kuwa alizeti inavunwa na kuhifadhiwa kwa kutunzwa katika ubora, kusindikwa vizuri na kupata mafuta bora. Lakini pia, hata yale mabaki yanayopatikana baada ya kuzalisha mafuta hutengeneza bidhaa nyingine.

Mfano katika kongano ya alizeti licha ya kwamba wanasindika mafuta lakini pia wanatengeza mkaa, mafuta yakisafishwa mara ya pili mabaki wanatengenezea sabuni, yanayobaki tena baada ya sabuni yanazalisha rangi ya viatu.

Kwa hiyo wana kongano hasa wakulima wamefundishwa mnyororo mzima wa thamani kuanzia mbegu hadi bidhaa yenyewe ikiwa katika ubora . Sido inahamasisha kuanzisha vikundi au kongano na kwamba zina mafanikio makubwa kwa wakulima na wajasiriamali kwani ni uanzishwaji na ukuaji wa viwanda vidogo vidogo unaoonekana na wenye manufaa.

“Kongano hizo si kwamba wanachama wakae sehemu moja kuna wanaosambaa maeneo tofauti lakini wana jumuika na kuwa na umoja wao ambao wanazungumza pamoja changamoto na mafanikio ambayo kwa Sido inakuwa rahisi kutatuliwa na kuona hatua zinazofikiwa kimaendeleo” anasema Kibende.

Anaongeza kuwa shirika hilo limeona baadhi ya wajasiriamali walioko kwenye kongano vijijini wameweza kujipatia vibali vya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa sababu Sido inafanya kazi na wadau kwa ukaribu ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara walioko kwenye kongano wanamaliza mnyororo wa thamani na kufikia hatua ya kuuza bidhaa bora na kuwa chachu ya viwanda vinavyohudumia soko la Afrika Mashariki.

WANA KONGANO

Mmoja wa wanakongano walioshiriki kongamano na maonyesho hayo ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Kichawama kutoka Magu mkoani Mwanza, Juma Jangani, anayesema kupitia Sido wamepata mikopo ya mashine kubwa ya kisasa ya kukoboa mpunga yenye thamani ya shilingi milioni 90.

Anasema kikundi kilifanikiwa kwa waliojiunga pamoja na kilichangia asilimia 25 ya mkopo na kiasi kilichobaki walipewa na wafadhili wengine wa mpango wa kusaidia fedha, masoko, kuongeza thamani ya mazao vijijini (MIVARF)

Anasema: “Changamoto kubwa inayowakwamisha wajasiriamali ni mazingira magumu ya kufanyia kazi lakini wakiungana pamoja wanapata suluhisho la changamoto hizi kwa kuwa wanaungwa mkono na Sido.”

Jangani anasema kikundi chao kina wanachama nane na hivyo ulikuwa ushauri wa Sido kujiunga katika makundi ili kupata mashine hiyo ya kukoboa mpunga kwa kiwango cha hali ya juu tofauti na mashine ndogo.

“Mashine inafanyakazi kwa haraka na kwa ubora zaidi. Sasa tunanunua mpunga kutoka wa wakulimu na kuuongeza thamani kwa haraka na kwa viwango”.

Anasema pamoja na kufanikisha hilo, changamoto nyingine wanayokabiliana nayo kama kikundi ni uhaba wa vifungashio na kutambuliwa na mashirika ya uthibiti wa chakula na kupewa cheti mfano Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula Madawa (TFDA) ili kusaidia kupata cheti cha uhakiki na kuuza mazao yao kwenye maduka makubwa ya supermarkets na hata nje ya mipaka.

“Tayari mzao yetu ni bora na tumeongeza thamani lakini bado tunahitaji mtaalamu wa kuchataka aliye na mafunzo, vifungashio, nembo na uthibitisho au cheti na ruhusa kutoka kwa mamlaka za udhibiti ni muhimu utusaidie kufikia  masoko makubwa zaidi iwe ndani na nje ya nchi” anaongeza Jangani.

MASHINE

Meneja wa kituo cha uendelezaji teknolojia cha Sido mkoani Kigoma, Mabamba Majogoro, anasema wanatengeneza mashine za kuchakata mazao mbalimbali kama  korosho, karanga, maharage, mahindi na alizeti ambayo ni rahisi kuzitumia.

“Kigoma tayari tumeshaanza mpango wakutengeneza machine ambazo zitapatikana kwa wakulima wengi kwa mfano wa mawese tuna mashine zinazolenga mkulima mmoja mmoja na kundi kubwa hivyo tumeanza kuzizalisha kulingana na mahitaji ya kila mmoja,” anasema.

Akifungua rasmi maonyesho na kongamano hilo, Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa, anazitaka taasisiza kuendeleza tafiti na kusaidia viwanda zifanye kazi kwa pamoja ili kusaidia wajasiriamali kukuza na kuwekeza kwenye bidhaa mbalimbali.

“Serikali ina matarajio makubwa kwenye sekta ya viwanda, ubunifu na maarifa vinahitajika kwenye kukuza viwanda,” anasema na kuitaka Sido kubuni teknolojia rahisi ambazo zitawezesha wajasiriamali kijijini kuwa na mitambo ili iwe rahisi kuongeza thamani za biashara zao.

Anakumbusha kuwa viwanda vidogo na vya kati vina mchango mkubwa katika uchumi, maendeleo na ustawi wa nchi yoyote na kwamba vinatoa ajira kwa watu wengi hivyo havipashwi kubezwa.

 

 

Habari Kubwa