Watumishi wanaume Z’bar kupewa likizo ya uzazi

22Sep 2016
Rahma Suleiman
Nipashe
Watumishi wanaume Z’bar kupewa likizo ya uzazi

WANAHARAKATI walio mstari wa mbele kudai haki zao kuhusiana na haki za kijinsia, wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanawake dhidi ya wanachokiita ‘mfumo dume.’

Ni mfumo ambao tafsiri yake inasimama kwenye dhana kwamba wanaume wanakuwa mstari wa mbele kuhodhi madaraka na maamuzi mbalimbali ya kijamii.

Inadaiwa kuwa wanaume wanajitoa katika mengi yanayowahusu kama vile mpango wa uzazi na malezi ya familia.

Inaelezwa kuwa wanaume hawajui haki zao na kusababisha baadhi yao kutojua kwamba wana stahili likizo ya uzazi, ili wakae na wake zao wanaojifungua na kuwasaidia katika malezi ya mtoto au watoto.

Sheria ya Utumishi ya Mwaka 2004 ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeweka wazi haki ya wanaume kuchukua likizo ya siku tano, wake wanapojifungua.

Pia, Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2014, inafafanua kwamba kila mtumishi wa umma anayejifungua anaruhusiwa kupewa likizo ya malipo kwa muda wa siku tano za kazi.

Fursa kama hiyo ya likizo kwa mzazi wa kiume imo katika Sheria ya Ajira na Mahusaino Kazini ya mwaka 2004, inayotumika Tanzania Bara.

Sharti lililopo katika sheria hiyo ni kwamba mtumishi anatakiwa kuchukua likizo hiyo ndani ya siku saba tangu azaliwe mtoto na kuambatanishwa taarifa zingine sahihi.

WANAUME WANAJUA?

Khamis Mussa ni mfanyakazi katika Wizara ya Kazi na Uwezeshaji, anayekiri kutofahamu kuwapo likizo ya uzazi na anafafanua:

“Nilikuwa sifahamu kama na sisi wanaume tuna likizo ya uzazi. Nimepata watoto watatu. Lakini, sijawahi kuchukua likizo hiyo hata mara moja na nilikuwa nakuja kazini kama kawaida,” anasema.

Pia anaongeza kuwa suala la likizo ya uzazi kwa wanaume ni la kuzingatiwa na kupewa taarifa sahihi kuhusiana na sheria hiyo, ili waitumie vyema.

Anaahidi kuwa itakapotokea anabahatika kujifungua tena, ataitumia fursa hiyo, ili amsaidie kumlea mtoto hasa katika kipindi hicho kigumu baada ya kujifungua.

“Mimi naweza kusema kuwa ni kosa la mwajiri wangu, kwa kutonielewesha mapema kuhusu Sheria ya Uzazi kwa wanaume na ndio maana, wengi hatuelewi na wala hatuichuki likizo hii,” anasema.

Khamis Ali Haji, ni mwajiriwa wa SMZ, anayekiri hakuwa anafahamu sheria hiyo na alidhani likzo pekee iliyopo ni ya siku 28 za mapumziko ya kila mwaka.

Anasema hadi sasa ana miaka 20 kazini tangu alipoajiriwa na serikali na hajawahi kusikia mtumishi wa kiume anapatiwa likizo ya uzazi.

Hata hivyo, sheria hiyo ya kazi ina miaka 12 ikitumika.

“Zaidi naona wanawake tu wanapotaka kujifungua huwa wanachukua likizo, lakini kwa wanaume ni nadra sana,” anasema Khamis.

MWANAUME MNUFAIKA

Maulid Kassim, ni mtumishi katika Kamisheni ya Kazi Zanzibar, anayesema likizo ya uzazi kwa wanaume ni nzuri na ina faida nyingi, ikiwamo kutoa fursa ya mume kukaa na mke nyumbani kulea kumbe chao kipya.

“Mwanamke huwa ameshabeba mimba miezi tisa, hivyo siku ya kujifungua, huwa anahitaji kupumzika,” anasema.

“Ni jambo la busara mwanaume kuitumia likizo ya uzazi, kumsaidia ulezi na shuguhli za nyumbani ili aweze kupumzika” anafafanua.

”Baadhi ya wanaume, wake zao wanafika kujifungua mtoto hadi mtoto anakuwa, baba hajawahi kumbeba mtoto wake au kumuhudumia mtoto, kumuosha au kumsafisha anapojiasaidia, ” anasema.

“Mimi binafsi nimeshachukua likizo ya uzazi mke wangu alipojifungua mwaka jana, 2015.

“Nilikuwa nyumbani nikimsadia kulea mtoto kwa muda wa siku tano za likizo, bila ya kwenda kazini,” anasema.

Anasema jambo hilo limekuwa la manufaa kwao katika kujua kujua shida anazozipata mama anazozipata na namna ya kumsaidia majukumu ya nyumbani.

Anasema siku tano za likizo ya uzazi kwa mwanaume hazitoshelezi na hivyo kuiomba serikali kuziongeza siku hizo, walau kwa muda wa mwezi mmoja.

Mtumishi huyo wa serikali anakiri hali ngumu anayopata mwanamke katika kipindi cha uzazi na anakuwa na uhitaji wa kusaidiwa.

Ushauri wake kwa wanaume walioko katika utumishi ni kwamba waifuatilie kwa ukaribu sheria hiyo husika kwa kutumia vyema fursa hiyo ya kisheria kusaidia malezi ya wenzao wanapojifungua.

WANAWAKE WAUNGA MKONO

Matha Nassor Khamis, ni mwanamke anayeeleza furajha yake kwa wanaume kupewa likizo ya uzazi, kwani wengi wao baada ya kujifungua huwatelekeza wake zao wakihangaika na ulezi majumbani.

Anasema likizo hiyo, itawasaidia sana kinamama, kwani kuna wanaume wana dhana kwamba, mke anapojifungua, mke hubuni safari ya kukwepa majukumu, lakini anapokuwapo nyumbani, anakuwa na msaada zaidi.

“Kutokana na tabia ya baadhi ya wanaume kushindwa kuwa karibu na watoto wao wanapokuwa wadogo, wanashindwa hata kugundua endapo mtoto atakuwa na matatizo, mama ndio anamgundua mtoto anaumwa au ana njaa,” anasema.

Anawashauri wanaume kuitumia likizo ya uzazi kikamilifu kwa kukaa nyumbani na kusaidia malezi ya mtoto aliyezaliwa.

Leila Mohammed Haji, anasema likizo ya uzazi kwa wanaume ni nzuri, kwa sababu mama anapojifunguwa, anahitaji ukaribu wa mume kumsaidia.

“Likizo ya uzazi ni muhimu, kwa sababu kipindi cha uzazi huwa ni kigumu. Mama aliyejifungua anamhitaji mwenza wake (mume) kumsaidia,” anasema.

Leila anaipongeza SMZ kuweka kanuni hiyo ya likizo ya uzazi kwa jinsia zote, akitaja ina manufaa ya kumfariji mwanamke, hatya pale anapomuona mumewe kamchukua mtoto na kumlea.

KAULI YA SERIIKALI

Ofisa Utumishi katika Wizara ya Kazi Zanzibar, Haji Khamis Haji, anasema licha ya kuwapo sheria ya likizo ya uzazi kwa wanaume, ni asilimia ndogo ya wanaume wanaoifahamu sheria hiyo.

Anasema sheria inatoa fursa hata kwa wanaume wenye wake zaidi ya mmoja, wanapojifungua katika kipindi kimoja, nao wanapata likizo ya uzazi ya siku tano kwa kila mke aliyejifungua.

Hiyo inatoa fursa ya kwenda kumuhudumia mke, kila mmojakwa wakati wake.

Anasema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa watumishi wa umma kuhusu kanuni ya sheria, kuwawezesha wanaume kuchukuwa likizo hiyo inayowahusu.

“Niwashauri watumishi wezangu kuitumia fursa hii ya likizo ya uzazi, ili kuweza kuwasaidia kinamama kipindi ambacho wapo katika hali ngumu ya uzazi,” anasema Ofisa huyo.

Aaongeza:”Kipindi hicho ni
kigumu kwao (kinamama) kutoka katika uzazi, sio kazi rahisi.”

Haji anasema kuwa, serikali iliamua kuweka kanuni hiyo kupitia Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2011, kwa kutambua haki za msingi za kibinadamu, ikiwemo utoaji likizo ya uzazi kwa wanawake wa wanaume.

WAZIRI CASTICO

Waziri wa Kazi,Uwezeshaji,Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Maudline Castico, anasema likizo ya uzazi kwa wanaume, ina manufaa katika kupunguza vitendo vya udhalilishaji wanawake.

Anasema baadhi ya kinamama wanapojifungua, hutelekezwa na waume zao bila ya kuhudumia familia na mzigo wa malezi huwarejea kinamama.

Waziri Castico anasema, wizara yake inanuia kuhakikisha inatoa elimu kwa watumishi wake kuzijua sheria za utumishi na kazi, ikiwamo kipengele cha haki ya likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume, jambo lenye manufaa kwa familia.

“Nitahakikisha siku moja nafanya kikao maalum cha kuwakutanisha watumishi wa umma katika wizara hii, kila mwenye mke au mume kuja naye katika kikao, ili wanawake kuwabana waume zao kuchukua likizo ya uzazi,” anasema waziri huyo.

Anaongeza katika familia, mume na mke wanapokuwa karibu katika kipindi chote cha shida na raha, hujenga bora na imara.

Maudline anawakumbusha watumishi wenziwe na jamii, kwamba mzuri wa kukubalika katika jamii, inaanzia katika familia.
Na kukubalika kwa familia ni kuwa na mshikamano katika vipindi vyote vya shida na raha.

Habari Kubwa