Wavuvi wanavyouhusisha uhaba wa samaki na dhambi

13Nov 2022
Mary Geofrey
Mtwara
Nipashe Jumapili
Wavuvi wanavyouhusisha uhaba wa samaki na dhambi

JANA katika sehemu ya kwanza ya ripoti hii, kulikuwa na ushuhuda wa shida zinazowakabili wavuvi na wachuuzi wa samaki katika Soko la Feri mkoani Mtwara kutokana na uhaba wa samaki uliolikumba eneo lao. Endelea na sehemu ya mwisho kupata undani wa kinachowasibu.

Kilio cha uhaba wa samaki katika Soko la Feri pia kinasikika kutoka kwa Dalali wa Samaki, Said Omary anayebainisha kuwa tangu kuadimika kwa bidhaa hiyo, kipato chake kimeshuka kutoka wastani wa Sh. 100,000 hadi Sh. 40,000 kwa siku.

"Na hii inategemea boti imeenda na kurudi mara ngapi lakini siwezi kulinganisha nilichokuwa ninapata awali na sasa. Miaka ya nyuma nilijenga na nilimudu vizuri kuhudumia familia ila sasa tunapata riziki kidogo," anasema.

Dalali huyo anasema sababu ya kuadimika samaki ni kuwapo anachokitaja mabadiliko ya bahari ambayo chanzo chake ni watu kufanya uharibifu wa kukata miti na uvuvi haramu.

Mfaume Mangoda, mfanyabiashara wa samaki katika kizimba kwenye eneo la soko hilo, anasema samaki wa kilo 2.5 anawanunua kwa Sh. 20,000 na kuuza kwa Sh. 23,000 hadi Sh. 25,000.

"Samaki wameadimika, wavuvi hawana vifaa vya kisasa vya kuvua samaki, serikali ijitahidi kununua boti na meli zinazowezesha uvuvi wa kina kirefu," anashauri.

WAVUVI NA DHAMBI

Mvuvi Abdallah Hamadi (42) anaamini kuwapo dhambi na mambo ya yasiyompendeza Mungu yanayoendelea duniani, kumesababisha Mungu aamue kushusha adhabu ya kuadimika kwa samaki.

"Tuache dhambi, turejee kwa muumba wetu. Yeye ndiye kila kitu kwenye maisha yetu, tusipofanya hivyo, kila kitu kitabadilika maishani mwetu," anaonya Hamadi na kubainisha kuadimika huko kwa samaki kumebadili mfumo wa kipato, kazi yake na maisha kwa ujumla.

Anakumbusha alianza shughuli za uvuvi miaka 22 iliyopita wakati huo walitumia saa moja na nusu hadi saa mbili kwenda na kurudi kutoka baharini kuvua samaki na walikuwa na uhakika wa kupata samaki wa kujaa ndoo 70 zenye ujazo wa lita 10 na kuwauza mnadani, wakigawana Sh. 15,000 hadi 20,000 kila mmoja.

"Kwenye mtumbwi mmoja tunakuwa wavuvi 15 ambao tukishavua na kurudi nchi kavu samaki wanapigwa mnada na hapo unakuta tunagawa kila mmoja kiasi hicho cha fedha  kwa safari moja. Kwa siku tulikuwa na uwezo wa kuondoka na Sh. 70,000 hadi 100,000 kila mmoja.

"Sasa hali ni tofauti kwa sababu tunatumia saa tatu kufika eneo lenye kina kirefu wanakopatikana samaki na kuvua. Kuna wakati hatupati samaki wa kutosha, tunaambulia ndoo tano hadi 10 na kupata Sh. 15,000 hadi 20,000 kila mmoja kulingana na wingi na ukubwa wa samaki tuliopata siku hiyo," anasema.

Mfanyabishara wa Samaki, Aisha Mikidadi anazitaja imani potofu za kishirikina na matukio mabaya ya mauaji ya binadamu yanayofanyika baharini, yanasababisha kuadimika kwa viumbe hao.

Anasema kuwa ili kupata samaki kwa wingi kama ilivyokuwa awali, watu wanapaswa kuacha uovu ili Mungu aachilie baraka zake zilizokuwapo.

"Kila kukicha mauaji, balaa hazipungui, kafara, wanaume wanakuwa kama wanawake na wanawake kama wanaume na mambo mengine ambayo dunia inastaajabu. Kweli bado bahari nayo iwe sawa?" Aisha anahoji.

UONGOZI SOKONI

Mwenyekiti wa Wafanyabishara wa Soko la Samaki Feri, Mwinyi Mzaina anayataja mabadiliko ya tabianchi kuwa kiini cha kuadimika kwa samaki, akifafanua kuwa msimu wanaotarajia kupata samaki kwa wingi, hawawapati lakini wanawapata kipindi ambacho hawana matarajio hayo.

Kiongozi huyo pia anasema ongezeko la wavuvi nalo limechangia kuadimika kwa samaki, akiwasilisha takwimu kwamba sasa Manispaa ya Mtwara inao 1,025 na mkoa mzima wana wavuvi 6,400.

"Kuna ongezeko kubwa la vijana wasio na leseni wanaovua samaki kinyemela, ndiyo sababu samaki kuendelea kupungua kwenye maji ya kina kifupi na kukimbilia maji ya kina kirefu," anasema Mzaina na kutaja hatua wanazochukua zinajumuisha kutoa elimu kwa wavuvi na kuzuia shughuli za uvivu haramu ili kuepuka mabadiliko ya tabianchi yanayoleta athari kubwa.

Ofisa Mazingira Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Tumaini Mosha, anasema samaki wameadimika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

"Haya ni moja ya madhara yake, samaki wameadimika katika eneo la bahari, wanakimbilia maji ya kina kirefu na hivyo wavuvi kukosa mazao ya kutosha ya samaki," anasema na kukiri kuwapo tatizo la uvivu haramu ukiwamo wa kutumia mabomu na hivyo kuua mazalia ya samaki walio katika kina kifupi cha maji.

"Elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi wanaofanya shughuli zao kando ya bahari kuendelea kuitunza na kuepuka shughuli zinazochangia kuwapo kwa tatizo hilo," anasema.

Nipashe pia inatua mezani kwa Ofisa Uvuvi Mkoa wa Mtwara, Emelitha Sauro, anayekiri kuadimika kwa samaki katika eneo hilo la bahari anakokutaja kunachangiwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na ukataji wa miti ya mikoko eneo la bahari na uvuvi haramu. Anasema miti hiyo ni chanjo cha chakula cha samaki.

Katika kukabiliana na uhaba wa samaki mkoani Mtwara, ofisa huyo anasema wamechukua hatua kuhakikisha wavuvi wanakuwa na vyombo vya kisasa vya uvuvi na kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wameweka mipango ya kupeleka boti za kisasa kwa ajili ya wavuvi.

Anasema wanashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambayo imeingia mkataba na wizara kwa lengo la kuwakopesha wavuvi boti za kisasa na kuinua kipato chao huku wakiwataka wavuvi kuachana na mitumbwi ya mbao ambayo hutumia miti mingi kuitengeneza na hivyo, kuendelea kuharibu mazingira.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, kupitia hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha ya Mei mwaka huu, alibainisha sekta ya uvuvi inanufaisha zaidi ya watu milioni 4.5 nchini, huku ikichangia asilimia 1.8 kwenye Pato la Taifa.

Alibainisha kuwa hadi Aprili 30 mwaka huu, tani 34,841.72 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo vipande 169, 089 viliuzwa nje ya nchi na kuliingizia taifa Sh. bilioni 475.01.

Waziri Ndaki pia alibainisha kuwa shughuli za uvuvi nchini zinafanywa zaidi na wavuvi wadogo kwenye maji ya asili, ambao huchangia takriban asilimia 95 ya samaki wote wanaovuliwa nchini kupitia vyombo vya uvuvi vipatavyo 57,991.

Habari Kubwa