Wateuliwa wajue cheo ni dhamana, wanapoondolewa ndivyo siasa ilivyo

19Jun 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Wateuliwa wajue cheo ni dhamana, wanapoondolewa ndivyo siasa ilivyo

CHEO ni dhamana na uongozi ni utumishi, ni dhana zilizozoeleka miongoni mwa Watanzania, ingawa baadhi yao ni kama wameziweka pembani na kudhani kwamba nafasi wanazoteuliwa au kuchaguliwa basi ni haki yao.

Rais John Magufuli akiwa katika shughuli ya kuapisha wateule wake. PICHA: MTANDAO

Wapo wanaoamini kuwa cheo ni matokeo ya jitihada za mtu binafsi na si dhamana ambayo anapewa na kwamba kupata cheo kunatokana na elimu yake au uzoefu ama uwezo wa kukuza uhusiano mzuri kati yake na watu wengine.

Wapo wanaofikia kusema kuna haja ya kuondokana na fikra za kijamaa kwamba cheo ni dhamana na uongozi ni utumishi.

Hawa wanasisitiza kuwa cheo ni matokeo ya jitihada za mtu binafsi na si dhamana ambayo mtu anapewa.

Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kwamba cheo ni dhamana kama ambavyo inasisitizwa kwenye Ahadi ya 5 ya Mwanachama wa TANU ambayo imerithiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ahadi hiyo inasema: “Cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu au cha mtu mwingine kwa faida yangu.”

Hilo ndilo jambo la msingi la kutambua maana ya dhana hii ya cheo ni dhamana.

Kwa mujibu wa wataalamu wa lugha ya Kiswahili, neno dhamana ni kama kitu au ahadi inayotolewa kumdhamini mtu anayetaka kukopa mali au anayekabiliwa na mashtaka mahakamani.

Aidha, ni kitu apewacho mtu ili atimize jambo fulani, kama kuwa katika ofisi ya umma au kutimiza wajibu mwingine wowote, vinginevyo anaondolewa.

Ni muhimu kwa maana hiyo kueleweka kwamba hata kama mtu amesoma kiwango gani cha elimu na akapata cheo kutokana na elimu na uzoefu wake, kumbe sehemu anayofanyia kazi inaweza kuendelea kuwapo bila yeye.

Hivyo ni vyema wanaopewa vyeo wakatambua kuwa wameshikilia dhamana.

MSINGI WA UTANGULIZI

Msingi wa utangulizi nilioanza nao hapo juu ni mkutano wa saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aprili mwaka 2012, uliibuka mjadala mkali uliosababisha mawaziri sita na naibu wawili kupoteza nafasi zao.

Mawaziri hao walitoswa baada ya kutajwa au kuhusishwa na madudu ya usimamizi usiofaa wa fedha za serikali kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pia mawaziri hao waliguswa na Ripoti za Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Ardhi, Maliasili na Mazingira za mwaka wa fedha wa 2009/2010.

Cha ajabu baada ya kutemwa tu zikaibuka kauli mbalimbali za kushangaza zilizotolewa na baadhi yao pamoja na wapambe wao kwamba wameonewa.

Kuna waziri alimwandama aliyekuwa naibu wake, akidai kwamba alimgeuka kwenye baadhi ya maamuzi, hali ilionyesha wazi kuwa hakukubaliana kuondolewa katika nafasi hiyo.

Mbali na huyo, kuna waziri mwingine ambaye aliibuka na kudai kwamba alionewa, akisema bila kumumunya maneno kwamba aliondolewa kwa sababu ya fitna na chuki.

Ilifikia hatua ya baadhi yao kuibuka na mbinu mbalimbali kwenye majimbo yao kuhamasisha wananchi kufanya mikutano ya kuwasafisha au maandamano.

Na kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafuasi wao waliandika mabango ya kuwasafisha kwamba hawana makosa yoyote, na wengine wakitishia kutopigia kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Walisahau dhana ya kuwa cheo ni dhamana wakiamini kuwa haitatokea wakaondolewa kwenye nafasi walizokuwa wakishikilia na kujikuta wakilalamikia mamlaka za uteuzi.

Jambo la msingi hapa ambalo walalamikaji walipaswa kulifanya ni kuendelea na majukumu mengine kama kawaida, badala ya kulalamika.

Nimeanza kwa mifano hiyo michache ili kuonyesha ni jinsi gani baadhi ya viongozi wanaamini wakishateuliwa au kuchaguliwa, basi huwa ni kwa maisha yao yote kitu ambacho ni kupotoka.

Ieleweke kwamba unapoteuliwa au kuchaguliwa katika nafasi fulani ya uongozi, unaapishwa na kupewa kanuni unazopaswa kuzizingatia wakati ukitekeleza majukumu yako, lakini ukienda kinyume kuna uwezekano wa kuondolewa.

Hata hivyo, somo la cheo ni dhamana linaelekea kueleweka kwa sasa tangu kuingia madarakani serikali ya awamu ya tano mwishoni mwa mwaka 2015, kitu ambacho ni cha msingi.

Hadi sasa kuna zaidi ya mawaziri 10 ambao wameondolewa kwenye nafasi zao, na wanaendelea kutumikia wananchi wao kama kawaida bila kulalamika.

MAWAZIRI HAO

Mei mwaka 2016, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alitumbuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Mwigulu Nchemba.

Pia Mei 2017 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitumbuliwa.

Aidha, Septemba mwaka 2017, George Simbachawene (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alijiuzulu katika nafasi hiyo baada ya jina lake kuonekana katika ripoti zilizotolewa na Kamati ya Bunge kwenye uchunguzi kuhusu madini ya Tanzanite.

Katika mwendelezo huo wa mawaziri kutumbuliwa, ulimgusa pia aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe na naibu wake Mhandisi Ramo Makani (Wizara ya Maliasili na Utalii).

Wengine ni Dk. Nchemba aliyerithiwa na Kangi Lugola, Charles Mwijage Wizara ya Viwanda na Uwekezaji, Charles Tizeba (Waziri wa Kilimo) na Nape Nnauye (Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo).

Mwingine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Susan Kolimba aliyeachwa Septemba 2018, na nafasi yake ikachukuliwa na Dk. Damas Ndumbaro.

Hivi karibuni, mrithi wa Mwijage katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda naye aliondolewa kwenye nafasi hiyo.

La msingi hapa wote hawa wanaendelea kuwatumikia wananchi katika nafasi nyingine bila malalamiko.

Hiyo inaonyesha ni jinsi gani wanatambua maana nzima ya dhana ya cheo ni dhamana, ambayo kimsingi ni vyema kila kiongozi aizingatie.

Kwamba hawa hawajaenda majimboni kulalamika kwa wapigakura kudai wameonewa kama ambavyo iliwahi kutokea kwa baadhi ya mawaziri walioondolewa madarakani mwaka 2012, wakatafuta kila njia ili kuonekana wameonewa.

Kama nilivyosema, wenye mawazo ya aina hiyo ni wale ambao wanakalia ofisi za umma na kusahau kwamba cheo ni dhamana, lakini kwa yule anayejua hilo anaachia ngazi na maisha yanaendelea kama kawaida.

Mawaziri wa sasa waliotumbuliwa wanaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa ukimya wao ambao wameuonyesha, hasa kwa kutambua nafasi ya uongozi ni kama koti la kuazima ambalo mwisho wa siku litarudishwa kwa mwenye nalo.

Kimsingi hakuna aliyezaliwa akiwa na cheo au alizaliwa ili awe waziri bali anakuta nafasi hiyo baadaye, kwa kuchaguliwa ama kwa kuteuliwa, hivyo akiondolewa katika cheo ajue dhamana aliyokabidhiwa imeisha.

Habari Kubwa