Watumiaji ‘apps’ za wapenzi hutumia njia hatarishi kujenga mwonekano

25Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Watumiaji ‘apps’ za wapenzi hutumia njia hatarishi kujenga mwonekano

WANAWAKE na wanaume wanaotumia ‘apps’ ili kupata wapenzi wanaowataka, wako hatarini kutumia njia zisizofaa kiafya ili kudhibiti au kupunguza mwili, utafiti unaeleza.

Utafiti uliofanywa nchini Marekani kwa watu 1,700 umebaini kwamba kujitapisha, matumizi ya dawa za kupunguza mwili na kufunga kula ni njia zinazotumika kwa wingi.

Apps za kutafuta wenza zimekuwa maarufu sana kutokana na kuwepo kwa mitandao ya simu na intaneti miaka ya hivi karibuni.

Watu hutumia apps kuwapata wenzi wanaofikiri wanawafaa kwa kutazama mwonekano wa miili yao pia.

Katika utafiti huu, uliochapishwa kwenye jarida liitwalo Eating Disorders, watafiti wamefananisha tabia za watu wanaotumia apps kutafuta wenza na wasiotumia ‘application’ hizo.

Wakabaini kuwa watumiaji wa ‘application’ hizo wana namna sita za kudhibiti miili yao ili kuwa na mwonekano mzuri kwenye mitandao.

Kwamba hutumia njia ya kujitapisha, dawa za kuharisha, kufunga kula, dawa za kujikondesha na dawa za kujenga miili au misuli yao.

Kutoka kwa watu wazima waliohojiwa 1,726 wanawake na 209 wanaume wanasema wanatumia apps kupata wenza.

Kwenye kundi hilo, karibu nusu ya wanaume na wanawake wameripoti kwamba wanatumia njia ya kufunga kula, ili wasiwe na uzito mkubwa na mmoja kati ya wanawake watano na mwanaume mmoja kati ya watatu wanasema hujitapisha ili kuepuka kuwa na uzito wautakao.

Mmoja kati ya wanawake wanne na asilimia 40 ya wanaume, wanatumia dawa za kuharisha.

Dk. Alvin Tran aliyeongoza jopo la watafiti anasema utafiti umebaini kwamba kuna matumizi ya hali ya juu ya njia hizi miongoni mwa watumiaji.

MWONEKANO WA MWILI

Dk. Tran anasema: “Wakati hatujui kama watu kwenye utafiti huu walikuwa wakitumia njia hizi kabla ya kuanza kutumia apps za kuwatafuta wapenzi, tunahofu kwamba matumizi yake yanaweza kuzaa tabia hizo,” anaongeza:

“Hapa tunapaswa kutambua madhara ya kutumia apps za wapenzi na mabadiliko ya tabia katika kudhibiti mwonekano wa mwili.”

Anabainisha kuwa ni muhimu kutilia maanani kwamba utafiti huu hauthibitishi mahusiano ya moja kwa moja kati ya apps na tabia zisizofaa kiafya katika kudhibiti uzito.

“Hata hivyo, ni muhimu kwa watumiaji wa apps ambao wanaweza kuwa hatarini kuingia kwenye tabia za kutokula vya kutosha, wakapata msaada kuondokana na tabia hiyo,” anasema. BBC

Habari Kubwa