Waundwa mkakati kuwawezesha wafanyakazi, waajiri kujitambua

26Jan 2021
Beatrice Philemon
Dar es Salaam
Nipashe
Waundwa mkakati kuwawezesha wafanyakazi, waajiri kujitambua

CHANGAMOTO za wafanyakazi kutozifahamu haki zao pamoja na masuala ya kupuuza sheria kazini, ni miongoni mwa mambo yanayoifanya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, kuanzisha dawati la kupokea malalamiko yanayohusu kazi na ajira.

Ofisa wa ActionAid, Jovina Nawezake (mwenye kipaza sauti), akizungumzia kazi zenye staha na kuzingatia sheria za kazi kwenye jukwaa la kitaifa lililojadili mustakabali wa ajira nchini. PICHA: BEATRICE PHILEMON

Pamoja na kuwapo dawati hilo, wizara inalenga kuelimisha umma kuhusu haki za wafanyakazi na wajibu wa waajiri, ili waajiriwa wafahamu stahiki zao na waliowaajiri kufuata sheria na taratibu za kazi.

Ofisa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Fred Nyaupumbwe, anasema hayo hivi karibuni kwamba lengo ni kusaidia wafanyakazi kujua na kutumia dawati hilo na pia kufahamu haki zao, kufanya kazi zenye staha na waajiri kufuata sheria za kazi.

Anasema lengo ni kuhamasisha na kuelimisha wafanyakazi kuhusu Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini  pamoja na taratibu za kupata vibali vya kazi kwa wageni wanaoomba kazi nchini, kwa upande wa waajiri.

Ofisa huyo anatoa maelezo hayo kwa maofisa kazi, wafanyakazi kutoka sehemu mbalimbali na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA)  katika mjadala wa kitaifa kuhusu kazi za staha  ulioandaliwa na Shirika la ActionAid Tanzania.

Anasema uelimishaji utafanywa kupitia vyombo vya habari na uelimishaji umma kuhusu dawati la kupokea malalamiko yanayohusu kazi na ajira katika wizara hiyo.

Aidha, anawaambia washiriki kuwa wafanyakazi ndiyo wahusika wakuu na kuwataka watoe taarifa kuhusu changamoto zao iwapo maofisa kazi kutoka idara ya kazi watakwenda  kukagua sehemu za kazi.

“Ili kusaidia wafanyakazi kuwasilisha malalamiko yao, idara ya kazi imetoa namba maalumu ya kutuma au kuwasilisha dukuduku kupitia namba 0655 49489 pamoja na kutuma malalamiko yao kwenye tovuti au anwania ya barua pepe [email protected]” anasema.

Nyaupumbwe anawaambia washiriki kuwa wameamua kujikita katika eneo hilo baada ya kugundua kuwa waajiri na watumishi wengi hawana uelewa wa sheria ya kazi wakati wafanyakazi hawafahamu haki zao katika maeneo yao na kuwahimiza kutumia fursa hiyo ili waweze kufanya kazi katika mazingira bora, kazi zenye staha na kujua haki zao.

Ofisa Kazi kutoka Idara ya Kazi Mkoa wa Pwani, Richard Muhenga, anasema, asilimia kubwa ya waajiriwa na waajiri kwenye sekta binafsi hawana elimu ya kutosha kuhusu sheria ya kazi na uhusiano kazini na hii inasababisha kuwapo migogoro katika maeneo ya kazi.

Mbali na hilo, ingawa maofisa kazi wamekuwa wakitembelea  katika maeneo  mbalimbali ili kufanya ukaguzi viwandani na kwenye kampuni  ili kujua changamoto zinazowakabili wafanyakazi, wengi wanaogopa kutoa taarifa sahihi kuhusu matatizo yanazowakabili katika maeneo ya kazi kwa sababu wanaogopa vitisho na kufukuzwa.

“Tunaomba  ofisa kazi  anapofika kwenye ukaguzi  toeni taarifa sahihi,  msiogope  kufukuzwa kazi ili tujue changamoto  zinazowakabili, tuweze kuzitatua na hatimaye  mfanya kazi zenye staha,” anasema na kuongeza kuwa yote hayo yatafanikiwa kwa kuzingatia sheria na kuheshimu taratibu.

Akizungumzia wawekezaji wanaotoka nje, anawataka kuwasiliana na mamlaka zote zinazohusika bila kutumia mawakala na kuwakumbusha maeneo ya kuwasiliana ni pamoja na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC).

Mamlaka nyingine ni ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa  Mazingira (NEMC), Wakala wa Usalama na Afya Kazini (OSHA), Idara za Uhamiaji, Kazi , TRA pamoja na mamlaka za halmashauri sehemu anayotaka kuwekeza. “Lengo ni kuepusha usumbufu na migogoro baina ya wafanyakazi, waajiri na serikali,”anasema.

Mkuu wa Programu na Sera wa ActionAid, Jovina Nawenzake, akizungumzia suala la kazi zenye staha, anasema ni wajibu wa maofisa kazi kuhakikisha kuwa katika  maeneo yao  ya kazi au wilaya zao kuna kazi za staha  na  pia kusaidia  wafanyakazi kupata stahiki zao bila kujali anafanya kazi wapi.

“Maofisa kazi mwangalie namna gani suala hili litaweza kufanyika katika maeneo yenu kwa sababu wafanyakazi wengi wanapata shida kazini kama halitatimizika basi  muangalie mtafanyaje ukizingatia  sasa taifa limekuwa Tanzania ya viwanda na masuala ya dijitali yamekuwa yakihusisha uvunjwaji wa haki za  watu na kwamba utaongezeka kadri mabadiliko yanavyoongezeka pia,” anasema.

Mbali na hilo, anawaambia wahakikishe kuwa wanaweka mikakati ili watu wafanye kazi zenye  kulinda utu wao,  heshima na wanapata  haki zao na  mafao yenye tija akisema ni jambo hilo ni mtambuka, linahitaji ushirikiano kutoka serikalini na sekta binafsi na kuishauri serikali kuweka mazingira mazuri ya wafanyakazi ili kufanya kazi zenye staha na katika mazingira bora, anakumbusha ofisa huyo.

“ActionAid Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali  ili kusaidia waajiriwa kufanya kazi zenye staha,  pia tunaangalia sera mbalimbali za kuisaidia serikali kupata mapato au kukosa mapato ikiwamo kodi na tunatoa mapendekezo yetu namna gani ya kuboresha sera hizo  ziboreshwe ili serikali iweze kupata mapato,” anasema Jovina.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Jordan University  College- Morogoro, Asifiwe Alinanuswe, anasema kuwa maofisa kazi wafanye ukaguzi  katika maeneo ya kazi  ikiwamo sekta rasmi na  isiyo rasmi kwa sababu huko ndipo kuna  unyanyasaji mkubwa na  haki za wafanyakazi kwani waajiri hazifuati. Tatizo hili tumelibaini kutokana na kesi tunazozipata katika ofisi zetu ukiwamo ukiukwaji wa vipengele vya mikataba, upungufu wa stahiki za kazi, kufukuzwa kazi bila kufuata utaratibu  wa sheria za kazi na masuala mengine mengi.

Anasema: “Maofisa kazi dumisheni utu, heshima na haki za wafanyakazi kwa sababu wafanyakazi wengi katika maeneo ya kazi wanachangamoto nyingi sana, kumbukeni haki za wafanyakazi zinapatikana kwa sheria, washaurini waajiri iwapo wanakiuka sheria.”

Wakizungumzia changamoto zinazowakabili vijana katika maeneo ya kazi wanasema  rushwa ya ngono, kukosa elimu kuhusu mifuko ya hifadhi, mshahara midogo inayochelewa,kukosa mafao ya wafanyakazi, kutofanyika ukaguzi maeneo ya kazi, ubaguzi kazini , wafanyakazi kutoruhusiwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi, kukosa  likizo na stahiki za uzazi ni  baadhi ya changamoto zinazowakabili katika maeneo ya kazi.

Wanasema changamoto hizo walizibaini baada ya kufanya  utafiti na kwamba waajiri wengi hawaruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi  kwa hofu kuwa watajua haki zao na baadae watadai na kupata fidia zao.

Vijana hao wanawaomba maofisa kazi kabla hawajakwenda kukukutana na waajiri, waanzie kwa wafanyakazi kwani ndiyo waonapata matatizo kazini yanayotokana na uvunjwaji wa sheria.

Habari Kubwa