Watanzania na mchango wa kipekee kuondoa joto duniani

05Jul 2019
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania na mchango wa kipekee kuondoa joto duniani

NI wazi kuwa usalama wa dunia, unaowezesha uzalishaji mali na ukuzaji uchumi unategemea afya ya mazingira.

Wiki iliyopita Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira umemalizika karibuni huko Bonn nchini Ujerumani na kuibua masuala mengi yanayolielekeza kila taifa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti ya tathmini ya mabadiliko ya tabianchi iliyotolewa na jopo la kiserikali la kimataifa linalotathimini hali hiyo (IPCC), inasema kuwa kufikia mwaka 2030 joto la dunia linaweza kuongezeka na hadi nyuzi joto 1.5 jambo ambalo ni hatari zaidi kwa afya ya baharí na viumbe wengine na kuhatarisha maendeleo na uchumi wa dunia.

Hali hiyo kama haitadhibitiwa ikiachwa kuendelea kama ilivyo itakapofika mwaka 2052 nyuzi joto duniani zitapanda hadi mbili (2) kutoka 1.5 na kuhatarisha maisha ya viumbe baharí ikiwa ni pamoja na visima kama Zanzibar, Mafia na Pemba kutoweka.

Ongezeko la joto duniani linaathiri nchi kavu na bahari, hii inamaanisha kuwa kuna kupanda zaidi kwa kina cha bahari kunakotokana na kuyeyuka kwa mabonge ya theluji yanayojaza kina cha bahari. Hivyo bila kuhakikisha matumizi na ulinzi endelevu wa bahari ni wazi eneo hilo litakuwa limeathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa mtandao wa global watch, tafiti zinaonyesha kuwa kina cha bahari kinajaa kwa kasi kutokana na barafu iliyoko kwenye bahari ya Arctic kuyeyuka.

Mtandao unaeleza kuwa theluji hiyo yenye ukubwa sawa na taifa la Marekani, kuanzia mwaka 1978 hadi 1996, imesinyaa na kuyeyuka na kiasi cha kilometa za mraba 34,300 zinayeyuka kila mwaka.

Aidha, barafu ya Greenland, ambayo ni kubwa kuliko zote duniani nayo imeendelea kuyeyuka na athari zinaishia kwenye kujaza kina cha bahari ikiwamo ya Hindi.

Pamoja na hofu hiyo, si wakati wa kuhofishana zaidi, bali kutafuta njia na ufumbuzi. Mbinu mojawapo kubwa ya kupunguza ongezeko la joto duniani ni kuotesha miti na kutunza misitu ambayo kama mimea inatoa hewa ya oksjeni na kutumia karbon au hewa ukaa, iliyo chanzo cha joto duniani.

Wakati mkutano huo ukimalizika huko Bonn, jambo la msingi kwa Tanzania sasa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa mazingira na kulinda miti ili kuzuia athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kwani hali ilivyo ni kwamba ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu utunzaji wa mazingira miongoni mwa wanavijiji wanaoishi jirani na misitu ya asili, unatajwa kuwa moja ya vyanzo vya uharibifu wa misitu katika maeneo na mikoa mingi.

Katika mkutano wa Bonn kinachosisitizwa ni kupunguza ongezeko la joto ambalo sasa kama wataalamu wanavyosema limefikia nyuzijoto 1.5. Lakini wananchi wengi hawajatambua kuwa misitu ni rasilimali ambayo wakiitumia kwa namna endelevu inawaondolea umaskini wa kipato na pia inaokoa dunia kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Uharibifu wa mazingira unaotishia uhai wa misitu unahusisha kuvuna mbao, kuchoma mkaa na kukata magogo na kuni.

Misitu mingi iko vijijini.Huko kuna Kamati za Misitu za Kijiji, zinazoundwa na viongozi mbalimbali wakiwamo wa wilaya, ni wakati wa kuzitathimini na kujiuliza zinawashirikisha kikamilifu wana vijiji kutunza mazingira?

Kama sivyo juhudi zianze sasa ili wadhibiti kila aina ya uharibifu na unyong’onyezaji wa misitu ambayo ni muhimu zama hizi katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Misitu ya Tanzania inaweza kumalizika kwa sababu mamlaka za kusimamia misitu zinashindwa kutoa elimu kwa wanavijiji ambao bado hawajaelimishwa ipasavyo kuhusu faida za utunzaji wa misitu.

Ni vyema serikali kuwekeza kwenye kuwapa elimu wana kamati za misitu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ili wawafahamishe wanakijiji umuhimu wa rasilimali hiyo.

Kamati za maliasili za vijiji zisaidiwe na wadau kama Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Idara ya Maliasili na asasi za kiraia za kutunza mazingira ili ziwe na elimu ya kutosha ili ziwafahamishe wananchi kuhusu umuhimu wa misitu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza joto duniani ili kulinda usalama wa dunia na viumbe wa bahari.

Juhudi zifanywe kuhamasisha wananchi kuacha uharibifu wa kuvuna misitu hiyo ovyo, wafuate utaratibu na kufanyakazi za kuvuna miti, mbao, mkaa , kuni na hata kufungua mashamba kwa taratibu za kisheria ili zikiwamo kulipia gharama zinazowezesha kupata fedha kwa njia ya kulipia tozo, ushuru na kodi yote hayo yataleta fedha zinazochangia kulinda rasilimali hiyo pamoja na maendeleo ya vijiji.

Kutowashirikisha wananchi walioko karibu na misitu ni hasara kwani hawataweza kunufaika na rasilimali hizo hivyo kuchangia kuumiza taifa ambalo nalo linahitaji kujilinda na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wataalum wa Idara ya Maliasili watoe elimu kuanzia ngazi za kitongoji, vijiji na kushirikiana na kamati za mazingira na uhifadhi ili makundi hayo yatambue wajibu wao katika kulinda misitu kwani ndiyo pekee ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ongezeko la joto duniani.

Ni wakati wa kuwafundisha wanavijiji walio jirani na misitu kuhusu sheria, sera, taratibu na kanuni mbalimbali zinazosimamia kulinda na kuendeleza misitu nchini na pia kuwaeleza wananchi haki na wajibu wao kwenye jukumu hilo.

Ni wazi kuwa baadhi ya vijiji nchini vimeanza kunufaika na utunzaji wa misitu kwa kujipatia fedha zinazochangia kufanikisha shughuli za maendeleo endelevu ya misitu.

Ni vyema sasa kuanza kuangalia mwongozo wa usimamizi shirikishi wa misitu kwa jamii, unaohimiza kuwashirikisha wananchi kutunza misitu inayomikiwa na inayosimamiwa na halmashauri za vijiji.

Mwongozo huu unaeleza kuwa jamii inatoa maamuzi na katika usimamizi shirikishi wa misitu unaohusisha udhibiti, uvunaji, uboreshaji au kuongeza uwezo wa upatikanaji wa mazao ya misitu.

Kwa mujibu wa mwongozo huu wa usimamizi shirikishi wa mazao ya misitu hauanzishi taasisi mpya bali unatumia zilizopo kulinda na kutunza rasilimali hiyo.

Wadau na serikali wazitumie kikamilifu taasisi za kimataifa kama Mfuko wa Kutunza Mazingira World Wide Fund for Nature (WWF) na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira (UNEP) ili kutoa elimu kwa jamii kuhusu utunzaji wa misitu pamoja na kuhamasisha umma kunufaika na rasilimali za misitu na kuiokoa dunia na mabadiliko ya tabianchi.

Habari Kubwa